SOKO LA NYAMA NJE YA NCHI LAFIKIA TANI 14,701 KWA MWAKA 2023/2024
Na Gustaphu Haule,Tanzania
*● Ni matunda ya ushirikiano mzuri na Mataifa ya nje*
#KAZIINAONGEA
KUFUATIA jitihada zinazofanywa na Rais wa awamu ya sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ushirikiano na Mataifa mbalimbali Duniani, juhudi hizo zimesaidia pia kwa upande wa Kibiashara kuhamasisha upatikanaji wa masoko ya nyama nje ya nchi.
Ushirikiano huo wa Dkt. Samia umechangia kwa kiasi kikubwa kupanda kwa mauzo ya nyama nje ya nchi kutoka tani 10,415 kwa mwaka 2021/2022, tani 12,243 kwa mwaka 2022/2023 hadi kufikia tani 14,701 kwa mwaka 2023 hadi 2024.
Matokeo hayo yameonyesha kuimarika kwa ufugaji wa kisasa na uzalishaji wa nyama, kunakopelekea kuongeza kipato kwa wafugaji na ajira kwa Watanzania.
Jithada za Dkt. Samia zimewezesha masoko ya nyama nje ya nchi, kuendelea kuongezeka na kuzifikia nchi 12 ambazo ni Bahrain, Comoro, Hong Kong, Jordan, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Rwanda, Saudi Arabia, UAE na Vietnam ambapo hadi kufikia Aprili 2024, ongezeko la mauzo ya nyama nje ya nchi limefikia takribani Shilingi Bilioni 100.
Akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi na makabidhiano ya Kituo atamizi cha ufugaji wa kibiashara kwa Vijana kilichopo Kongwa Mkoani Dodoma Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa, kituo hicho maalumu kwa ajili ya unenepeshaji wa mbuzi kimegharimu Shilingi bilioni 1.6.
Amesema, nyama ya mbuzi imeendelea kuongoza katika mauzo ya nyama nje ya nchi ambapo imechangia asilimia 70.1 ya mauzo yote na kwamba hali hii inathibitisha kwamba mradi huu una manufaa makubwa ya kiuchumi katika nchi yetu kwa kuwa nyama ya mbuzi ina uhitaji mkubwa ndani na nje ya nchi.
Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa vijana kuitumia fursa ya uwepo wa kituo hicho kwa manufaa yao binafsi na manufaa ya Taifa kwa ujumla.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua machinjio ya Nyama huko Kongwa Mkoani Dodoma katika hafla ya uzinduzi wa machinjio hayo iliyofanyika hivi karibuni.
Lengo la mradi huo ni kuwapatia vijana ujuzi kwa vitendo ikiwemo elimu ya ujenzi wa mabanda, ulishaji, matibabu na usimamizi wa mradi wa ufugaji mbuzi lakini pia kutoa mafunzo ya biashara ili wawe wajasiriamali na waweze kuendeleza biashara ya unenepeshaji mbuzi.
Ametoa wito kwa wafanyabiashara na wasindikaji wa nyama washirikiane na kituo hicho ili kupunguza changamoto ya upatikanaji ya mifugo bora kwa ajili ya uzalishaji wa nyama na mazao yake.
Machinjio mapya ya Nyama yaliyozinduliwa juzi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo, Abdallah Ulega amesema kuwa sekta ya mifugo inawahitaji sana wadau, wafugaji, wafanyabiashara, walaji na watoa huduma za afya katika kuongeza tija na kuongeza uzalishaji na kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepanga kukifanya Kituo Atamizi cha Ufugaji kilichopo Kongwa, kuwa kituo kikubwa kwa ajili ya ufugaji na unenepeshaji wa mbuzi nchini.
Kituo hicho kilichokuwa kikisimamiwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya PASS kimekabidhiwa kwa Serikali na kitakuwa chini ya uangalizi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TARILI).
#KAZIINAONGEA




Comments
Post a Comment