SHAURI YOMBAYOMBA :LAMI KUANZA JANUARI ,NIPENI KURA MZIDI KUFURAHI


Na Gustaphu Haule,Kibaha

MGOMBEA wa nafasi ya mwenyekiti katika Mtaa wa Mailimoja" B" uliopo Kata ya Tangini katika Halmashauri ya Mji Kibaha Shauri Yombayomba amewaomba wakazi wa Mtaa huo kuendelea kumuamini katika miaka mitano ijayo.

Shauri, ametoa ombi hilo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wake wa kampeni uliof: anyika katika viwanja vya kanisa la TAG lililopo Mtaa wa Mailimoja "B"

Katika mkutano huo Yombayomba amesema kuwa miaka mitano ya kwanza walimuamini na kumchagua lakini alifanyakazi kubwa ya kufungua barabara ambazo miaka mingi hazikupitika.

Amesema, awamu hii wakimchagua kasi ya maendeleo itakuwa kubwa ikiwa pamoja na kuendeleza zoezi la kufungua barabara za Mitaa ambazo kwasasa hazipitiki na hivyo kuleta changamoto kwa Wananchi.

Ameongeza kuwa ,mbali na kufungua barabara hizo lakini pia Mtaa wake umefanikiwa kupata barabara za lami ikiwemo kutoka kwa kwa Malata kupitia Mailimoja Pharmacy mpaka kufika katika ofisi ya Mtaa na kuunganisha Minazini.

Yombayomba, amesema kuwa barabara nyingine ni kutoka Mailimoja stendi ya zamani kupitia barabara ya Kontena - Msikiti wa Al-qaida na kuunganisha barabara inayotoka ofisi ya Serikali ya Mtaa na kwenda Minazini.

Amesema kuwa, sio mwisho kwani hata barabara ya Malata kupitia KCC kwenda Loliondo nayo itapata lami na hivyo kufanya Mtaa kupitika kirahisi wakati wote.

Amesema barabara hizo zitaanza Kutengenezwa Januari 2025 na kwamba hatua hiyo ni matunda ya kazi iliyofanyika ndani ya miaka mitano ya uongozi wake .

"Naombeni Novemba 27 kesho kutwa  twende tukapige kura kukichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye mgombea wake ni mimi Shauri Yombayomba lakini nipeni na wajumbe wangu wote ili tukapate urahisi wa kufanyakazi ndani ya Mtaa wetu,"amesema Yombayomba 

Mgeni rasmi katika kampeni hiyo ni Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo Clement Kagaruki ambaye amewataka Wananchi wote kuchagua wagombea wa CCM .


Diwani wa viti maalum Kibaha Mjini Selina Wilson amewataka Wananchi hao kuacha kudanganywa na wapinzani kwani CCM ndio Chama pekee kinacholeta maendeleo .

Amewaomba wananchi kuungana kwa pamoja Novemba 27 ili kwenda kuwachagua wagombea wa CCM kwakuwa ndio watekelezaji ilani ya uchaguzi.

Mwisho.


Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA