SERIKALI YA SAMIA YAJA NA MKAKATI WA KUBORESHA BARABARA RUKWA



 


Na Gustaphu Haule,Tanzania

#KAZIINAONGEA

SERIKALI ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekuwa ikifanya jitihada  za kuimarisha na kuboresha miundombinu ya barabara ili kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuzilinda ziweze kutumika kwa muda mrefu.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Rukwa Mhandisi Chacha Moseti amesema, Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia imefanya kazi kubwa katika kuimarisha mtandao wa barabara ili uweze kupitika kwa misimu yote kwa kutenga fedha mwaka hadi mwaka.

“Tunamshukuru Rais Samia kwa kuongeza bajeti ya TARURA Mkoa wa Rukwa kutoka shilingi bilioni 5.1 hadi kufikia shilingi bilioni 12.9, kwa kiasi kikubwa imesaidia kuimarisha mtandao wa barabara katika mkoa wetu”, amesema Moseti

“Kupitia ongezeko hilo TARURA mkoa wa Rukwa inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kwa kufungua barabara mpya ili kufika kusiko fikika na kuboresha barabara zilizopo ili zipitike wakati wote”, ameongeza.

Amesema, barabara za lami zimeongezeka kutoka Kilomita 29.33 na kufikia Kilomita 43.14 ambazo ni sawa na ongezeko la Kilomita 13.81%, wamejenga barabara za zege Kilomita 0.631, barabara za changarawe Kilomita 480.76 na ujenzi wa madaraja na maboksi kalavati 147.


Ameeleza kuwa wameweza kuongeza idadi ya madaraja na kufungua maeneo yaliyokuwa hayafikiki na sasa yanafikika muda wote kwa kujenga madaraja 17 kwa kutumia teknolojia ya mawe katika Halmashauri za Wilaya ya Sumbawanga, Kalambo na Nkasi.



Ameongeza kuwa, wametekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa daraja la mto Kalambo lenye urefu wa mita 80 ambalo limenufaisha wananchi wa kata za Sopa na Pombwe wilayani Kalambo kusafirisha mazao yao sokoni kwa urahisi.

Mkazi wa Nkasi Sarafina Mbalamwezi, ameipongeza Serikali kwa kile inachokifanya kuhakikisha miradi ya barabara inatekelezwa na kukamilika kwa wakati na wananchi kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma mbalimbali ikiwemo ya matibabu.

Mkazi wa Sopa wilayani Kalambo Amon Kabwe amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kuboresha miundombinu vijijini ili kuhakikisha wananchi wanasafiri na kusafirisha mazao yao sokoni kwa urahisi.

TARURA Mkoa wa Rukwa  inahudumia mtandao wa barabara wenye urefu wa Kilomita 2,304.26 ambapo kati ya hizo barabara za lami ni Kilomita 44.3, barabara za changarawe Kilomita 1,145.68 na barabara za udongo Kilomita 1,114.28.

#KAZIINAONGEA

Club News Editor - Charles Kusaga

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA