RC - PWANI AWAONGOZA WANANCHI KUPIGA KURA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA
Na Gustaphu Haule,Pwani
Club News Editor - Charles Kusaga
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge mapema leo saa 2:15 asubuhi amewaongoza wakazi wa Mkoa wa Pwani kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa watakaokaa madarakani kwa muda wa miaka mitano ijayo.
Kunenge,amepiga kura katika Mtaa wa Mkoani "A" uliopo Kata ya Tumbi Halmashauri ya Kibaha Mjini ambapo pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa hali ya Mkoa wa Pwani kiusalama ipo shwari.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge watano mwenye shati ya bluu akipanga mstari kwa ajili ya kupiga kura kuwachagua viongozi wa Serikali ya Mtaa leo Novemba 27 katika kituo cha Mkoani "A" kilichopo Kata ya Tumbi Kibaha Mjini.
Amesema, uchaguzi huo ni muhimu kwani unakwenda kutoa viongozi ambao watahudumia Wananchi kwa ukaribu zaidi kwa ajili kuleta maendeleo hivyo ni vyema kila mwananchi ajitokeza kutimiza haki yake ya kikatiba.
Amesema, muda wa kupiga kura ni kuanzia saa 2 asubuhi mpaka saa 10 jioni na kwamba muda ukimalizika watu waliopo katika foleni wote watapiga kura bila usumbufu wowote .
Baadhi ya Wananchi wakipiga kura kuwachagua viongozi wa Serikali ya Mtaa katika kituo cha Mkoani "A" Kata ya Tumbi Kibaha Mjini Mkoa wa Pwani
"Nawaomba wakazi wa Mkoa wa Pwani wajitokeze kupiga kura kwani inachukua dakika moja au tatu na hii itakufanya wewe mwananchi kutimiza haki yako ya kikatiba ya kuchagua kiongozi wako wa Mtaa ,"amesema Kunenge
Aidha, Kunenge ameongeza kuwa Serikali ya Mkoa imejipanga vizuri kusimamia uchaguzi kwani vyombo vyote vya usalama vipo kila sehemu huku akiwahakikishia Wananchi waende kupiga kura wakiwa na amani kwani vituo vipo salama.
Hatahivyo, Kunenge amemshukuru Rais wa awamu ya Sita Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa siku ya kupiga kura kwa kufanya maamuzi sahihi ya kuweka mapumziko ili kila mmoja ashiriki kupiga kura.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipiga kura kwa ajili ya kuchagua viongozi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mtaa katika kitongoji cha Sokoine, Chamwino mkoani Dodoma tarehe 27 Novemba, 2024.
"Maamuzi ya Rais Samia ni mazuri kwani yamesaidia kutoa fursa kwa Wananchi kutimiza haki yake ya kupiga kura hivyo ni vyema Wananchi wote kwa pamoja wakaungana na Rais Samia katika kuhakikisha adhma ya kuweka mapumziko siku ya leo inatimia", amesema Kunenge.
Comments
Post a Comment