RC KUNENGE: ZIARA ZA RAIS SAMIA NCHI MBALIMBALI DUNIANI ZALETA MAFANIKIO, APOKEA WAWEKEZAJI 23 KUTOKA CHINA,WAKUBALIANA MAZURI.



Na Gustaphu Haule, Tanzania 

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa ziara alizofanya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt . Samia Suluhu Hassan katika nchi mbalimbali duniani zimeanza kuleta mafanikio makubwa katika Mkoa wake kwakuwa tayari ameanza kupokea wageni wanaotaka kuwekeza katika maeneo mbalimbali.

Kunenge amesema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari mara  baada ya kikao kifupi na wageni 23  kutoka Jimbo la Jilin lililopo nchini China ambao wametembelea Mkoa huo.

Wageni kutoka Jimbo la Jilin lililopo nchini China pamoja na sekretarieti ya Mkoa wa Pwani katika kikao cha pamoja cha kuangalia fursa za uwekezaji zilizopo ndani ya Mkoa wa Pwani ,kikao hicho kimefanyika leo Novemba 8 katika ofisi za Mkuu wa Mkoa  zilizopo Mjini Kibaha 

Kunenge, amesema lengo la ziara ya wageni  hao kutoka China ni kuangalia fursa za maeneo ya uwekezaji ikiwa ni baada ya kushawishika na uhamasishaji uliofanywa na Rais Samia alipokwenda nchini kwao na kukutana na Rais wa China hivi karibuni.

"Ninatumia fursa hii kumshukuru Rais Samia kwa ziara yake aliyoifanya nchini China hivi karibuni kwani leo tumeona mafanikio yake ya kupokea wageni wengi kutoka Nchini China waliokuja kwa nia ya kuangalia fursa za uwekezaji," amesema Kunenge 

Kunenge amesema kuwa katika kikao hicho cha pamoja  wamekubaliana kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali ya uwekezaji ambapo kutakuwa na mkataba wa maalum wa makubaliano kwenye uwekezaji wa maeneo yatakayowekezwa.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza katika kikao cha pamoja na wageni kutoka Nchini  China waliokuja kuangalia fursa uwekezaji zilizopo katika Mkoa wa Pwani.

" Kabla ya kuja hapa nchini na katika Mkoa wetu walifanya utafiti na kubaini Pwani ni Mkoa unaoongoza kwa uwekezaji wa viwanda, tumewaambia tunachotaka ni kuwa na uwekezaji wenye tija na sisi tutajifunza kutoka kwao," ameongoza Kunenge 

Mkuu huyo wa Mkoa amesema mbali ya ukaribisho uliofanywa na Rais Samia pia sera za nchi ni moja ya vitu vilivyowavutia raia hao kuja nchini kwa ajili ya kufanya uwekezaji.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge( Kulia) akibadilishana hati ya makubaliano ya  uwekezaji na makamu mwenyekiti wa kamati ya maendeleo katika Jimbo la Jilin  lililopo nchini China Gao Guangbin ( kushoto)katika kikao maalum kilichofanyika leo Novemba 8 Mjini Kibaha.

Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa kamati ya watu wa Jimbo la Jilin lililopo nchini China ambaye pia ndiye kiongozi wa msafara huo  Gao Guangbin, amesema kuwa ujio wao Mkoa wa Pwani umetokana na ushirikiano wa nchi mbili ikiwemo Tanzania na China 

Makamu mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya maendeleo katika Jimbo la Jilin lililopo nchini China Gao Guangbin akizungumza katika kikao maalum na uongozi wa Mkoa wa Pwani kuhusu ziara yao ya kuangalia fursa za uwekezaji iliyofanyika leo Novemba 8 katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Guangbin, amesema kuwa Rais wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amekuwa Rais mwenye kuendeleza ushirikiano mzuri na amekuwa akitangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika nchi yake ndio maana na wao wamekuja kuangalia fursa zilizopo.

Amesema, kufanya ziara hiyo Mkoa wa Pwani haikuwa bahati mbaya kwani kwa muda mrefu kumekuwa na wawekezaji wengi kutoka China ambao wanafanya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali katika Mkoa wa Pwani ambao umekuwa na fursa nyingi za uwekezaji.


Ameongeza kuwa, pamoja na mambo mengine China inaushirikiano mkubwa na Afrika na Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikishirikiana kwa ukaribu na China katika kufanya uwekezaji mbalimbali.


"Tanzania ni nchi nzuri kwa China katika kufanya uwekezaji ndio maana kila siku tunakuja kwa ajili ya kuangalia fursa zaidi na Mkoa wa Pwani ndio sehemu pekee ambayo imekuwa na mvuto mzuri wa uwekezaji kwakuwa bidhaa tunazozalisha zinakuwa na Soko kubwa na zinapendwa watu,"amesema Guangbin.

Awali Katibu Tawala Msaidizi wa uchumi na Uzalishaji Shangwe Twammala, amewaambia wageni hao kuwa Mkoa wa Pwani bado kuna ardhi ya kutosha na inayofaa kwa uwekezaji katika  nyanja mbalimbali ikiwemo ujenzi wa viwanda,Uvuvi, Kilimo, Utalii na Sekta nyingine.

Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Pwani Shangwe Twammala akiwasilisha mada katika kikao cha pamoja na wageni kutoka Nchini China waliokuja Mkoani humo leo Novemba 8 kwa ajili ya kuangalia fursa za uwekezaji ndani ya Mkoa huo.


Twammala amesema kuwa kwa upande wa viwanda Mkoa wa Pwani umekuwa ukiongoza ambapo mpaka kufikia Machi mwaka huu Mkoa ulikuwa na viwanda 1,535 vilivyosaidia kutoa ajira za kudumu na muda mfupi zaidi ya 18000.

Hatahivyo, kikao cha pamoja na wageni hao kimehudhuriwa pia na  Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta, sekretarieti ya Mkoa, baadhi ya Wakuu wa taasisi za Serikali ikiwemo Ruwasa na Tanroads na wakuu wa idara kutoka Halmashauri ya Mji Kibaha akiwemo Leah Lwanji.



Club News Editor - Charles Kusaga

Comments

Popular posts from this blog

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA

RC PWANI AFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MKURUGENZI WA KIBAHA MJINI DKT.ROGERS SHEMWELEKWA