RAIS SAMIA APELEKA NEEMA MKOANI TABORA, AIDHINISHA SH. BILIONI 19 KUSAMBAZA UMEME VITONGOJI 180



Na Gustaphu Haule,Tanzania
 KAZIINAONGEA
 
SERIKALI ya awamu ya Sita kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatekeleza mradi wa Sh.bilioni 19 wa kusambaza umeme katika vitongoji 180 utakaonufaisha Kaya 5,940 Mkoani Tabora.
 
Hayo yameelezwa na msimamizi wa miradi ya REA Kanda ya Magharibi, Mhandisi Robert Dulle Novemba 07, 2024 Mkoani Tabora mbele ya Mkuu wa Mkoa huo Paul Chacha wakati wa kumtambulisha mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo Kampuni ya Sinotec Company Ltd kutoka nchini China.

“Napenda kuwafahamisha wananchi wa Tabora kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ameridhia kiasi cha Sh.19,057,015,682.55 kitumike kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 180 mkoani hapa na leo hii tupo hapa kumtambulisha mkandarasi anayetekeleza mradi huu,” amesema Dulle.
 
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha amemuelekeza mkandarasi kuhakikisha anakamalisha kazi hiyo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa na amepongeza REA kwa kuendelea kutimiza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo.
 
Akielezea utekelezaji wa mradi, Mhandisi Dulle amesema mradi huo unatekelezwa ndani ya Majimbo yote 12 ya mkoani humo na kwamba unatekelezwa kwa muda wa miaka miwili na utakamilika Mwezi Agosti, 2026 ambapo kila jimbo vitongoji 15 vitanufaika.
 
Mhandisi Robert Dulle Msimamizi wa miradi ya REA Kanda ya Magharibi, akielezea mradi kwa Waandishi wa habari

Amefafanua kuwa  hadi sasa vitongoji vilivyosambaziwa umeme ni vitongoji 1,323 kati ya vitongoji 3,749 na kwamba vitongoji vitakavyosalia vitasambaziwa umeme kulingana na upatikanaji wa fedha.
 
Mhandisi Dulle amesema mradi umelenga kusogeza miundombinu ya umeme kwa wananchi katika majimbo yote ili waweze kunufaika na nishati ya umeme katika kujiletea maendeleo hasa katika kuongeza thamani ya mazao, ufundi seremala, viwanda vidogo vidogo, mashine za kusaga na kukoboa sambamba na shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.
 


“Vitongoji vitakavyonufaika ni kutoka katika Majimbo ya Sikonge, Urambo, Igalula, Tabora Kaskazini, Kaliua, Ulyankulu, Bukene, Nzega Vijijini, Nzega Mjini, Igunga, Tabora Mjini na Manonga ambapo kila jimbo litapata vitongoji 15, Mashine umba 15 na wateja 495 na msongo mdogo (LV) umbali wa kilomita 30,” amefafanua Mhandisi Dulle.
 
Amesisitiza kuwa gharama ya kuunganishiwa umeme kwa wananchi ndani ya vitongoji hivyo ni Sh. 27,000 na kwamba mradi hautakuwa na fidia.
 
Mhandisi Dulle amesisitiza kuwa Wakala kwa kushirikiana na TANESCO unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali nchi nzima pamoja na kuwasimamia kwa karibu wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi na kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliopangwa ili iweze kuwanufaisha wananchi kama ilivyo dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
 



Naye Meneja wa Mradi kutoka Kampuni ya Sinotec Company Ltd, Mhandisi Alphred Kessy amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa watakamilisha mradi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Club News Editor - Charles Kusaga

Comments

Popular posts from this blog

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA

RC PWANI AFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MKURUGENZI WA KIBAHA MJINI DKT.ROGERS SHEMWELEKWA