UCHAPAKAZI WA MWANTUMU RAJABU ULIVYOMPA USHINDI KURA ZA MAONI



Na Gustaphu Haule,Pwani

YAANI mimi wakati napokea Kitongoji miaka yangu mitano ya kwanza sijakuta hata meza ya kuandikia lakini nikapambana nikapata viti na meza angalau kwasasa tunavifaa .

Ikawa haitoshi, baada ya kupata viti na meza baadae nikapambana tena nikafanikiwa kununua kiwanja cha kujenga ofisi yetu ya Kitongoji.

Hayo ni maneno ya Mwantum Rajabu mgombea wa nafasi ya uenyekiti katika Kitongoji cha Kambini kilichopo Kijiji cha Vigwaza Kata ya Vigwaza katika Halmashauri ya Wilaya Chalinze Bagamoyo Mkoani Pwani.
Mwantum ambaye kwasasa ni mama mwenye umri wa miaka 46 na mwenye mtoto mmoja tayari ameteuliwa kugombea nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM ).

Katika mahojiano na mwandishi wa makala haya,Mwantum anasema kuwa kwasasa ni mara yake ya pili kugombea nafasi ya kuwa mwenyekiti wa Kitongoji cha Kambini.

Mwantum,anasema alianza harakati za kugombea nafasi za uongozi mwaka  2014 ambapo akiwa katika Kitongoji hicho aligombea nafasi ya kuwa mjumbe wa Serikali ya Kitongoji cha Kambini na kufanikiwa kushinda nafasi hiyo.
Mwantum Rajabu wa kwanza aliyefunga shungi akiwa katika moja ya kikao cha shughuli za kijamii katika Kitongoji cha Kambini Kijiji cha Vigwaza Chalinze Mkoani Pwani 


"Mwaka 2014 niligombea ujumbe wa Serikali ya Kitongoji cha Kambini na nikafanikiwa lakini ilikuwa nafasi ambayo ilinipa umaarufu mkubwa kutokana na kufanya kazi karibu na jamii,"anasema Mwantum 

Anasema akiwa mjumbe wa Serikali ya Kitongoji hicho alipata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ya kiuongozi jambo ambalo lilimpa ujasiri na kujiamini katika kugombea nafasi nyingine ya juu.

Anasema kuwa,ilipofika mwaka  2019 aliamua kupanda na kugombea nafasi ya kuwa mwenyekiti wa Kitongoji cha Kambini na hatimae kushinda katika uchaguzi wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mwantum, anasema uchaguzi wa ndani ya Chama aligombea na wenzake wanne ambapo kati yao wanaume walikuwa watatu na mwanamke mmoja lakini alifanikiwa kushinda kwa kura nyingi.

Ushindi wake ndani ya CCM ulimpa nafasi kubwa ya kuwa mwenyekiti wa Kitongoji kwani hata katika uchaguzi wa Serikali alishinda kwa kishindo na  kuwa mwenyekiti aliyeongoza kwa muda wa miaka mitano mpaka ilipofika 2024.

Aidha mgombea huyo anasema katika uchaguzi wa mwaka huu ndani ya Chama chake hakuna mgombea mwingine yeyote aliyechukua fomu zaidi yake kwani amepita peke yake bila kupingwa.

"Safari hii ndani ya Kitongoji changu hakuna mgombea aliyechukua fomu kwakuwa wote waliamua mimi niendelee kuwaongoza ndani ya miaka mitano mingine"amesema Mwantum

Mwantum, ameongeza kuwa sababu ya yeye kugombea mwenyewe ni mapenzi ya Wananchi wake juu ya yale aliyoyafanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita huku akisema uenda wamekuwa na matumaini makubwa juu yake.

Ameongeza kuwa, katika kipindi cha uongozi wake wa miaka mitano iliyopita Mwantum mbali na kununua kiwanja cha kujenga ofisi, meza na viti lakini yapo mengine mengi ameyafanya kwa Wananchi wake.

Mgombea huyo anasema amefanikiwa kutatua changamoto nyingi za Wananchi wake ikiwemo kutatua kero za migogoro ya ardhi, kuwasaidia shida ndogo ndogo za kiuchumi na hata kushiriki katika shughuli za kijamii kama vile sherehe,ugonjwa na hata misiba.
Mwantum Rajabu mgombea wa nafasi ya uenyekiti katika Kitongoji cha Kambini kilichopo Kijiji cha Vigwaza Kata ya Vigwaza katika Halmashauri ya Wilaya Chalinze Bagamoyo Mkoani Pwani.

"Vitu ambavyo nimevifanya kwa Wananchi nahisi vimesababisha wanipende na kuamua kunipa nafasi nyingine maana hata hizo meza na viti nilivyonunua vimetusaidia katika vikao vyetu ",amesema Mwantum

Je,ni changamoto gani umepitia katika miaka mitano ya kwanza ya uongozi wako?

Mwantum anasema changamoto katika uongozi ni kawaida licha ya kuwa amejitahidi kupambananazo huku akitaja kuwa maneno ya kejeli yamekuwa mengi kwakuwa tu yeye mwanamke.

Anasema pamoja na changamoto hiyo lakini ameweza kupambana kwa kushirikisha Wananchi katika makundi mbalimbali na ndio maana hapakuwa na ugumu sana katika kutekeleza majukumu yake.

Je,Mwantum unapataje msaada kutoka kwa Mume wako ?

Niseme tu mume wangu ni mtu wa kutafuta ,inapofika asubuhi uondoka nyumbani na kwenda kutafuta lakini kwangu amekuwa na msaada kwakuwa siku ninapotaka kwenda katika shughuli zangu za kuwahudumia Wananchi huwa ananipa nauli.

Lakini hata nilipotaka kugombea Kwa awamu ya kwanza nilipomwambia hakukataa kwani alinipa ushirikiano mzuri na kuniruhusu kugombea na sasa mambo yanaenda vizuri tena kwa ushirikiano mkubwa ,"anasema Mwantum

Wewe ni mama na pia ni kiongozi, unapangaje ratiba yako ya kulea familia na kuhudumia Wananchi?

Anasema nikitoka asubuhi naenda kwenye shughuli zangu za kujitafutia kipato na kama kuna dharula 
au ofisini napita ofisini nawasaidia wananchi nikimaliza naenda kuendelea na kazi zingine lakini kuhusu watoto asubuhi wanaenda Shule na wakirudi kama sijarudi nyumbani watoto wanaenda Kwa bibi na mimi nikirudi nawapitia ndipo tunarudi nyumbani kwa ajili ya kupika.

Je,unaweza kuweka bayana sababu zinazowakwamisha Wanawake kutokugombea nafasi za uongozi?

Katika hili Mwantum anasema kuwa Wanawake wengi wanashindwa kugombea kutokana na kukataliwa na waume zao.

Anasema kuwa,wapo Wanawake wanapenda kugombea lakini wanapowaeleza waume zao hukataa na hivyo kufanya ndoto zao kuishia njiani japo anasema wakati mwingine ni uoga wa Wanawake wenyewe.

Unatoa ushauri gani kwa Wanawake wenzio?

Mimi ni mwanamke tena nimegombea mara mbili sasa hivyo nawashauri Wanawake wenzangu kuchangamkia fursa za uongozi pale zinapotokea kwakuwa haki ya kugombea ni ya kila mtu.

Anasema kuwa ,kwasasa amekuwa akiwashawishi Wanawake kugombea Kwa kutumia mbinu mbalimbali huku akisema mbinu ya kwanza ni kuunda majukwaa ya akina mama na kuwapa uongozi .

"Nimeunda majukwaa ya Wanawake ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na katika majukwaa hayo nimechagua wana wake wawe viongozi ambapo kupitia majukwaa hayo huwa nawafundisha namna ya wao kuwa Viongozi,"anasema Mwantum.

Vipi kuhusu miaka mitano hii ukichaguliwa utafanya nini?

Nina mambo mengi ya kufanya kipindi hiki endapo Wananchi wangu watanichagua kwani nataka kuleta mabadiliko makubwa.

Anasema, jambo kubwa ambalo anataka kufanya ni kuhakikisha Kitongoji cha Vigwaza kinapata ofisi yake ili shughuli zote zifanyikie ofisini tofauti na sasa ambapo kazi za kiofisi zinafanyika nyumbani kwake au barabarani.

"Viti nimenunua ,meza nimenunua lakini hatahivyo tumekuwa tukifanyia vikao nje ya nyumba yangu mpaka miaka mitano imeisha ila kama nitachaguliwa nitaendelea kushirikiana na wananchi wangu ili tuhakikishe tunapata ofisi yetu",amesema Mwantum 

Anasema, kwakuwa ameshapata kiwanja cha ofisi kazi iliyobaki ni kujenga huku akibainisha kuwa mpaka sasa tayari amenunua matofali 270,saruji mifuko Nane na nondo moja.

Mwantum, anasema siku akitangazwa kuwa mshindi kazi ya kwanza ni kuendelea na mipango yake ya kujenga ofisi kwakuwa anataka kuona miaka mitano hii anakamilisha ndoto yake ya kupata ofisi pamoja na kufanya mambo mengine ya kimaendeleo.

Je,una ndoto gani za baadae au unataka kuishia katika nafasi hii ya mwenyekiti wa Kitongoji?

Daaah! Sitaki kuishia kuwa mwenyekiti wa Kitongoji lakini hapa nipo najifunza huko baadae nitaangalia kama naweza kusongambele kwenye nafasi ya uenyekiti au kuingia Chama,"anasema 

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Vigwaza Amiri Rashid anasema kuwa Kata ya Vigwaza inajumla ya Vitongoji 53 lakini kati ya hivyo Wanawake wagombea ni 14.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ,Vijiji na Vitongoji unatarajia kufanyika Novemba 27 mwaka huu nchini kote ambapo Mwantum Rajabu ni mmoja kati ya Wanawake wanaogombea nafasi ya mwenyekiti wa Kitongoji cha Vigwaza .



Club News Editor





Comments

Popular posts from this blog

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA

RC PWANI AFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MKURUGENZI WA KIBAHA MJINI DKT.ROGERS SHEMWELEKWA