KUTANA NA SIMULIZI YA ZAMDA MTENDE MWANAMKE ALIYEPANIA KUFANYA MAKUBWA KITONGOJI CHA MLANDIZI MJINI


Na Gustaphu Haule,Pwani

NI Mwanamke jasiri, hodari na shupavu  aliyejitoa kwa ajili ya kuwapigania Wananchi kwa kuwatatulia kero zao na hata kuleta maendeleo ya  Kitongoji cha Mlandizi Mjini .

Huyu si mwingine bali ni Zamda Mtende(48) mama wa watoto watatu ambaye kwasasa ni mgombea wa nafasi ya mwenyekiti Kitongoji cha Mlandizi Mjini katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani.


Zamda kiuzoefu ni mwanasiasa nguli anayetokana na Chama Cha Mapinduzi ( CCM)ambaye amebahatika kushika nafasi mbalimbali katika chama hicho ikiwemo ya kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Kata ya Mlandizi.

Zamda amekuwa mwenyekiti wa UWT kwa vipindi viwili mpaka hivi sasa mahali ambapo amejipatia uzoefu mkubwa wa kiuongozi na hata kupata umaarufu katika Kitongoji chake.

Tunamtaja Zamda Mtende kama darasa na kioo kwa Wanawake wenzake kutokana na historia yake ya kiuongozi toka mwaka 2014 wakati alipoingia katika masuala ya Siasa.

Zamda Mtende (wa pili kutoka kulia)  akiwa na Wanawake wenzake katika moja ya shughuli za kijamii katika Kitongoji cha Mlandizi Mjini Kibaha Vijijini.

 Novemba 14 mwaka huu Mwandishi wa makala haya alipata fursa ya kuzungumza kwa kina  na mgombea huyo, na mazungumzo yetu yalikuwa hivi,

Zamda Mtende wewe ni nani?

Mimi ni mama niliyeolewa  na kubahatika kupata watoto watatu lakini licha ya kuwa na nafasi ya UWT lakini kwasasa ni mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa Kitongoji cha Mlandizi Mjini ninaye kwenda kupigiwa kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa,Vijiji na Vitongoji hapo Novemba 27 mwaka huu.

Je, harakati za masuala ya kiuongozi umezianza lini na nini uzoefu wako kwa nafasi unayogombea?
 
Niseme tu ,harakati za uongozi nimeanza kitambo sana na kihistoria nakumbuka Kitongoji cha Mlandizi Mjini kilizaliwa mwaka 2014 wakati huo Kata ya Mlandizi  ilikuwa na Vitongoji viwili kikiwemo Saidi Domo na Mlandizi Mjini kwahiyo wakati vinagawanywa mimi nilikuwa mjumbe wa Serikali ya Kitongoji.

Lakini vilipogawanywa mwenyekiti wangu Mwasiti Pembe akagombea na mimi nikawa mjumbe wa Serikali ila wakati nikiwa mjumbe pia nilikuwa nafanyakazi kama Katibu wa mwenyekiti wa Kitongoji na imeendelea hivyo mpaka mwaka 2019.

Ilivyofika  mwaka 2019 mwenyekiti wangu akagombea tena na akapita bila kupingwa kwakuwa wakati huo wapinzani hawakuchukua fomu na mimi nikaendelea kuwa Katibu .

Nimekuwa katibu tangu 2019 na ilipofika Oktoba 10,2020  mwenyekiti wangu Mwasiti Pembe akafariki wakati wa kampeni na ofisi ikafungwa kwa muda.

Cha ajabu, baada ya mwenyekiti kufariki mtendaji wa Kata akaniruhusu nifungue ofisi ili niendelee kutoa huduma kwa Wananchi ,kwahiyo nimehudumia Kitongoji nikiwa kama Katibu na wakati huo nikiwa nakaimu mwenyekiti Kitongoji cha jirani ambacho ni Saidi Domo.

"Sasa nimehudumia tangu 2020 mpaka sasa na ilipofika 2024 nikasema mbona kama  mimi naweza ikabidi nitie nia niingie katika kinyang'anyiro ili nigombee kuwa mwenyekiti wa Kitongoji,"anaeleza Zamda.

Je, Kitongoji chako kimenufaika nini na wewe kwa muda wote huo uliohudumu kama Katibu?

Mwenyekiti wangu alipofariki aliacha kiwanja cha ofisi lakini mimi kwa nafasi yangu kama Katibu nilipambana,tukachangishana kwenye Kitongoji chetu tukaanza ujenzi wa ofisi lakini nikaona watu wangu hawana uwezo wa kusema tunaweza kujenga ofisi ndio nilipoanza michakato ya kwenda kwa wadau.

Hakika, nilitembea kwa wadau usiku na mchana na hatimaye kufanikisha kujenga ofisi na sasa tupo katika ofisi yetu ingawa haijakamilika na hilo ndio likanipa moyo nikasema kumbe naweza kwanini nisigombee.

Unasababu zipi za kugombea katika Kitongoji chako?

Mimi nimegombea kwasababu nimeona bado yapo mahitaji yanayohitajika katika Kitongoji chetu na wapo wengi ambao wanaweza kuwa viongozi lakini nikasema ngoja nijitoe mimi kwanza lakini nashukuru nilipoamua kujitoa Wananchi wenzangu wameridhia mimi niwe mwenyekiti wa 2024 - 2029.

" Nimegombea kura za maoni nimeshinda kwa kishindo kwakuwa katika uchaguzi huo tuligombea wawili na mimi nilipata kura 121 dhidi ya kura 30 alizopata mgombea mwenzangu Ally Mohamed,"anaeleza Zamda 

Je, endapo utashinda katika uchaguzi nini malengo yako mahususi?

Kitongoji chetu kilikuwa hakina ofisi lakini tumepata ofisi japo haijakamilika Kwa kupata choo na mimi nia yangu ni kuhakikisha ofisi inakamilika na kupata choo nzuri ya kisasa.

Ukiachia hilo, Kitongoji chetu hakina hata Shule ya watoto wadogo kwahiyo endapo nitashinda natamani Kitongoji kipate kituo cha malezi ili watoto chini ya miaka minne hadi mitano wale ambao hawajaingia chekechea wawe wanasoma hapo.

Ukiachilia mbali suala la ofisi na kituo cha malezi ya watoto ,nini hasa changamoto nyingine zilizopo katika Kitongoji chako?

Hakika zipo changamoto nyingi katika Kitongoji chetu ikiwemo barabara, barabara nyingi zimekuwa zikisumbua wakati wa mvua na hivyo kukwamisha shughuli za uzalishaji kwa wananchi .

Lakini ,mimi kama mimi siwezi ila nimewaomba wanachama wenzangu siku naomba kura kwamba nipo tayari wanitume na nitawatumikia na hayo ndio malengo yangu.

"Lakini tutakapokaa kwenye mikutano yetu watakachosema wanachotaka mimi nitakuwa tayari kufanya kwa ajili ya manufaa ya Kitongoji cha Mlandizi Mjini", anaendelea kusema Zamda

Vipi kuhusu mtazamo wa wanaume juu yako na wanakuchukuliaje baada ya kushinda uchaguzi wa kura za maoni?

Yaani nikuambie tu Mwandishi wa habari wanaume wa Kitongoji hiki wanaimani kubwa sana na mimi, yaani niseme tu kwenye uchaguzi huu mimi sijasema bali nimesemewa na miongoni mwa walionisemea asilimia 80 ni wanaume.

"Wanaume waliniambia Zamda unatosha nenda kachukue fomu tupo nyuma yako na mimi sitowaangusha kwani nataka nifanye vile ambavyo wao wanataka kwa mustakabali wa Kitongoji chetu,"anaongeza Zamda .

Vipi Mume wako analeta vipingamizi gani juu ya wewe kugombea?

Mimi nimeolewa na nina watoto watatu namshukuru mume wangu ameniruhusu bila shaka na amekuwa na imani na mimi na anajua utendaji wangu ndio maana aliposikia nimeshinda uchaguzi wa kura za maoni alishangilia sana na hakushangaa kwakuwa anajua na ananipa ushirikiano kabisa.

Je, unaweza kutuambia ni kitu gani hasa kinasababisha wanawake kutogombea nafasi za uongozi?

Mimi naweza kusema sababu kubwa Wanawake wengi wanashindwa kujiamini lakini Wanawake tunaweza ila mtu hajadhubutu ninaimani ukishaingia utaona hahahaha kumbe ipo hivi na utafanya vizuri ila  wanatanguliza uoga tu.

Sasa unawashauri nini Wanawake wenzako?

Mara nyingi nimekuwa nikiwashauri kuwa wasiogope maana uongozi sio kazi ila kinachotakiwa unapokuwa  kiongozi shirikisha wengine ili uongozi husiwe mgumu , uongozi utakuwa mgumu kama huu wa Kitongoji au Kijiji kama utakuwa unang'ang'ania  kazi zote hufanye mwenyewe.

"Kama mimi mwenyekiti wa Kitongoji ninao wale wajumbe watano wa Serikali tukishagawana yale majukumu ukizingatia na mabalozi wapo kazi hii sio ngumu ,ni kushirikiana tu ,huyu akishika hiki  yule akishika kile panaposhindikana mnashare wote mambo yanaenda,"anasema Zamda

Je,kipindi ukiwa Katibu ni changamoto gani uliziona kama mwanamke?

Changamoto zipo,unajua hizi kazi zetu zipo zile shida za usiku maana yupo mtu atakugongea usiku wa manane anatatizo na anahitaji msaada wako kwahiyo iwe hisiwe lazima utatoka .

Kwahiyo mimi mume wangu huwa ananisindikiza au kama mtoto wangu wakiume yupo huwa ananisindikiza pia na sijawai kupigiwa simu usiku nikasema eti siwezi kutoka yaani nitafanya kila njia lazima nikapambane nimalize tatizo .

"Watu au wananchi wa hapa ukiwauliza watasema Zamda tunampendea hilo tu ,hajawai kushindwa kutatua matatizo yetu ,mpigie simu wakati wowote anakuja,"Zamda akifafanua.

Je, tutarajie kumuona Zamda wa namna gani hapo baadae?

Mmmh!malengo yangu ya baadae ngoja kwanza niendelee taratibu hivi,ingawa natamani hata kufika niwe diwani wa viti maalum ili niweze kuwasemea Wanawake wenzangu lakini naenda kwa stepu.

"Kidogo kidogo naenda hatua hii ukiona ipo sawa unaenda taratibu maana wanasemaga mambo mazuri hayataki haraka na mimi naenda taratibu,"amesikika akisema Zamda



Pamoja na mambo mengine Zamda anawashukuru Wanawake wenzake kwa kumtia moyo katika kufikia ndoto zake akiwemo mbunge waVitimaalum Hawa Mchafu,Diwani wa Kata ya Mlandizi Euphrasia Kadala na Diwani wa viti maalum Josephine Gunda .

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ,Vijiji na Vitongoji unatarajia kufanya Novemba 27 mwaka huku kampeni zake zikitarajiwa kuanza Novemba 21 mpaka Novemba 26.


Club News Editor - Charles Kusaga

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA