ELIMU BILA MALIPO MKOMBOZI KWA WATANZANIA WENGI
Na Gustaphu Haule, Tanzania
SERIKALI ya awamu ya Sita iliyo chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanikisha kuendeleza utoaji wa huduma ya elimu ya msingi bila malipo, hali iliyowawezesha Watanzania wengi kupeleka watoto wao shule.
Ikumbukwe kuwa dhana ya elimu Msingi bila malipo inawezesha utoaji wa elimu kwa Mwanafunzi yeyote bila mzazi au mlezi kulipa ada wala michango ya fedha katika shule.
Utozaji wa ada au michango mbalimbali shuleni kwa mwanafunzi ilikuwa ni kikwazo kikubwa hasa kwa Wazazi au Walezi wasio na uwezo jambo ambalo lilisababisha watoto wengi wakitanzania kushindwa kusoma.
Katika kipindi cha kuanzia April, 2021 hadi Februari, 2024 jumla ya Shilingi Trilion 1.1 zimetolewa na Serikali ya awamu ya Sita na kutumwa Shuleni kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa Elimu ya msingi bila malipo.
Fedha hizo ni kwa ajili ya ruzuku ya uendeshaji shule, fedha za chakula cha wanafunzi, fidia ya ada (Bweni na Kutwa) na posho za madaraka kwa wakuu wa Shule na maafisa Elimu Kata.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye aliyefanya mapinduzi katika Elimu bila ada kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita wananufaika na mpango huu.
Kwa sasa kila mwezi Serikali inatoa bilioni 33 ambapo awali ilikua ikitolewa bilioni 29, ongezeko hili la shilingi bilioni 4 kila mwezi limewawezesha Watoto ambao walikua wanashindwa kuendelea na masomo yao ya kidato cha Tano na Sita kwa kukosa fedha sasa wote wako darasani.
Taarifa hii ni kwa mujibu wa muhtasari wa mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia tangu aingie madarakani iliyotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
#KAZIINAONGEA

Comments
Post a Comment