WAZIRI BASHUNGWA AWAPA MATUMAINI WANANCHI MLANDIZI ,ASEMA BARABARA YA MLANDIZI - KITUO CHA SGR RUVU STESHENI KUWEKWA LAMI.




Na Gustaphu Haule,Pwani

WAZIRI wa Ujenzi Innocent Bashungwa amewahakikishia wakazi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mlandizi iliyopo Kibaha Vijijini kuwa Serikali itafanya jitihada kuhakikisha inajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kilomita 23 inayoanzia Mlandizi stendi na kuelekea katika kituo cha reli ya mwendokasi ( SGR) kilichopo Ruvu Stesheni.

Bashungwa ametoa kauli hiyo Oktoba 8 wakati akizungumza na wakazi hao katika mkutano wake wa hadhara aliohufanya katika Kata ya Janga ikiwa ni sehemu ya ziara yake aliyoanza kufanya Wilayani Kibaha Oktoba 8.

Waziri wa ujenzi Innocent Bashungwa akizungumza na Wananchi katika moja ya mikutano yake aliyoifanya Wilayani Kibaha ikiwa sehemu ya ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali.

Bashungwa, amesema kuwa barabara ya Mlandizi inayoelekea katika kituo cha reli ya mwendokasi Ruvu ni muhimu kwakuwa ikikamilika itawasaidia Wananchi wanaotumia reli hiyo kusafiri kirahisi.

Amesema kuwa, si tu kufika katika kituo cha reli hiyo lakini pia kujengwa kwa barabara hiyo kutasaidia kufungua fursa za uchumi kwa Wananchi sambamba na kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa viwanda katika maeneo hayo .

"Nimepita katika barabara hii nimegundua inaumuhimu mkubwa kwakuwa inaelekea katika reli yetu ya mwendokasi kituo cha Ruvu Stesheni ,hospitali ya Wilaya na hata katika eneo la uwekezaji wa viwanda hivyo nitakwenda kuifanyiakazi ili kusudi tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami,"amesema Bashungwa 

Aidha, Bashungwa amesema kuwa wakati zikisubiliwa fedha za ujenzi huo lakini kutokana na umuhimu wake kuwa mkubwa lazima ianze kukarabatiwa kwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika.

Amemuagiza meneja wa Tanroads Mkoa wa Pwani Baraka Mwambage kufanya utaratibu wa kumpata mkandarasi ambaye atairekebisha na kuiweka sawa ili iweze kupitika kwa urahisi na hivyo kupelekea shughuli za kiuchumi na masuala mengine yaweze kuendelea.

Amesema kuwa, anafahamu barabara hiyo ni ndefu kwakuwa inaunganisha Bagamoyo- Makofi - Mlandizi - Mzenga  Maneromango mpaka vikumburu lakini ni vizuri ikaanza kujengwa kidogokidogo kuliko kusubiri mpaka fedha zote.

Amewaomba Wananchi kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kuweka jitihada na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwani anaamini Rais Samia ni Rais wa vitendo na kila jambo litatekelezwa kulingana na mipango iliyopo.
Waziri wa ujenzi Innocent Bashungwa akikagua mradi wa ujenzi wa Soko la kisasa jana linalojengwa katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini Mkoani Pwani Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge 

Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa amewahamasisha Wananchi kujitokeza katika kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vitongoji ikiwa pamoja na kujiandikisha katika daftari la wapiga kura ili kusudi muda ukifika wapate fursa ya kuchagua viongozi wazuri watakaowaletea maendeleo.
 
Akiwa Wilayani Kibaha Bashungwa ametembelea mradi wa Shule ya Sekondari Msangani uliopo Kata ya Msangani, mradi wa ujenzi wa Sekondari Kata ya Viziwaziwa katika Halmashauri ya Kibaha Mjini huku Halmashauri ya Kibaha Vijijini ametembelea hospitali na ujenzi wa Soko la kisasa.

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa (Kulia)akikagua hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini katika ziara yake aliyoifanya Oktoba 8 mwaka huu na kushoto mwenye koti na kofia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa barabara hiyo ikijengwa itafungua fursa nyingi kiuchumi ambapo pia amemuomba Waziri Bashungwa kutoa kipaumbele kwa barabara zote zinazopita kwenye miradi  ya kimkakati ili kusudi wawekezaji waweze kuja kwa wingi.

Pamoja na mambo mengine Kunenge ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi anayyoifanya hususani kwa Wananchi wa Mkoa wa Pwani.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza katika moja ya mikutano ya hadhara kwenye ziara ya Waziri wa ujenzi Innocent Bashungwa jana Wilayani Kibaha.


Kunenge, amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Mkoa wa Pwani umepokea jumla ya Sh.trilioni 1.3 fedha ambazo zimekwenda kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Shule,vituo vya afya ,maji barabara,umeme na hata masuala mengine.

Hatahivyo, Kunenge amesema kazi kubwa wanayoifanya ni kuhakikisha wanazisimamia fedha hizo ili kusudi zifanyekazi iliyokusudiwa na kwa upande wa Mkoa wake fedha hizo zimefanya mambo makubwa na kufanya Mkoa kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo.

Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA

RC PWANI AFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MKURUGENZI WA KIBAHA MJINI DKT.ROGERS SHEMWELEKWA