TRA PWANI YAMWAGIWA SIFA, WAFANYABIASHARA WAFURAHIA UTENDAJI KAZI WAO



Na Gustaphu Haule,Pwani

KIKAO cha baraza la biashara Mkoa wa Pwani kimetoa pongezi kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Pwani kwa namna inavyowahudumia na kupunguza kero kwa wafanyabiashara tofauti na ilivyo awali.

Kikao hicho kilichofanyika Oktoba 2 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani iliyopo Mjini Kibaha kilikuwa na lengo la kufanya majadiliano baina ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi (PPD) sambamba na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara.

MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA

Katika kikao hicho TRA Mkoa wa Pwani ilionekana kuwa taasisi ya Umma ambayo kwasasa imekuwa ikiongoza kwa kutoa huduma bora na  nzuri kwa wafanyabiashara kiasi ambacho imekuwa  ikileta mvuto kwa wafanyabiashara wengi Mkoani Pwani.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wafanyabiashara Mkoa wa Pwani Abdallah Ndauka,amesema kuwa TRA kwasasa inafanya vizuri na wao kama wafanyabiashara wanaridhishwa na hatua hiyo kwani kwasasa TRA wamekuwa rafiki kwa wafanyabiashara.

Mwenyekiti wa Jukwaa la wafanyabiashara Mkoa wa Pwani Abdallah Ndauka akizungumza katika kikao cha majadiliano kati ya sekta ya Umma  na Sekta za binafsi kilichofanyika Oktoba 2 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani 

Ndauka, amesema kuwa TRA ni mfano wa taasisi nyingine za Serikali kwani mara nyingi wamekuwa wakitoa elimu ya Kodi kwa wafanyabiashara na wameachana na tabia ya kufunga maduka hovyo na hivyo kufanya wafanyabiashara kulipa Kodi kwa hiari.

Ameongeza kuwa, awali ugomvi mkubwa ulikuwa ni juu ya wafanyabiashara na TRA kufunga maduka yao na hata kuwapiga penati hovyo wafanyabiashara lakini kwasasa mambo hayo yamekwisha kwani wafanyabiashara wapo huru katika kuendeleza biashara zao .

"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa sisi wafanyabiashara wa Mkoa wa Pwani tunaridhishwa na huduma za Mamlaka ya Mapato TRA Mkoa wa Pwani kwani wamekuwa marafiki wetu na hata yale mambo ya kufungiana maduka, kupigwa penati hovyo yote yamekwisha na sasa tunalipa kodi kwa hiari," amesema Ndauka.

Ndauka , amesema itakuwa vizuri endapo taasisi nyingine za Serikali zikaiga mfano huo huku akilalamikia tabia za maafisa biashara kugombana na wafanyabiashara bila sababu ya Msingi.

Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Masawa Masatu ( aliyevaa Suti Kulia) akisikiliza hoja zinazotolewa na wafanyabiashara katika kikao cha majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi kilichofanyika Oktoba 2,2024 katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani uliopo Mjini Kibaha kikao hicho kiliandaliwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambao TRA walikuwa miongoni mwa wafadhili wa kikao hicho.

Hatahivyo, Ndauka amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge kwa kuona umuhimu wa kukutana na wafanyabiashara ili kujua na kutatua changamoto zao ambapo ameomba vikao kama hivyo vishuke chini katika ngazi ya Wilaya na hata Kata.

Nae mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Wamachinga Mkoa wa Pwani (SHIUMA) Philemon Maliga pamoja na kutoa pongezi nyingi kwa TRA lakini pia ameiomba taasisi hiyo kuendelea kutoa elimu ya ulipaji kodi kwa wafanyabiashara wadogo ili waweze kuwa wafanyabiashara wakubwa wa hapo baadae.

Maliga, ameipongeza Serikali ya Mkoa wa Pwani kupitia Mkuu wake wa Mkoa Abubakar Kunenge kwa kuwajengea ofisi wamachinga na hivyo kufanya biashara zao kwa uhuru .

Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Wamachinga Mkoa wa Pwani Philemoni Maliga akizungumza katika kikao cha majadiliano kati ya Sekta za Umma na Sekta binafsi kilichofanyika Oktoba 2 katika ukumbi wa mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.

Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Masawa Masatu,amesema kuwa pamoja na mambo mengine waliona ni vyema wakawa sehemu ya kufadhili kikao hicho kwani malengo yake ni kukutana na wadau na kisha kuona namna ya kutatua changamoto katika maeneo yao ya kazi.

Masatu, amesema kuwa baada ya kupokea maoni na kero kutoka kwa wafanyabiashara wao kama taasisi ya Serikali wanakwenda kuifanyiakazi ili kusudi kutoa nafasi kwa kila mfanyabiashara na hata mjasiriamali kuipenda nchi yake na hatimae kuwa mzalendo wa kulipa Kodi kwa hiari.

Kuhusu TRA kufanya vizuri Masatu amesema kuwa mabadiliko katika taasisi hiyo ndio chachu ya wafanyabiashara wengi kuvutiwa na hivyo kuwa walipa Kodi wazuri na kwamba uhalisia unaonyesha hata katika makusanyo ya Kodi .

Masatu , amesema kuwa kubwa ni kufuata utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan ambaye ameeleza wazi kuwa lazima kuwe na ushirikishwaji wa pamoja na walipa Kodi ikiwa pamoja na kutenga muda wa kusikiliza shida zao .

Ameongeza kuwa TRA Mkoa wa Pwani imefuata na itaendelea kufuata maelekezo hayo na kwamba kwasasa tayari wametenga siku ya Alhamis ya kila wiki ikiwa maalum kwa ajili ya kuwasililiza walipakodi na kuwatatulia changamoto zao .

"Sisi TRA tumetenga siku ya Alhamis ya kuwasikiliza walipakodi na kutatua changamoto zao ndio maana imekuwa ikiwaridhisha  na kitendo hicho kinasababisha ongezeko la walipakodi na kufanya makusanyo ya kodi kuongezeka zaidi,"amesema Masatu

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameeleza kufurahishwa na kikao hicho kuisifu TRA kwa kazi nzuri inayofanya lakini ameutaka uongozi wa TRA kuendelea kufanya vizuri ili kuhakikisha kila mfanyabiashara anapata elimu na hivyo kulipa Kodi bila kutumia nguvu.

Katibu Tawala Msaidizi viwanda na Biashara Rehema Akida,amesema kuwa Mkoa unaendeleaje kuweka jitihada kwa ajili ya kuhakikisha wafanyabiashara wanakutanishwa pamoja kwa ajili ya kusikiliza changamoto zao ili kusudi Serikali hiweze kuzifanyiakazi.

Katibu Tawala Msaidizi Viwanda na Biashara Mkoa wa Pwani Rehema Akida akizungumza katika kikao cha majadiliano kati ya Sekta za Umma na Sekta binafsi (PPD) kilichofanyika Oktoba 2 katika ukumbi wa mkuu wa Mkoa uliopo Kibaha Mjini.

Hatahivyo,amesema Mkoa umejipanga vizuri katika kutangaza bidhaa na biashara mbalimbali zilizopo Mkoani Pwani ikiwa pamoja na kuhakikisha yanaandaliwa maonesho maalum ya kutangaza bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vya Mkoa wa Pwani.


Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA