UCHAGUZI KURA ZA MAONI CCM WATIKISA, WENGI WASHINDA KWA KISHINDO
Na Gustaphu Haule, Kibaha PWANI
UCHAGUZI wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kwa ajili ya kuwapata wagombea katika kinyanga' nyiro cha uchaguzi wa Serikali za Mitaa umefanyika jana Oktoba 23 katika maeneo mbalimbali huku baadhi wa wagombea wakiibuka na ushindi mnono.
Wagombea walioibuka kinara katika uchaguzi huo ni pamoja na Shauri YombaYomba Mwenyekiti mstaafu wa Mtaa wa Mailimoja"B" kutoka tawi la Yombayomba aliyeibuka mshindi kwa kupata kura 186 dhidi Shamira Salum aliyepata kura mbili na Anthony Fudua akiambulia kura Moja.
Mwenyekiti mstaafu wa Serikali ya Mtaa Mailimoja "B"Shauri Yombayomba akiwashukuru wajumbe mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi katika wa uchaguzi wa kura za maoni tawi la Yombayomba uliofanyika Oktoba 23 mwaka huu.
Uchaguzi wa tawi la Yombayomba umesimamiwa na Juma Kasheshe pamoja na Yohana Mwananzila kutoka CCM Kata ya Tangini ambapo hatahivyo waliendesha uchaguzi huo kwa utaratibu mzuri uliowavutia wagombea na wapiga kura .
Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa kwake Yombayomba amewashukuru wajumbe kwa kuendelea kumuamini kwa kumpa kura nyingi huku akiomba ushirikiano zaidi kwa ajili ya kuhakikisha wanashinda katika uchaguzi wa Novemba 27 mwaka huu.
Mtaa wa Tangini aliyeibuka kinara ni Mwenyekiti anayetetea nafasi yake Pilmini Gama ambaye katika uchaguzi huo ameibuka kuwa mshindi kwa kupata kura 307 dhidi ya kijana Idd Mfaume aliyapata kura 120 na Philemoni Mabuga aliyejikuta akipata kura 67.
Gama, pamoja na mambo mengine ameeleza kufurahishwa na ushirikiano mkubwa alioupata katika uchaguzi huo huku akiwashukuru wajumbe kwa kumpata kura nyingi za kuongoza.
Mwenyekiti mstaafu wa Serikali ya Mtaa wa Tangini Pilmini Gama akiomba kura katika uchaguzi wa kura za maoni ( CCM) uliofanyika Oktoba 23 mwaka huu ambapo hatahivyo Gama ameshinda kwa kupata kura 307.
Gama, amewaomba wanaCCM wote wa Kata ya Tangini kushikamana kwakuwa uchaguzi wa ndani umekwisha lakini kazi kubwa inatakiwa kufanyika kwa ajili ya kuhakikisha wagombea wote wa CCM wanashinda Novemba 27.
Katika Mtaa wa Kilimahewa Benedict Alphonce ameshinda kwa kupata kura 108 huku Ayubu Joel ambaye ni mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Tangini akipata kura 76 na Ramadhani Ngowo akipata kura 52 na Rukia Mahenge akipata kura 23.
Msimamizi wa uchaguzi tawi la Kilimahewa Jeremiah Komba (Shungu) Mjumbe wa Kamati ya Siasa Kata ya Tangini amesema uchaguzi katika eneo hilo ulikuwa wa amani na utulivu na kwamba mpaka matokeo yanatangazwa hapakuwa na sitofahanu yoyote.
Mtaa wa Mailimoja ni moja kati ya Mitaa ambayo ilikuwa ikichunguliwa na wengi kutokana na ushindani wa wagombea wake dhidi ya Yassin Mudhihir aliyekuwa mgombea mtetezi na Athumani Mkongota (Chichi).
Hii foleni ya wapiga kura katika uchaguzi wa kura za maoni katika tawi la CCM Mailimoja Oktoba 23 ambapo wagombea wake walikuwa ni Athumani Chichi na Yassin Mudhihir.
Mailimoja ambayo imebeba jina maarufu katika Halmashauri Mji Kibaha uchaguzi wake ulikuwa na hamasa kubwa kwani wanaCCM wengi waliojitokeza kupiga kura wametoka katika makundi ya wauza matunda,wachoma chipsi, bodaboda,wauza maji na wajasiriamali wengine.
Duru la uchaguzi katika Mtaa wa Mailimoja lilionekana kumuangukia Chichi ambaye katika uchaguzi huo ndiye aliyeibuka kinara kwa kupata kura 146 dhidi ya Mudhihir aliyepata kura 52.
Kwa upande wa Mtaa wa Machanjioni mshindi wa kwanza ameongoza kwa kupata kura 116 huku anayefuatia akipata kura 45 .
Athumani Chichi (Kulia) katika tukio la kujiunga na CCM hivi karibuni huko katika Kata ya Mkuza Kibaha Pwani.
Kufanyika kwa uchaguzi wa kura za maoni ni hatua ya kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27 mwaka huu ambapo wagombea wa vyama mbalimbali wataingia katika kinyang'anyiro hicho .
Comments
Post a Comment