TGNP NA TADIO YAWANOA WAANDISHI WA HABARI KUANDIKA HABARI ZENYE MLENGO WA JINSIA, YATAKA WAANDISHI KUHAMASISHA WANAWAKE KUGOMBEA.
Na Gustaphu Haule
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na mtandao wa Radio Jamii Tanzania wameendelea kuwapiga msasa Waandishi wa habari kuhusu kuhamasisha ushiriki wa Wanawake katika uongozi hasa katika kipindi cha kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mafunzo hayo ya siku tatu yameanza kufanyika leo Oktoba 29 katika ofisi za TGNP zilizopo Jijini Dar es Salaam na kumalizika Oktoba 31 mwaka huu yakiwa chini ya wakufunzi wawili akiwemo Deogratius Temba na Vera Assenga.
Katika mafunzo hayo TGNP imewakutanisha waandishi wa habari zaidi ya 50 kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam.
Akifungua mafunzo hayo afisa habari wa TGNP Monica John, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuendelea kuhamasisha Wanawake kutumia fursa zilizopo hasa katika uchaguzi kugombea nafasi mbalimbali.
Afisa habari wa Mtandao wa Kijinsia Tanzania Monica John (kushoto) akifungua mafunzo ya siku tatu kwa Waandishi wa habari kuhusu masuala ya kuandika habari zenye mrengo wa Kijinsia,mafunzo hayo yameanza kufanyika Oktoba 29 katika ofisi za TGNP zilizopo Jijini Dar es Salaam.
Monica, amesema kuwa mwaka huu Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kwamba hiyo ni fursa kwao hivyo TGNP wanatumia nafasi hiyo kuwanoa wanahabari ili wakatumie kalamu zao katika kuwahamasisha Wanawake.
Amesema, katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 Wanawake waliojitokeza kugombea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni asilimia 2.1 jambo ambalo kwasasa lazima lipiganiwe ili Wanawake wajitokeze.
"Mwaka huu kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa na tayari fomu zimeanza kutolewa kwahiyo ni wakati muafaka wa Waandishi wa habari kutumia nafasi zetu kwenda kuhamasisha Wanawake kujitokeza katika uchaguzi huo", amesema Monica
Aidha, Monica amesema TGNP inatambua umuhimu wa Vyombo vya habari hapa nchini ndio maana inaendelea kutoa mafunzo ya kuwanoa Waandishi wa habari lengo ni kuhakikisha Wanawake wanashiriki katika chaguzi mbalimbali.
Awali mkufunzi wa mafunzo hayo Vera Assenga, amesema kuwa anaamini waandishi wa habari wakifanyakazi zao vizuri kuna uwezekano wa kuwepo na mabadiliko makubwa ya wanawake kujitokeza.
Vera Assenga mkufunzi wa mafunzo ya Waandishi wa habari kuhusu kuandika habari zenye mrengo wa Kijinsia yanayotolewa na TGNP kuanzia Oktoba 29 mwaka huu Jijini Dar es Salaam.
Assenga, amewaomba Waandishi hao kwenda kujitoa katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuhakikisha Wanawake wanaingia katika Vyombo vya maamuzi.
Baadhi ya Waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo akiwemo Christopher Lilai na Grace Mwakalinga wameishukuru TGNP kwa kutoa mafunzo hayo huku wakiahidi kuyafanyiakazi kikamilifu.
Comments
Post a Comment