SHAURI AFUNGUA DIRISHA UCHUKUAJI FOMU UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA
Na Gustaphu Haule
MGOMBEA wa nafasi ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mailimoja "B" kupitia Chama Cha Mapinduzi" CCM" Shauri Yombayomba tayari amechukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo.
Yombayomba amechukua fomu hiyo mapema leo Oktoba 28 katika ofisi za Mtaa huo akiambatana na wajumbe wake watano akiwemo Webina Gimasa, Josephu Sanga, Mwanaidi Ndotia, Omari Mfaume na Zainabu Charles.
Mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti Serikali ya Mtaa Mailimoja B Shauri Yombayomba (CCM) akipokea fomu kutoka kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi katika Mtaa huo Suzana Awiti leo Oktoba 28, 2024
Miongoni mwa viongozi alioongozana nao ni Mwenyekiti wa CCM tawi la Yombayomba, Amina Musa, Katibu wa tawi Kizito Iyulu na Katibu wa itikadi uenezi na mafunzo Chedy Shaban.
Akiwa ofisini hapo Yombayomba alikabidhiwa fomu hiyo na msimamizi Msaidizi wa uchaguzi Mtaa wa Mailimoja "B" Suzana Awiti ambaye alimueleza mgombea huyo kuwa ofisi hiyo inakuwa wazi mpaka saa 10 jioni.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo Yombayomba amesema amechukua fomu hiyo pasipo changamoto yoyote kutokea huku akiwashukuru viongozi wa CCM kwa ushirikiano mkubwa wanaotoa.
Yombayomba, amesema kuwa zoezi la kuchukua fomu limepita lakini zipo hatua nyingine ambazo zinafuata ikiwemo kurudisha fomu na hata kusubiri michakato mingine inayofuata.
Amewaomba Wananchi wa Mtaa wa Mailimoja B kuendelea kumpa ushirikiano yeye binafsi na kwa chama chake na kwamba endapo atashinda nafasi hiyo utakuwa ushindi wa Wananchi wote.
Mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti Serikali ya Mtaa wa Mailimoja B Shauri Yombayomba akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) tawi la Yombayomba mara baada ya kuchukua fomu katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa Mailimoja B leo Oktoba 28, 2024
"Leo nimekuja hapa katika ofisi zetu za Mtaa kwa ajili kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya kuwa mwenyekiti wa Mtaa huu, nimepata ridhaa ya Chama changu kwakuwa kimeniamini na mimi natumia nafasi hii kuomba ushirikiano ndani ya Chama changu na hata nje ya chama,"amesema Yombayomba
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM tawi la Yombayomba Amina Musa, amesema kuwa ndani ya Chama tayari wamepata mgombea lakini uchaguzi bado haujaisha hivyo amewaomba wanaCCM na wananchi wote kukiunga mkono CCM katika hatua zinazofuata.
Zoezi la kuchukua fomu kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa zimeanza leo Oktoba 28 hadi Novemba 1 huku uchaguzi wake ukitarajia kufanyika Novemba 27.
Hongera sana ujiona wengi wamesema jambo la wengi lifanyie kazi kiongozi mzuri ni yule mwenye hekima
ReplyDelete