RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA
Na Gustaphu Haule, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amewaongoza wakazi wa Mtaa wa Mkoani" A" uliopo Kata ya Tumbi Halmashauri ya Mji Kibaha katika zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura lililoanza leo Mkoani Pwani.
Aidha, Kunenge akiwa katika kituo hicho aliambatana na Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimoni pamoja na mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Rogers Shemwelekwa.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akiwaongoza Wananchi wa Mtaa wa Mkoani "A", Kata ya Tumbi Halmashauri ya Mji Kibaha kujiandikisha katika daftari la wapiga kura zoezi ambalo limeanza leo Oktoba 11 hadi Oktoba 20 mwaka huu
Akizungumza mara baada ya kujiandikisha katika kituo hicho Kunenge amesema kuwa zoezi hilo limeanza kufanyika Mkoa wa Pwani leo Oktoba 11 na litamalizika Oktoba 20 mwaka huu.
Kunenge amesema kuwa kufanyika kwa zoezi hilo ni maandalizi ya kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
Kunenge, amewashukuru Wananchi waliojitokeza kujiandikisha katika kituo hicho huku akiwaomba wakazi wa Mkoa wa Pwani kujitokeza kwa wingi katika maeneo yao ili kujiandikisha kwenye daftari hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akitoa elimu ya kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura mara baada ya kumaliza kujiandikisha katika kituo cha Mtaa wa Mkoani "A "Kilichopo Kata ya Tumbi Kibaha Mjini,zoezi hilo limeanza Leo Oktoba 11 hadi Oktoba 20 mwaka huu .
Amesema kuwa zoezi la kujiandikisha katika daftari hilo litakuwa likifanyika kuanza saa 2 asubuhi mpaka saa 12 jioni huku akisema kujiandikisha ni muhimu kwakuwa lipo kisheria.
Kunenge, amesema Mkoa wa Pwani Kuna Vijiji 417, Vitongoji 2028, Mitaa 73 na vituo 2374 ambapo ameongeza kuwa mtu akitaka kutimiza haki yake ya kumchagua kiongozi anayemtaka lazima hawe amejiandikisha.
Amesema vituo vya uandikishaji vimewekwa kwa wingi ili kuwarahisishia Wananchi wasiende mbali lakini pia kuondoa msongamano na hata kupoteza muda hivyo Wananchi wanatumie fursa hiyo kwani ni haki yao.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akijiandikisha katika daftari la wapiga kura katika Mtaa wa Mkoani A,Kata ya Tumbi Halmashauri ya Mji Kibaha zoezi ambalo limeanza Leo Oktoba 11 na kumalizika Oktoba 20 mwaka huu
"Msingi wa utawala bora wa nchi hii unaanza na uongozi wa ngazi zetu za mwanzo kabisa na wananchi ndio wanaowajua viongozi wazuri hivyo wakijiandikisha ndipo watapata fursa ya kumchagua kiongozi mzuri,"amesema Kunenge.
Mkazi wa Mtaa wa Mkoani "A" Fatma Lupinda, amesema wamelipokea vizuri zoezi la kujiandikisha na ndio maana wamejitokeza kwa wingi huku akisema kila Mtanzania ana haki ya kujiandikisha ili aweze kutimiza haki yake ya Msingi.
Afisa mtendaji Kata ya Tumbi Msemakweli Karia amesema kuwa kwasasa wameanza kuandikisha kwa kuchukua majina yao na umri wao lakini tarehe 21 majina yote yatapandikwa ukutani kwa ajili ya kupiga kura.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge (katikati)akiwa kwenye picha ya pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Rashid Mchatta wa kwanza Kulia, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimoni wa pili kutoka kushoto Katibu Tawala Wilaya Kibaha wa kwanza kushoto na mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Rogers Shemwelekwa wa pili kutoka kulia mara baada ya kujiandikisha katika daftari la wapiga kura Leo Oktoba 11 katika Mtaa wa Mkoani "A"uliopo Kata ya Tumbi.
Kwa mujibu wa Sensa ya Mwaka 2022 Mkoa wa Pwani una jumla ya wakazi 2,024,947 kati yao Wanaume 998,616 na Wanawake 1,026,331.
Comments
Post a Comment