RC KUNENGE : TAASISI ZA SERIKALI ACHENI KUWA KERO KWA WAFANYABIASHARA WADOGO,TOENI ELIMU IWASAIDIE KUKUZA MITAJI YAO.




Na Gustaphu Haule,Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameziagiza taasisi za Serikali zilizopo ndani ya Mkoa wake kuacha kuwa kero kwa wafanyabiashara wadogo na badala yake wawasaidie kuwapa mbinu na  elimu ya namna ya kukuza na kuendeleza biashara zao.

Kunenge,ametoa kauli hiyo  Oktoba 2,2024 Mjini Kibaha wakati akifungua kikao  cha baraza la biashara la Mkoa kilicholenga kufanya majadiliano kati ya Sekta za Umma na Sekta binafsi (PPD).

Kunenge, amesema kuwa wafanyabiashara wadogo wanatakiwa kupewa elimu ya kukuza biashara zao ili waweze kufikia malengo ya kuwa wafanyabiashara wakubwa ili mwisho wa siku Serikali iweze kukusanya kodi vizuri.

Baadhi ya viongozi walioshiriki kikao cha baraza la biashara kilichofanyika Oktoba 2 Mjini Kibaha kikao hicho kilihusu majadiliano kati ya Sekta za Umma na Sekta binafsi( PPD).

Amesema, zipo baadhi ya taasisi ambazo zimekuwa kero kwa kukimbilia  kuwapiga penati na kutoza kodi bila kutoa elimu jambo ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa wafanyabiashara na hivyo kufunga biashara zao.

Amesema, kitendo cha wafanyabiashara kufunga biashara zao ni wazi kuwa kunasababisha Serikali kukosa mapato jambo ambalo haliwezi kukubalika kwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Amewataka, maafisa biashara wa Halmashauri ya Miji na Wilaya kuwa wabunifu katika utekelezaji wa kazi zao ikiwa pamoja na kuacha tabia ya kuwafungia hovyo wafanyabiashara maduka yao.

"Nataka wafanyabiashara wa kawaida  wasikilizwe na ikiwezekana chukueni maoni yao ili tuyafanyiekazi maana tunataka kuona nao wananyanyuka na kuwa wafanyabiashara wakubwa na tuache kuwa kero kwao," amesema Kunenge 
Baadhi ya washiriki katika kikao cha majadiliano ya Sekta za Umma na Sekta binafsi kilichofanyika Oktoba 2 Mjini Kibaha .

Kunenge, ameongeza kuwa Rais  Dkt.Samia Suluhu Hassan ameweka mazingira mazuri ya uwekezaji na anataka kuona malengo yake yanatimia hivyo ni vyema kila anayehusika afanyekazi kwa bidii.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chemba ya Biashara Mkoa wa Pwani (TCCIA) Said Mfinanga amepongeza hatua iliyochukuliwa na Mkuu wa Mkoa kwa kuwakutanisha pamoja kwa ajili ya kujadili changamoto zinazowakabili.

Mfinanga, amesema kuwa TCCIA imekuwa na mahusiano mazuri  na Serikali na mahusiano hayo yanatakiwa kuendelezwa kwa faida ya pande zote mbili.

Mwenyekiti wa Chemba ya wafanyabiashara Mkoa wa Pwani (TCCIA) Said Mfinanga akizungumza katika kikao cha majadiliano kati ya Sekta za Umma na Sekta binafsi kilichofanyika Oktoba 2,2024 Mjini Kibaha 

Amesema, wafanyabiashara sio wahalifu na kwamba kinachotakiwa kwasasa ni kuhakikisha taasisi za Serikali zinawashauri wafanyabiashara namna nzuri ya kulipa kodi kuliko kukimbilia kutoza faini.

Mfinanga amesema faini wanazopigwa wafanyabiashara zinatoka katika mitaji yao na sio faida na kwamba kufanya hivyo kunapelekea biashara nyingi kufungwa na hatimae kulikosesha Taifa mapato.

Mwakilishi wa Kongani ya viwanda (Sinotan) iliyopo Kata ya Kwala katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Bary Chale amesema changamoto kubwa kwasasa ni umeme unaokwamisha uzalishaji wa bidhaa katika eneo hilo.

Hatahivyo,Chale ameiomba Serikali kufanya ufumbuzi wa haraka ili kuhakikisha umeme unapatikana kwa haraka na kufanya uzalishaji huwe wa uhakika zaidi.




Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA

RC PWANI AFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MKURUGENZI WA KIBAHA MJINI DKT.ROGERS SHEMWELEKWA