OFISI YA MKUU WA MKOA WA PWANI YAENDESHA KONGAMANO KWA MAKUNDI MAALUM KUTOA HAMASA YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA.




Na Gustaphu Haule,Pwani

OFISI ya mkuu wa Mkoa wa Pwani imeendesha kongamano maalum la kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, kugombea na hata kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27 mwaka huu .

Kongamano hilo limefanyika Oktoba 9, Mjini Kibaha kwa kushirikisha makundi mbalimbali ikiwemo vyama vya Siasa, viongozi wa dini, makundi ya sanaa, bodaboda, Mamalishe, Machinga, mashirika yasiyo ya Kiserikali na hata makundi mengine.

Baadhi ya washiriki katika kongamano la kuhamasisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa lililofanyika Oktoba 9, katika jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge Katibu Tawala wa Mkoa huo Rashid Mchata amesema kuwa kongamano hilo ni  moja ya maandalizi ya kufanikisha uchaguzi huo.

Mchata, amesema kuwa katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 imelenga kupeleka madaraka kwa Wananchi na miongoni mwa madaraka hayo ni wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Vitongoji wanaotokana na uchaguzi wa Serikali za Mitaa.


Amesema, katika uchaguzi wa mwaka huu mkoa wa Pwani umejipanga na kuratibu shughuli zote za uchaguzi na kwamba makundi hayo ni muhimu kuwa mabalozi wakuhamasisha Wananchi kujitokeza katika kujiandikisha, kugombea na hata kupiga kura.

Mchatta, amesema makundi hayo yanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani pasipo migogoro huku akisisitiza zitumike 4R za Rais Samia.

Aidha, Mchatta amewaomba wawakilishi wa makundi hayo kwenda kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura ambapo kwa Mkoa wa Pwani zoezi hilo litaanza Oktoba 11 hadi 20.

Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta ( Kushoto) pamoja na mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania (UWT) Mkoa wa Pwani Zainabu Vullu(Kulia) wakishiriki kongamano la uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa makundi maalum lililofanyika Oktoba 9 katika jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa lililopo Mjini Kibaha.

Awali mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi Mkoa wa Pwani  George Nsajigwa, amesema kuwa maandalizi ya uchaguzi huo yanakwenda vizuri na kongamano hilo ni sehemu ya kuwakumbusha kuhusu uchaguzi huo .

Nsajigwa amesema pamoja na mambo mengine lakini malengo makubwa ya kongamano hilo ni kutoa elimu ya kuhamasisha wananchi kujitokeza katika kujiandikisha, kugombea na hata kupiga kura.

Amesema kuwa, kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi huo Novemba 1 hadi 7 ni uchukuaji wa fomu huku kampeni zikitarajiwa kuanza Novemba 20 hadi 26 na Novemba 27 ni siku ya kupiga kura kwa ajili ya kuchagua wenyeviti wa Serikali za Mitaa .

Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi Mkoa wa Pwani George Nsajigwa akizungumza katika kongamano la uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa makundi maalum lililofanyika Oktoba 9 Mjini Kibaha kwa maandalizi ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Muongozaji wa kongamano hilo Zablon Bugingo,  ameweka bayana mada katika uchaguzi huo ikiwemo Wanawake na uchaguzi,vijana na uchaguzi, ushauri wa wazee kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mada nyingine mbalimbali.

Baadhi ya watoa mada katika kongamano hilo akiwemo mjumbe wa Kamati ya maadili ya Mahakama Kibaha Mjini Joyce Fransis amesema kuwa uchaguzi huo ni muhimu na anaimani kuwa makundi hayo yatakwenda kutoa hamasa kubwa.

Fransis, amesema ni vizuri vyama vya Siasa vikaungana  kuhakikisha wanakwenda kuhamasisha kwa ajili ya kupata viongozi wazuri ambao watasaidia kuleta maendeleo katika jamii.

Hatahivyo, mwenyekiti wa wazee wastaafu Mkoa wa Pwani John Kirumbi ameishukuru ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani kwa kuitisha kongamano hilo kwakuwa litasaidia kuongeza hamasa ya Wananchi kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta akiwa na picha ya pamoja na washiriki wa kongamano la uchaguzi wa Serikali za Mitaa lililofanyika Oktoba 9 Mjini Kibaha.

Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA