MAMA SAMIA AJA NA KAMPENI YA KUTOA MSAADA WA KISHERIA KWA WANANCHI BURE



Na Gustaphu Haule, Tanzania 

MOJA ya maeneo ambayo yanawatesa Watanzania wengi kutokana na kukosa uwezo ni eneo la kupata huduma za kisheria hasa Mahakamani.

Gharama za uendeshaji kesi kwa kutumia Mawakili ni kubwa jambo ambalo limekuwa likiwashinda wananchi wengi wa hali ya chini.



Kwa kuliona hilo serikali ya awamu ya Sita iliyo chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na wadau wengine imekuja na kampeni maalum ya kutoa huduma za kisheria kwa wananchi.

Huduma hiyo inatolewa  bure huku ikipewa jina  kama Mama Samia Legal Aid.



Oktoba 28,2024 Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria wamefanya kikao kazi kilichokusudia kuandaa mkakati wa pamoja wa kutoa msaada wa huduma za kisheria kwa wananchi bure kupitia kampeni hiyo.

Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika  Mkoani Iringa, Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi, amesisitiza umuhimu wa TLS na Serikali kuwafikia wananchi wa pembezoni ambao hawawezi kumudu gharama za mawakili katika masuala mbalimbali yanayohitaji msaada wa kisheria.

Aidha Kampeni ya Mama Samia Legal Aid imejikita katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi, hasa katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, na usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala na masuala yanayohusiana na haki za binadamu kwa ujumla.


Lengo kuu la kampeni hiyo, inayotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini huku ikitarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika jamii na kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wote, bila kujali hali zao za kiuchumi.

Club News Editor - Charles Kusaga

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA