MILIONI 410 ZA MAPATO YA NDANI ZATENGENEZA MADAWATI 4000 KIBAHA MJINI
Na Gustaphu Haule, Pwani
HALMASHAURI ya Mji Kibaha iliyopo Mkoani Pwani imetoa kiasi cha Sh .milioni 410 za makusanyo ya mapato ya ndani kwa ajili ya Kutengeneza madawati 4000 ya Shule za Msingi na Sekondari zilizopo katika Halmashauri hiyo.
Hafla ya uzinduzi wa ugawaji madawati hayo imefanyika leo Oktoba 25 mwaka huu katika viwanja vya Shule ya Msingi Mkoani iliyopo Kata ya Tumbi ambapo mgeni rasmi katika hafla hiyo ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka( katikati) akikata utepe kwa ajili ya uzinduzi wa ugawaji wa madawati, viti na meza 4000 kwa Shule za Msingi na Sekondari zilizopo katika Halmashauri ya Kibaha Mjini ,hafla hiyo imefanyika leo Oktoba 25 kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mkoani iliyopo Kata ya Tumbi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa amesema kuwa ugawaji wa madawati hayo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa awamu ya Sita Dkt,Samia Suluhu Hassan anayetaka kuhakikisha changamoto na kero za Wananchi zinatatuliwa.
Amesema kuwa, fedha zilizotengeneza madawati hayo zimetokana na makusanyo ya mapato ya ndani na mpango huo utakuwa endelevu kwa ajili ya kuhakikisha Halmashauri inaondoa tatizo la upungufu wa madawati, viti na meza kwa Shule zote za Halmashauri hiyo.
Dkt.Shemwelekwa amesema kuwa Halmashauri ya Mji Kibaha inajumla ya Shule 66 za Serikali ambapo kati hizo Shule za Msingi zipo 46 na Sekondari 20 zikiwa na jumla ya wanafunzi 17,424.
Moja kati ya Shule zilizopo Halmashauri ya Mji Kibaha
Amesema, bajeti ya Halmashauri ya Mji Kibaha katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 ilikuwa ni zaidi ya bilioni 7.5 lakini bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 ni zaidi ya bilioni 8.4 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 11 ya bajeti iliyopita.
Aidha, Shemwelekwa ameongeza kuwa makusanyo ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025 katika kipindi cha Julai hadi Septemba ni zaidi ya Sh.bilioni 2.8 sawa na asilimia 33.2 ikiwa ni ongezeko la asilimia 8 ya makusanyo katika kipindi kilichopita.
Amesema kuwa, hali ya uboreshaji wa miundombinu katika kipindi cha Serikali ya awamu ya Sita imedhidi kuimarika kwani katika Sekta ya elimu Halmashauri ya Mji Kibaha imefanikiwa kujenga madarasa 217 na matundu ya vyoo 232 kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 4.3.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dkt .Roger's Shemwelekwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa madawati 4000 kwa Shule za Msingi na Sekondari hafla iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mkoani Kata ya Tumbi ambapo madawati hayo yametengenezwa kwa fedha za mapato ya ndani Sh.milioni 410.
Mbali na hizo lakini Halmashauri imepokea zaidi ya kiasi cha Sh .bilioni 5.1 kwa ajili ya ugaramiaji wa elimu Msingi bila malipo fedha ambazo zimetoka Serikali kuu.
" Leo tunazindua mkakati wa ugawaji wa madawati kwa Shule za Msingi na viti,meza kwa Shule za Sekondari ambapo lengo la mkakati huu ni kuhakikisha tunaondoa kabisa tatizo la upungufu wa madawati,viti,meza katika Shule zetu zote za Halmashauri ya Mji Kibaha," amesema Dkt.Shemwelekwa
Dkt.Shemwelekwa ametoa rai kwa wadau wa elimu kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za Serikali katika Sekta elimu hasa kwenye uboreshaji wa miundombinu huku akiwaomba wazazi na walezi kuhakikisha wanafuatilia mienendo ya wanafunzi kitaaluma, kitabia na hata kuwanunulia vifaa muhimu vya Shule.
Kwa upande Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka awali kabla hajazindua mpango huo amempongeza mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwa kazi kubwa aliyoifanya.
Hafla ya uzinduzi ugawaji wa madawati 4000 yaliyotengenezwa na Halmashauri ya Mji Kibaha kwa fedha za makusanyo ya mapato ya ndani Sh.milioni 410 Oktoba 25, 2024 katika viwanja vya Shule ya Msingi Mkoani Kata ya Tumbi.
Koka, amesema juhudi za mkurugenzi huyo zinaonekana kwani tangu ameteuliwa kuwa mkurugenzi wa Kibaha Mjini ameleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo sambamba na kufanikiwa kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani.
Amemuagiza mkurugenzi kuendelea kukusanya kodi kwa bidii lakini ziwe Kodi sahihi zinazolipika na kufanya Wananchi walipe Kodi hizo kwa hiari na hivyo kuongeza mapato ya ndani ambayo yanasaidia katika uboreshaji wa Mji kwa kujenga miundombinu mbalimbali.
"Mkurugenzi wa Mji ni mgeni lakini kwa kipindi kifupi ameonyesha namna ambavyo amekuwa kiungo muhimu katika Halmashauri kwani kupitia mwenyekiti wa Halmashauri, Mbunge na viongozi wa Chama amefanyakazi kubwa ya kupandisha mapato kwa muda mchache ,"amesema Koka
Amesema kuwa Kibaha Mjini imetoka mbali ambapo wanafunzi walikuwa wanatoka nyumbani na kiti na meza pamoja na ada na kama mwanafunzi akikosa ada alikuwa anafukuzwa Shule.
Amesema kwasasa mambo hayo yamekwisha kwani mwanafunzi akifaulu anakwenda shuleni bila ada lakini kizuri zaidi meza na kiti anavikuta shuleni.
Koka,ameongeza kuwa hali hiyo imetokana na uongozi mzuri pamoja na kazi nzuri ya Rais wa awamu ya Sita Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo katika Sekta ya elimu.
Koka amesema kuwa pamoja na mafanikio ya Sekta ya elimu yaliyopo Kibaha Mjini lakini pia kwasasa tayari milioni 370 zimetengwa na Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya mchepuo wa kiingereza.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Musa Ndomba amemshukuru mbunge huyo kwa kazi kubwa anayoifanya hususani ya kuwapigania Wananchi wake kimaendeleo ambapo amesema baraza la madiwani litaendelea kushirikiana na mkurugenzi ili kuifanya Kibaha Mjini kuwa ya kisasa zaidi.
Comments
Post a Comment