Mpango wa malezi Kiwangwa umeleta matarajio mapya kwa mtoto Amani



Julieth Ngarabali, Pwani.

Katika Mkoa wa Pwani, kijiji cha Kiwangwa, mpango wa malezi, makuzi, na maendeleo ya awali ya mtoto umeleta mabadiliko makubwa kwa mtoto Amani Juma mwenye umri wa miaka saba.

Amani ambaye alikumbwa na changamoto za afya na elimu kutokana na ukosefu wa rasilimali, ameweza kupambana na utapiamlo na sasa anaendelea vizuri katika masomo yake.

Kwa msaada wa huduma za afya na lishe bora zilizotolewa kupitia kliniki za watoto na elimu ya malezi, Amani anaonekana kuwa na maendeleo ya kuridhisha.

Fatuma Juma (43) ni mama mzazi wa mtoto huyo anasema Amani alikumbwa na changamoto za afya na elimu kutokana na ukosefu wa rasilimali na huduma bora, hii ilimfanya kuchelewa pia kuanza shule na kuwa na matatizo ya kiafya kwani alipata utapiamlo miaka mitano iliyopita.

"'mwaka 2018 nilijifungua lakini baada ya mwaka mmoja niligudua kupitia kwa wataalamu wa afya wa kituo cha afya Lugoba kuwa Amani ana uzito mdogo sana usioendana na umri wake''amesema 

Anasema Amani, aliyekuwa kiishi chini ya hali ngumu amepokea matibabu ya muhimu baada ya kupambana na utapiamlo ulioleta changamoto kubwa katika maisha yake.

''Amani, mwenye umri wa miaka saba sasa alihangaika na matatizo ya afya yaliyosababishwa na ukosefu wa lishe bora alikua mnyonge, ngozi isiyo na nuru anaumwa umwa homa hivyo nilipoenda kituo cha Afya Lugoba nikagombezwa sana na Daktari  mtoto sikuwahi kumpeleka kliniki nilikua bize na biashara yangu ya mama lishe, nilipata chanjo,dawa na somo la lishe' anasema Fatuma.

Ametoa simulizi hii kwa mwandishi wa makala haya mara baada ya kushiriki siku ya lishe  kijiji cha Kiwangwa ambapo kijiji hicho na vingine  huadhimisha kwa lengo la kuelimisha umuhimu wa lishe bora kwa watoto chini ya miaka nane kupitia mpango wa malezi na makuzi na wazazi huelekezwa namna bora ya kuandaa pia unga wa virutubisho kivitendo, Idara ya Lishe Chalinze ndio waratibu.

Mama mzazi huyo anasema Amani ambaye yupo darasa la awali sasa badala ya la kwanza  amefaidika na huduma za afya na lishe kupitia kliniki za watoto zilizoko kijijini hapo baada ya mama yake huyo  kupata elimu ya malezi na makuzi kupitia kwenye mikutano ya hadhara inayofanywa na Halmashauri na kwenye baadhi ya vyombo vya habari.

Mwalimu wa shule ya msingi na awali Kiwangwa B anakosoma mtoto huyu,Erasto Mosha anasema mwaka huu Amani ameanza kuonekana mchangamfu tofauti na mwaka mmoja uliyopita na kwamba anaendelea vizuri katika masomo yake na mwezi Novemba mwaka huu  anatarajiwa kuandikishwa darasa la kwanza 2025

Ameongeza kuwa mafanikio haya katika Mkoa wa Pwani kiujumla yanaonyesha jinsi mpango wa malezi, makuzi, na maendeleo ya awali ya mtoto ulivyo na athari kubwa kwenye maisha ya watoto, na umuhimu wa kuendelea kuimarisha juhudi hizi kwa ajili ya maendeleo ya watoto wote.

Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Pwani, Lidya Mafole, amebainisha kwa sasa mkoa huo una vituo 730 vya malezi ya watoto na wamekuwa wakizifuatilia kwa karibu kuona taratibu na kanuni za malezi zinatimizwa .

Ripoti ya afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya Malaria ya mwaka 2022 kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa inaonyesha kwamba asilimia 47 ya watoto wenye umri kati ya miaka 2-5 wanaishi na mama zao wako kwenye muelekeo sahihi wa ukuaji timilifu katika maeneo ya afya, ujifunzaji, na kihisia. Hata hivyo, asilimia 53 ya watoto wa umri huo wanatajwa kuwa hawako kwenye muelekeo sahihi wa ukuaji timilifu.

Hivi karibuni kwenye kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi, na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT MMMAM) kilichofanyika mjini Kibaha. Mwakilishi wa Shirika la Tecden, Christopher Peter, alisisitiza umuhimu wa malezi bora kwa watoto wa jamii, akionya kwamba suala hili linahitaji kupewa kipaumbele zaidi.

Christopher Peter ambaye ni muwezeshaji wa masuala ya watoto kutoka Shirika la TECDEN

Peter alifafanua kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila mwanaume anaambatana na mwenza wake kwenda kliniki, jambo ambalo linaweza kuleta ushirikiano chanya katika masuala ya malezi.

Aidha wadau mbalimbali wa Programu ya PJT MMMAM kutoka Mkoa wa Pwani wamekubaliana kuangalia upya viashiria vya utekelezaji wa programu hiyo.

Wadau hao ni pamoja na asasi zisizo za kiserikali, mashirika ya kimataifa, taasisi za benki, chama cha wafanyabiashara TCCIA, viongozi wa dini, Wizara ya Elimu, Chuo cha Ustawi wa Jamii, na wataalam kutoka Serikali ngazi ya Mkoa wa Pwani. Lengo lao ni kuboresha huduma za malezi, kusimamia ulinzi na usalama wa watoto, na kutoa taarifa za utekelezaji wa shughuli za malezi.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Edna Katalaiya, ametoa maelekezo kwa Halmashauri zote za mkoa huo kuendelea kutekeleza programu ya PJT MMMAM kwa usahihi na kupimana kupitia viashiria vyake.

Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Pwani Edna Katalaiya

 Aliagiza kutengwa bajeti maalum na kufanya tathmini kila robo mwaka ili kupima utekelezaji wa viashiria vilivyokubalika.

Takwimu zinaonyesha kwamba ulimwengu mzima una watoto milioni 250 wenye umri wa miaka chini ya mitano, na robo tatu hiyo ni sawa na asilimia 66 ya watoto hao katika kanda hiyo.

Katalaiya aliongeza kwamba bado kuna changamoto katika uwekezaji wa malezi na makuzi ya watoto, ambapo msisitizo umekuwa kwenye kupunguza vifo badala ya kuzingatia ukuaji wa watoto.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Kusirye Ukio, amekiri juhudi zinazofanywa na Wizara na wadau wa maendeleo katika utekelezaji wa programu hiyo, na kuamini kwamba itachangia kuboresha malezi ya watoto zaidi.

Programu ya PJT MMMAM mkoa wa Pwani imeanza mwaka 2023 na inatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali, Taasisi ya Anjita, Shirika la Tecden, Children in Crossfire, na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kwa pamoja juhudi hizi zina lengo la kuhakikisha watoto wanapata malezi bora na mazingira yenye afya ili waweze kufikia ukuaji timilifu.

Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022, idadi ya watoto wenye umri wa miaka 0-8 nchini Tanzania ni zaidi ya milioni 16 

-----------------------------










Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA