Kisa cha Gabriel na Grace: Safari ya huzuni na matumaini Mkoani Pwani.
Julieth Ngarabali, Pwani.
Katika kijiji cha Chalinze Mkoani Pwani, Gabriel Chumbi na mkewe Grace Petro wamepiga hatua muhimu katika maisha yao baada ya kupitia safari ndefu yenye huzuni.
Kwa miaka mingi walikabiliana na changamoto kubwa ya kupoteza mimba saba mfululizo kwa mujibu wa Gabriel na Grace ambao wameeleza jinsi walivyoishi katika hali hii ngumu.
Gabriel anasema kila mimba ilipofikia kati ya miezi mitano na saba walipata huzuni ya kupoteza mtoto aliyejifungua hali iliyoathiri sana maisha yao ya kila siku.
“Mimba saba amna hata mtoto mmoja, naenda hospitali nikiwa na mimba narudi nyumbani bila mtoto haikua rahisi, ilikuwa kipindi kigumu sana kwangu,” anasema Grace, huku akionyesha huzuni iliyokuwa ikiwakabili.
Hata hivyo, waliweza kutatua changamoto hiyo baada ya kupata mimba ya nane miaka mitatu iliyopita.
Wamesema ni kwa msaada wa wauguzi na madaktari wa hospitali na vituo vya afya waliyokua wakikimbilia ikiwemo Msoga, Tumbi, na Mloganzira ambako walipewa ushauri, maelekezo ya kufanya wakati wote wa ujauzio ulikuwepo ikiwemo kutumia lishe bora, dawa kinga na ya kuongeza damu na virutubisho mwilini.
''Huko tulipata ushauri wa umuhimu wa kuhudhuria kliniki mapema pale tu mama anapopata ujauzito na umuhimu pia wa kutumia kwa usahihi dawa na lishe hivyo kufanikisha kujifungua watoto pacha hawa wawili tulionao na kwa kweli ni hatua iliyoleta furaha kubwa kwa familia yetu'' amesema Grace
Mimba Kuharibika: Vyanzo na Sababu.
‘‘Magonjwa kama endometriosis na fibroids yanaweza kuathiri ukuaji wa mimba ,wakati mabadiliko katika viwango vya homoni vinaweza kusababisha matatizo haya pamoja na matatizo ya kijeni kama ulemavu wa kijeni yanaweza kuchangia kuharibika kwa mimba’’amesema
Aidh mtindo wa maisha pia unachangia,matumizi ya sigara,pombe, na madawa ya kulevya yanahusishwa na hatari kubwa ya kuharibika kwa mimba hivyo kwa jamii kutambua na kushughulikia vyanzo hivi kunaweza kusaidia kupunguza hatari na kuboresha afya ya uzazi.
Jinsi Wajawazito wanaweza kudhibiti hatari ya Mimba kuharibika
Muuguzi mkuu mkoani humo Alfred Ngowi ameeleza kuwa wajawazito wanaweza kuchukua hatua kadhaa kudhibiti hatari ya mimba kuharibika.
Kwanza, ni muhimu kupata huduma bora ya afya na kufuatilia ushauri wa daktari pili wajawazito wanapaswa kula chakula chenye virutubisho vya kutosha, kuepuka pombe, sigara, na madawa ya kulevya, kutekeleza mazoezi ya mwili kwa kiwango kinachokubalika na kuepuka msongo wa mawazo ni muhimu pia.
Ameongeza kutumia vidonge vya asidi ya foliki na kupima afya ya kijeni kabla ya ujauzito kunaweza kupunguza hatari kwa hiyo kwa kuchukua hatua hizi wajawazito wanaweza kuongeza nafasi za kuwa na ujauzito salama na wenye afya.
Mchango wa Serikali na Maendeleo ya Sekta ya Afya
Katika muktadha huu, Serikali ya Mkoa wa Pwani, kwa ushirikiano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya jitihada kubwa kuboresha huduma za afya sambamba na kuongeza idadi ya watoa huduma ikiwemo kada ya wauguzi ambao ni kada muhimu katika kuhakikisha wajawazito wanajifungua salama na watoto wanapata lishe bora na mahudhurio ya Kliniki.Katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa Rais Samia, Mkoa wa Pwani umepokea jumla ya Shilingi bilioni 25 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya.
Fedha hizi zimetumika katika ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, upanuzi wa hospitali, ununuzi wa vifaa tiba, na kuimarisha huduma za magari ya wagonjwa.
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Pwani, Edna Katalaiya, anasema, “Kupokea fedha hizi kumesaidia kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya afya ndani ya Mkoa wetu. Serikali inaendelea kulipa madai ya watumishi, huku ikihimiza maafisa utumishi kushughulikia madai yanayojitokeza.”
Katalaiya pia amewapongeza wauguzi wa Mkoa wa Pwani kwa kazi kubwa wanayofanya na kusema kuwa nguvu kubwa imeelekezwa katika kuwasaidia wauguzi.
“Tumeona maboresho makubwa katika sekta ya afya, lakini bado mambo makubwa yanaendelea kufanyika, na tunampongeza Rais kwa juhudi zake.” Amesema Katalaiya
Changamoto na Matarajio ya Wauguzi
Muuguzi Mkuu Mkoa wa Pwani, Alfred Ngowi, ameiomba Serikali kuhakikisha inalifanyia kazi suala la promosheni kwa wauguzi wenye sifa ili waweze kupata haki zao za msingi na kuongeza morali ya kazi.
Aidha, ameeleza mpango wa kujenga chuo cha uuguzi na ukunga kwa kutumia majengo ya awali ya Halmashauri ya Wilaya Chalinze, huku akiomba msaada wa wadau kwa ajili ya ukarabati na ununuzi wa vifaa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Kusirye Ukio, ameshukuru Serikali kupitia Rais Samia kwa namna anavyotoa fedha katika kuboresha sekta ya afya na kuongeza kuwa kazi inayobaki ni kwa wauguzi kutoa huduma kikamilifu.
“Wauguzi wanaapa kila mwaka kwa ajili ya kukumbushwa wajibu wao, na tunatarajia kuboresha maadhimisho haya kila mwaka kwa faida ya jamii wanayoitumikia,” alisema Dkt.Ukio.
Maoni ya wananchi Kuhusu kisa cha Gabriel na Grace
Salehe Omary ni mkazi wa Kibaha anasema "Kisa cha Gabriel na Grace ni cha kusikitisha lakini pia kinatia moyo kuona jinsi walivyoweza kushinda changamoto kubwa na hatimaye kufanikisha kupata watoto hii ni fundisho kwamba licha ya ugumu wa maisha, matumaini na juhudi zinaweza kuzaa matunda."amesema
Naye Monica Ngasero mkazi w Chalinze anasema "Ni jambo la kugusa sana kuona familia ikikabiliana na maumivu ya kupoteza mimba mara kwa mara lakini ni vizuri kwamba walipata msaada na hatimaye walipata furaha ya kupata watoto pacha hii inatufundisha kwamba msaada wa jamii na kufuata ushauri sahihi wa wataalamu wa afya unaweza kuleta matokeo chanya.
Hitimisho
Safari ya Gabriel na Grace inatufundisha kuhusu umuhimu wa ushirikiano kati ya jamii, sekta ya afya, na serikali. Kupitia msaada wa wauguzi na madaktari, na jitihada za Serikali, walifanikiwa kupokea watoto pacha baada ya kupitia kipindi kigumu. Huu ni mfano wa mafanikio ya pamoja katika kuboresha huduma za afya na kuonyesha jinsi jitihada za Serikali na huduma bora za afya zinavyoweza kubadilisha maisha ya watu.
PJT-MMMAM ni programu Jumuishi iliyoanishwa nchini kwa ushirikiano kati ya serikali na wadau mbalimbali wakiwemo Children in Crossfire (CiC), Mtandao wa Maendeleo ya awali ya mtoto nchini(Tecden) na Muungano wa Klabu za waandishi wa habari nchini(UTPC).
Programu hii inalenga kuyaangazia maisha ya watoto walio na umri wa kuanzia miaka sifuri hadi miaka nane katika nyanja za Afya bora, Lishe bora,ujifunzaji wa awali,ulinzi na usalama pamoja na malezi yenye mwitikio.
--------------------------------------
Comments
Post a Comment