FELISTER MSILLU, AZINDUA ALBAMU YA NYIMBO ZA INJILI, AOMBA WADAU WAMPE SAPOTI,ATAMANI KUMILIKI STUDIO
Na Gustaphu Haule
MUIMBAJI wa nyimbo za injili Felister Msillu, amezindua albamu yake Septemba 8, 2024 huku akiwaomba wadau mbalimbali kumuunga mkono ili aweze kuendeleza kipaji chake cha kumtumikia Mungu.
Uzinduzi wa albamu hiyo yenye nyimbo 11 na video 9 imebeba jina la "Niseme nini mbele zake Mungu" ikiwa na maana ya kuwa Mungu ametenda mengi makubwa na hakuna wa kuweza kumlipa.
Katika hafla ya uzinduzi wa albamu hiyo uliofanyika katika ukumbi wa Mwitongo uliopo Mailimoja Msillu aliambatana na viongozi wa dini kutoka Kanisa la KKKT Mailimoja pamoja na waimbaji mbalimbali wa nyimbo za injili.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya uzinduzi huo Msillu ametaja baadhi ya nyimbo katika albamu hiyo kuwa ni Niseme nini mbele zake Mungu, Mungu mtenda miujiza, Jina la Yesu,Hakuna Mungu kama wewe,na Mungu anamajina mengi.
Msillu, amesema kuwa kilichomsukuma kuimba nyimbo za injili ni kutaka kumtumikia Mungu kupitia nyimbo hizo kwakuwa anaamini nyimbo hizo zitaishi milele .
Amesema kuwa, matarajio yake makubwa ni kujenga studio kubwa ambayo atakuwa anarekodi nyimbo zake pamoja na kuhakikisha anaibua vipaji kwa vijana kupitia nyimbo za injili.
Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Poverty Alleviation for Tanzania Nativers (PATNA) Damasi Msaki (katikati) akizindua albamu ya nyimbo za injili zilizoimbwa na Felister Msillu, hafla hiyo imefanyika Septemba 8, 2024 kàtika ukumbi wa Mwitongo uliopo Mailimoja katika Halmashauri ya Mji Kibaha.
Aidha, amesema kuwa jambo kubwa analokusudia zaidi ni katika kusaidia kuibua na kuendelea vipaji vya kuimba kwa watoto yatima ambao watakuwa wanarekodi bure.
"Ninatamani siku moja nimiliki studio kubwa ambayo itakuwa inafanyakazi ya kuibua na kuendeleza vipaji vya kuimba nyimbo za injili kwa watoto yatima maana naamini wapo vijana wengi wanavipaji lakini wanashindwa kufikia ndoto zao kutokana na kukosa mtu wa kuwashika mkono," amesema Msillu.
Msillu, ameongeza kuwa mpaka sasa tayari amefanya tathmini na ufuatiliaji wa vifaa hivyo na kwamba mpaka kukamilika kwa studio hiyo itagharimu kiasi cha Sh.milioni 20.
Amesema,fedha hizo ni ninyi na kwamba yeye mwenyewe hawezi lakini anaamini kupitia wadau wakiwemo waimbaji wa nyimbo za injili, viongozi wa dini, viongozi wa Serikali na jamii kiujumla wakiungana kwa pamoja lengo hilo litatimia.
Msillu amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kusikia kilio chake na hivyo kuweza kumsaidia kadri ambavyo Mungu atambariki.
Mkurugenzi mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia masuala ya kupambana na umaskini Tanzania (PATNA) Damasi Msaki, amempongeza Msillu kwa kazi kubwa aliyofanya huku akiahidi kuchangia kiasi cha Sh.milioni 1.5.
Msaki ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa albamu hiyo amesema kuwa mtu yeyote anayefanyakazi ya Mungu ni vyema akasaidiwa kwakuwa kazi yake inalenga kuikomboa jamii iliyopoteza matumaini huku akisema Shirika la PATNA litaendelea kumuunga mkono kila wakati.
Hatahivyo, askofu wa Kanisa la Glory of God Ministry lililopo Mtaa wa Kilimahewa Kata ya Tangini katika Halmashauri ya Mji Kibaha Ernest Mrindoko amesema kuwa mafanikio ya kila jambo hupitia katika changamoto.
Askofu wa Kanisa la Glory of God Ministry lililopo Mtaa wa Kilimahewa Kata ya Tangini Kibaha Mjini Ernest Mrindoko akiwa tayari kufanya maombi maalum juu ya albamu ya nyimbo za injili zilizoimbwa na muimbaji Felister Msillu katika uzinduzi uliofanyika Septemba 8, Mailimoja Kibaha Mjini.
Mrindoko,amempongeza Msillu kwa hatua aliyofikia huku akimtaka kuacha kukata tamaa na badala yake asimame katika ndoto zake za kumtumikia Mungu kupitia nyimbo za injili.
Comments
Post a Comment