DR CHAKOU TINDWA AWASHIKA MKONO WAUMINI WA KANISA LA ANGLIKANA MJINI MKURANGA,ACHANGIA ZAIDI YA MILIONI 3 KUJENGA UZIO WA KANISA.
Na Gustaphu Haule, Pwani
MJUMBE wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Pwani Dr.Chakou Tindwa ameungana na waumini wa kanisa la Anglikana lililopo Mkuranga Mjini katika kuendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa uzio wa Kanisa hilo.
Dr.Tindwa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo alichangia papo hapo fedha taslimu kiasi cha Sh.milioni tatu ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika ujenzi wa uzio huo.
Dr.Tindwa ameendesha harambee hiyo juzi kanisani hapo mbele ya viongozi wa wa Kanisa hilo pamoja na waumini mbalimbali waliokusanyika mahususi kwa ajili ya harambee hiyo.
Mbali na kuchangia fedha hizo lakini pia Dr.Tindwa alitoa fedha nyingine kiasi cha Sh.laki nne kwa ajili ya kumuongezea Mwalimu wake wa Shule ya Sekondari Mwinyi ambaye awali aliahidi kuchangia lakini Moja .
"Jamani huyu Mwalimu wangu kwakuwa ameshatoa laki Moja mimi nitamuongezea lakini nne na sasa atakuwa amechangia Sh.500,000",amesema Dr.Tindwa.
Kutokana na hali hiyo Mwalimu huyo alijikuta amefikisha kiasi cha Sh .500,000 ya mchango wake katika kuchangia ujenzi wa uzio huo.
Akizungumza katika harambee hiyo Dr.Tindwa amesema kuwa mchango wake katika harambee hiyo sio mwisho kwani ataendelea kuchangia kadri mahitaji yatakavyokuwa.
Aidha,Dr .Tindwa amewaambia viongozi wa Kanisa hilo kuwa anaamini uzio wa Kanisa hilo utakamilika ambapo ametumia nafasi hiyo kuwaomba wadau wengine kujitokeza kwa ajili ya kuchangia ujenzi huo.
Hatahivyo, viongozi wa Kanisa hilo pamoja na waumini wake wamemshukuru Dr.Tindwa kwa namna alivyojitoa kusaidia Kanisa hilo na hata katika jamii nyingine huku wakimuomba aendelee kusaidia jamii kwakuwa mwenyezi Mungu huwa anawashika mkono watu wanaogusa jamii.
Comments
Post a Comment