WATOTO WATAJA VIBANDA UMIZA NA KAMALI VYANZO VYA UKATILI PWANI
Utitiri wa vibanda vya maonyesho ya video na michezo ya kamali(kubeti) maeneo mbalimbali Mkoani Pwani kumeelezwa kuwa ni baadhi ya vyanzo vinavyosababisha kuenea vitendo vya ukatili na unyanyaswaji dhidi ya watoto.
Mbali na maeneo hayo pia baadhi ya waendesha bodaboda wametajwa na watoto kuwa wamekuwa wakichangia wanafunzi kukatisha masomo kwa kuwapa ujauzito .
Hayo yamebainishwa baadhi ya wanafunzi kutoka shule za msingi na sekondari za Halmashauri ya mji wa Kibaha Mkoani humo kwenye mdahalo uliokuwa na lengo la kujadili masuala mbalimbali ikiwemo ya ukatili yanayowakabili watoto kuanzia umri wa miaka sefuri na kuendelea ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika Mkoani humo
Katika mdahalo huo uliowashirikisha wadau mbalimbali wanaojihusisha na masuala ya watoto mada kuu tatu za ushiriki wa wadau katika kutokomeza ukatili wa jinsia ,wajibu wa wazazi na walezi katika kuwasaidia watoto kuzingatia maadili na ya tatu ni kuwasaidia na kuwapa watoto fursa za ujifunzaji naa stadi za kazi ziliwasilishwa na kujadiliwa .
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki kwenye mdahalo wa kujadili masuala mbalimbali ikiwemo ya ukatili na unyanyasaji.
"Watoto wengine hushindwa kumaliza darasa la saba na sekondari kutokana na mimba za utotoni zinazosababishwa na vishawishi hasa kwa waendesha bodaboda na ngoma zinazoandaliwa na familia"amesema Evelini Mhema wa shule ya msingi Miembe saba.
Kutokana na hali hiyo amesema Seriikali inapaswa kuongeza kanuni ndani ya sheria zilizopo hasa kuwabana watu wanajiweka kando pindi wanapohitajika kutoa ushahidi mahakamani kwani wanasababisha kesi kukosa nguvu na watuhumiwa kuachiwa huru,
"Serikali iweke kanuni za kuwabana wanajamii ambao kwa makusudi wamekuwa wakikwepa kwenda kutoa ushaihidi mahakamani pindi wanapoitwa kwani kuna baadhi ya wanajamii wamekuwa wakifanya hivyo huenda kwa maslahi binafsi"amesema
Aidha Mwanafunzi Johnson Alex amesema njia nyingine inayoweza kuwajenga watoto wasijiingize kwenye maeneo hatarishi ambayo yanawasababishia kutumbukia katika vitendo vya ukatili na unyanyaswaji ni viongozi wa dini kuendesha mihadhara yenye maudhui ya neno la Mungu.
"Wapo baadhi ya watoto hasa wakike wamekuwa wakijirahisisha kwa madereva bodaboda kwa kuomba lifti na hada pesa za chipsi mwisho wa siku wanajikuta wanabakwa na haohao bodaboda kisha wanapata ujauzito hivyo kama watakuwa wanapewa mafundisho ya dini inaweza kusaidia"amesema
"Utakuta kesi inapelekwa mahakamani baada ya hapo mizunguko inaanza mara upelelezi haujakamilika na siku zinakuwa zinaenda na baadaye shauri linakosa nguvu hivyo ni vema serikali ikaliangalia hilo ili kukomesha vitendo hivyo"amesema.
Mkuu wa dawati la jinsia na watoto Mkoa wa Pwani kutoka Jeshi la Polisi Eliezer Hokororo amesema jeshi hilo limejipanga kudhibiti vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanachoomba ni kupata taarifa kwa wakati kutoka kwa wanajamii na kujotokeza kutoa ushahidi.
Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo Katibu Tawala msaidizi uchumi na uzalishaji Mkoa wa Pwani Shangwe Twamala amesema katika kudhibiti vitendo vya ukatili na unyanyaswaji dhidi ya watoto mkoa huo umekuwa ukitumia njia mbalimbali ikiwemo kutoa elimu na ulinzi na kwamba itaendelea kuongeza nguvu kwa kushirikuana na Taasisi mbalimbali
Mdahalo huo Juni 20 /2024 ulienda sambamba na maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika mkoani Pwani ambapo mgeni rasmi alikua Katibu Tawala msaidizi uchumi na uzalishaji Mkoa wa Pwani Shangwe Twamala (katikati waliokaa)
Mwisho
Comments
Post a Comment