Ukosefu wa ‘Buffer zones’ unavyochochea migogoro wanyamapori, binadamu Morogoro
Kutokuwepo mipaka maalum kati ya hifadhi na wanakijiji kumesababisha tembo kuvamia mara kwa mara makazi na mashamba ya wakazi wa Mang’ula, Ifakara.
Na Gustaphu Haule, Kilombero
Septemba mwaka jana tembo wanne waliingia shambani kwa Uyanjo Beda, mkulima na Mkazi wa Kijiji cha Mang'ula" B" katika Halmashauri ya Mji Ifakara wakakata mipapai wakala mihogo na ndizi zilizokuwemo katika eneo hilo.
Siku aliyeenda shambani kwake alikuta mazao yote yameharibiwa na hakuweza kuvuna chochote.
“Kuna siku walikuja nyumbani usiku, nilishtuka kusikia mipapai yangu inaanguka nilipoamka niliona kwa macho yangu tembo wakizunguka nje ya nyumba yangu huku wakitumia mikonga yao kuvunja ndizi na mapapai, hakika niliogopa sana," anasema Beda anayeishi Mita 200 kutoka hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa.
Beda, ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Mlimani iliyopo Kijijini hapo, uvamizi wa tembo kwenye makazi yao ni jambo la kawaida na licha ya kuwekeza nguvu zake katika kilimo lakini mpaka sasa hakuna mafanikio aliyopata zaidi ya kurudi nyuma kiuchumi.
Haya ni maisha ya karibu kila mwanakijiji anayeishi pembezoni na hifadhi katika eneo hilo.
Mkazi wa Kijiji cha Mang'ula, Aisha Ramadhani anasema tembo hutoka mara kwa mara hifadhini na kuingia katika makazi yao hali ambayo inawafanya kuishi kwa hofu ili kunusuru maisha yao.
"Hofu kubwa ni juu ya wanafunzi wetu ambao wanaamka saa 11 :30 alfajiri kwenda shule kwa ajili ya kuwahi namba kwani muda huo wanakutana na tembo barabarani jambo ambalo ni hatari na bila kuchukua hatua dhabiti usalama wa watoto wetu ni mdogo," anasema Aisha.
Uvamizi wa tembo kwenye mashamba na makazi ya watu katika Kijiji cha Mang'ula sio kwa Beda pekee bali kwa jamii nzima kutokana na kijiji hicho kuzungukwa na Hifadhi ya Taifa ya
Milima Udzungwa yenye wanyama wakali wakiwemo tembo, nyati na hata nyani.
Takwimu za Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) zinaeleza kuwa migogoro kati ya binadamu na tembo imeongezeka kwa asilimia 22.3 kutoka 2,304 mwaka 2021 hadi kufikia 2,817 mwaka 2023.
Utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala haya aliyetembelea vijiji vya Mang'ula, Sole, na Sanje umebaini kuwa mashamba na makazi ya watu yapo karibu na hifadhi za taifa za milima ya Udzungwa na Mwalimu Nyerere huku kukiwa hakuna ukanda wa kinga (Buffer zone) inayotenganisha hifadhi na eneo la shughuli za binadamu.
Kwa kawaida ukanda wa kinga ama ‘Buffer zone’ kwa kimombo katika hifadhi na maeneo ya shughuli za kibinadamu unatakiwa uwe Mita 100 mpaka 500 na hii inategemeana na aina ya hifadhi iliyopo katika maeneo husika.
Ukanda Kinga (Buffer zone) ni kigezo kilichowekwa kupitia wataalamu wa mazingira kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kilichowekwa mwaka 1970 na kutangazwa kama BRs (Biosphere Reserves) mwaka 1976 katika hifadhi 368 kwenye nchi 91 duniani. Lengo la kigezo hicho ni kulinda maeneo ya uhifadhi ili yasiweze kuharibiwa na hata kuvamiwa na watu.
Hata hivyo, katika hifadhi ya Milima Udzungwa, hakuna buffer zone baina ya wanakijiji na hifadhi hali ambayo imekuwa ikisababisha madhara kwa binadamu yanayotokana na tembo kutoka katika hifadhi na kuingia katika makazi na mashamba ya wanakijiji.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi katika hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa Abel Mtui anasema hifadhi hiyo ni kweli haina ukanda kinga lakini kwa sasa wanafanya jitihada za kushirikiana na wanavijiji kuweka mpango wa matumizi bora ya ardhi hasa katika maeneo wanayopakana na hifadhi.
Mtui anasema mpango huo utawawezesha wananchi au jamii kutumia ardhi iliyopo karibu na hifadhi kupanda miti ambayo itawasaidia katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na hata kujipatia kipato.
"Lakini kusema unatenga eneo la Ukanda Kinga (Buffer zone) kwa ufinyu wa ardhi uliopo katika bonde letu haitakuwa rahisi ila maeneo makubwa katika hifadhi ya Udzungwa yamepakana na misitu iliyohifadhiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS ) ikiwemo Nyang'anje pamoja na mazingira asilia ya Kilombero (Kilombero Natural Reserve)," anasema Mtui.
"Kwasasa tunaendelea na mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao unaratibiwa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero naamini mpango huu ukikamilika hakutakuwa na kesi za tembo Wala binadamu kuvamia maeneo ya hifadhi," anasema Mtui.
Anaeleza kuwa wanaendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii juu ya kuona umuhimu wa kuheshimu na kulinda maeneo ya uhifadhi. Elimu hiyo hutolewa kwa njia ya gari la sinema huku ikisaidia kutangaza utalii.
Wadau kwa kushirikiana na Serikali wanaendelea na jitihada za kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na binadamu.
Ofisa Ushoroba wa Nyerere Selous -Udzungwa kutoka Shirika la Kusini mwa Tanzania linaloshughulikia masuala ya tembo (STEP) Elizabeth Masatu anasema wameanza kujenga fensi ya umeme kuzunguka sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa lengo likiwa ni kuhakikisha tembo hawatoki na kuingia katika makazi ya watu zaidi ya kupita katika njia iliyowekwa katika ushoroba huo.
Masatu anasema fensi ya umeme itakuwa kikwazo cha tembo kutoka katika hifadhi kwani anapogusa fensi hiyo hupigwa shoti na hivyo kurudi katika eneo la hifadhi jambo ambalo litapunguza wimbi la wanyama hao kuingia katika makazi hayo.
Mbali na wigo wa umeme anaeleza tayari wameanzisha mradi mpya wa ujenzi wa fensi ya nguzo za zege inayoanzia katika Milima ya Udzungwa na kuelekea katika vijiji vya Magombera na Kanyenja kuuziba ushoroba huo wa Nyerere Selous - Udzungwa.
Tofauti na miaka ya nyuma, angalau jitihada zinazoendelea kuchukuliwa kuuongoa ushoroba na kuelimisha wananchi kukabiliana na wanyamapori zimeleta ahueni katika vijiji hivyo.
Fadhili Yahya, mkazi wa Kijiji cha Mang'ula anasema kuwa kabla ya kuimarishwa kwa ushoroba huo tembo walikuwa chanzo cha kufanya wanafunzi wasiende shuleni kwa kuwa walikuwa wanawakuta tembo nje asubuhi lakini ulipoboreshwa ushoroba huo adha ikapungua.
Elimu kwa wananchi haitoshelezi
Kuhusu elimu ya mipaka ya hifadhi, Yahya ambaye ni dereva wa bodaboda anasema hajawahi kupata elimu ya uhifadhi zaidi ya kuona elimu inatolewa shuleni huku akishauri Tanapa waongeze jitihada ya kutoa elimu kwa jamii na shuleni ili kuwaokoa wananchi na athari za wanyama hao.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mang'ula" B "Habibu Lipongola anasema miaka ya nyuma wananchi wake wengi walikuwa wanapata kipato kupitia kazi walizokuwa wanafanya ndani na karibu ya hifadhi ikiwemo kukata miti, kuchoma mkaa na hata shughuli za kilimo.
Kwa sasa, anasema hali hiyo imetoweka katika kijiji chake chenye watu 1,929 kutokana na Tanapa kutoa elimu ya hifadhi iliyohusisha kuheshimu maeneo ya uhifadhi pamoja na kuwashirikisha katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kijijini humo.
Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) unaeleza kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 kumekuwa na mafanikio makubwa hasa katika kuelimisha jamii juu ya kuondokana na tabia ya kutumia vibaya misitu iliyopo karibu nao kwa kukata miti na hata kuchoma mkaa.
Afisa miradi wa Mjumita Kelvin Shirima anasema kwa sasa yapo mabadiliko makubwa yaliyopatikana katika jamii ikiwemo kufanikiwa katika kupunguza tabia ya uvunaji haramu wa mazao ya misitu sambamba na kuviwezesha zaidi ya vijiji 30 kutengeneza mpango kazi wa matumizi bora ya ardhi.
Anasema kutokana na umuhimu wa kazi zinazofanywa na Mjumita hapa nchini mpaka sasa imefanikiwa kuunda Mtandao wa wanachama 129 iliyoundwa na kamati za maliasili za vijiji na vikundi vya kijamii vinavyohusisha na uhifadhi wa Misitu.
Ili kupunguza maumivu ya migogoro baina ya tembo na binadamu, Kaimu afisa mtendaji Kata wa Mang'ula Mohamed Mohamed anasema Serikali inaendelea kuchukua hatua ikiwemo kuwalipa fidia wananchi wanaoathiriwa na wanyama hao na kuimarisha ili kukabiliana na wanyama pale wanapoingia katika makazi ya watu.
Mohamed ,anawataka wakazi wanaokaa karibu na hifadhi au shoroba nchini kutunza mazingira ikiwa pamoja na kuacha kuingia katika maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kukata miti hovyo kwa ajili ya kuni, mkaa, na kilimo.
Kaimu afisa mtendaji Kata wa Mang'ula Mohamed Mohamed akimuonyesha mwandishi wa habari mashamba yaliyopo pembezoni mwa hifadhi ya taifa ya milima ya Udzungwa (Picha Na Gustaphu Haule)
Makala hii ni sehemu ya mafunzo ya uandishi wa habari za bioanuai yaliyofadhiliwa na watu wa Marekani kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaotekelezwa na Nukta Africa.






Comments
Post a Comment