Ngoma za asili zinavyochangia uhifadhi wanyamapori Morogoro


Na Monica Msomba


Wakati wasanii wengine wakiwekeza kuimba nyimbo za mapenzi ili kuburudisha mashabiki wao na jamii, kwa wasanii hawa ni tofauti.  

Wasanii wa ngoma za asili wa kikundi cha Sangula Fagilia Mazingira wamewekeza kuimba nyimbo zinazohamasisha uhifadhi na uendelezaji wa bioanuai wakiwemo wanyamapori. 

Kikundi hiki chenye makazi yake Kata ya Mang’ula ‘B’, Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro kinasifika zaidi kwa burudani inayohusu uhifadhi wa ushoroba wa Nyerere Selous-Udzungwa. 

Kikundi cha ngoma za asili cha Sangula Fagilia Mazingira katika picha ya pamoja na mwanadishi wa makala hii (aliyevaa blauzi ya kijani.)

Ushoroba huo umekuwa ni sehemu muhimu ya wanyamapori kupata chakula, kuzaliana na kupita katika mapitio ya asili kati ya Hifadhi za Taifa za Nyerere na Milima ya Udzungwa na Pori la Akiba la Kilombero. 

Hata hivyo, kutokana na ongezeko la watu, makazi na shughuli za kilimo, vimechangia migogoro kati ya binadamu na wanyamapori wakiwemo Tembo. 

Ili kupunguza migogoro hiyo, nyimbo na ngoma za asili  zimekuwa zikitumika kutoa elimu ya uhifadhi na kutafuta suluhu ya kukabiliana na migogoro hiyo. 

“Kupitia nyimbo zenye hamasa kuna mabadiliko makubwa, wananchi  wemeelewa wameacha tabia za kuingia hifadhini na kukata miti na kuokota kuni tofauti na ilivyokuwa awali ambapo walikuwa wakiingia na kuhariibu mazingira kwenye ushoroba wetu wa Nyerere Selous-Udzungwa,” anasema Deodatus Ngarama, mwenyekiti msaidizi wa Sangula Fagilia Mazingira.

Nyimbo na ngoma za asili za kikundi hiki zimekuwa zikipigwa katika matukio mbalimbali ikiwemo mikutano ya vijiji, mitaani, shughuli za kiserikali na watalii wanapotembelea hifadhi za Taifa zilizopo mkoani Morogoro. 

“Unapofika Udzungwa, kitu cha kwanza kukiona, utaona mali zetu wananchi tumetunza, hasa mlima wapendeza, hata ukiuona kwa mbali utajua  ni ndege tausi, na yeye  ametunzwa” Hiki ni kibwagizo cha wimbo wa utalii wa kikundi cha ngoma  ya Sangula Fagilia Mazingira. 


                Video ya wimbo wa Uhifadhi Maliasili .

Josephine Gwanka,  mchezaji wa ngoma za asili katika kikundi hiki anasema wapo kwa ajili kuhamasisha wananchi na jamii inayowazunguka kutunza hifadhi na kuzuia watu kuingia hifadhini.

“Sisi wote tunashikamana  kwa ajili  ya kuimarisha ulinzi wa misitu. Pia kila mtu anabeba jukumu la kuwa mlinzi wa mwenzake na yeyote anayekamatwa kuingia katika hifadhi anachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa na kufikishwa mahakamani,” anasema Gwanka.

Sheria ya Uhifadhi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) namba 5 ya mwaka 2009 inaeleza kuwa mtu yeyote anayekutwa katika hifadhi akifanya shughuli yoyote ya kibinadamu akikamatwa atakuwa amefanya kosa la jinai na anaweza kukabiliwa na kifungo na kulipa faini kulingana na ukubwa wa kosa.

Kuzaliwa kwa Sangula Fagilia Mazingira

Annastazia Nyang’ali ni katibu msaidizi wa kikundi cha Sangula Fagilia Mazingira anasema  kikundi hicho za ngoma za asili kilianzishwa mwaka 2017 kikiwa na wanachama 16 na hadi mwaka  2024 wamefikia 35.

Wanatoa elimu ya uhifadhi kwa kutumia nyimbo na ngoma za asili katika mikoa ya Morogoro na Iringa.

Pia wanafanya kazi na taasisi za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) na mashirikia yasiyo kuwa ya kiserikali likiwemo Associazione  Mazingira. 

Avenus Kakanga, mpiga ngoma wa kikundi hicho anasema kazi yao kubwa ni kutoa burudani na kuhamasisha utalii katika matukio mbalimbali ya msimu wa sikukuu na hata katika kipindi cha mavuno, sherehe za Serikali na wageni wanapokuja mkoani Morogoro. 


“Jamii imetupokea kutokana na nyimbo tunazoimba kwani zimesaidia kuleta  mabadiliko katika ushoroba wa Nyerere Selous-Udzungwa,  mvua zinanyesha kwa wakati, wanyama tunawaona katika makazi yetu kutokana na hifadhi kulindwa,” anasema Kakanga aliyekuwa akifanya mahojiano na mwandishi wa makala haya.

Mwandishi wa makala haya alipata mafunzo kwa vitendo kuhusu kuripoti habari za bioanuai yaliyoandaliwa na kampuni ya Nukta Afrika kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) kupitia mradi wake wa USAID Tuhifadhi Maliasili.


Kakanga anasema wamekuwa wakipata mapokezi mazuri kutoka kwa watu hasa wanapotumia lugha rahisi ya nyimbo kuelimisha kuhusu kuacha shughuli za kibinadamu zinazotishia kutoweka kwa bioanuai.

Pia kikundi hicho kimekuwa kikipata fursa ya kukutana na watalii wa ndani na nje ya nchi wanaotembelea Hifadhi za Taifa za Milima ya Udzungwa na Nyerere na hivyo kuimarisha utamaduni wa Tanzania.

Ujasiriamali pia unawaweka mjini

Licha ya kikundi hicho cha ngoma za asili kuwekeza nguvu kubwa katika kutoa elimu, pia wamekuwa wakifanya shughuli nyingine za ujasiriamali ili kujipatia kipato cha kuendesha maisha. 

Wanatengeneza majamvi, vyungu, nyungo na vifaa mbalimbali vya sanaa ya mikono ambavyo huuza katika matukio mbalimbali wanayoalikwa. 

“Mara nyingi tunapata hamasa kwa watalii ambao baada ya kumaliza kufanya utalii ndani ya shoroba wanakaa kwa ajili ya kupata burudani ya ngoma ya Sangula yenye ujumbe wa utunzaji wa mazingira na kuwakaribisha wao kama watalii na tunawaonyesha mambo ya asili ya utamaduni,” anasema Ngarama.

  Makamu Mwenyekiti wa kikundi cha Sangula Fagilia Mazingira Deodatus Ngarama.

Mafanikio ya kikundi hicho yametokana na malezi na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa wadau wa uhifadhi ikiwemo  Shirika la  Associazione  Mazingira na mlezi wao Suna Kulolela.

Serikali ya mkoani Morogoro imekuwa ikishirikiana na kikundi hicho kwa mambo mbalimbali na kuwashauri kuendeleza utamaduni wa ngoma na nyimbo za asili ili vizazi vinavyokuja viukute.          

Kaimu Afisa Tarafa ya Mang’ula  Acley Muhenga anasema kikundi hiki kimekuwa kikiwezeshwa na Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Associazione  Mazingira na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa ambapo kazi kubwa ni kuwainua  kiuchumi na kielimu. 

Muhenga anasema sasa hivi wananchi hawawezi kuingia hifadhini kufanya shughuli haramu ikiwemo uwindaji wanyamapori kwa sababu wameelimika na kuna doria za mara kwa mara ambazo zinapunguza uharibifu.  

Kaimu Afisa Tarafa ya Mang’ula katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara Acley Muhenga akizungumza na mwandishi wa makala haya Monica Msomba (hayupo pichani) umuhimu wa kikundi cha Sangula Fagilia Mazingira katika eneo hilo.


Utalii wapaa Milima ya Udzungwa

Kwa mujibu wa takwimu za utalii za Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, hifadhi hiyo imepokea watalii 8,000 katika kipindi cha Januari hadi Machi 2024. Watalii hao wamewezesha hifadhi hiyo kupata Sh300 milioni. 

Idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka na mwaka 2023, hifadhi hiyo ilipata watalii 11,000 ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo walikuwa hawazidi 8,000 kila mwaka.

Hili limetokana na ushirikiano na hamasa ya kutangaza hifadhi hiyo ikiwemo inayofanywa na Sangula Fagilia Mazingira. 

Naye Suna Kulolela, mlezi wa kikundi cha ngoma ya Sangula Fagilia Mazingira ambaye pia ni mwenyekiti wa kikundi cha mazingira cha wanawake kinachojihusisha na uzalishaji wa mkaa mbadala anasema kikundi hicho kipo chini ya Shirika la Associzione Mazingira.  

“Mimi kama mlezi wa kikundi hiki ninawashauri wasibweteke wafanye kazi kwa bidii na wao wenyewe wamewekeana misimamo hasa katika kuhudhuria mazoezi ili inapotokea wamepata mwaliko wanamkata katika malipo na fedha zao zinawekwa  akaunti,” anasema Kulolela na kuongeza kuwa,  

“Nyimbo zinazoimbwa na wanakikundi cha ngoma ya Sangula Fagilia Mazingira kwa kweli zimekuwa na mwitikio mkubwa na mapokeo  ya wananchi kuhusiana na utunzaji wa hifadhi zetu hii pia inafanya watu wasisahau utamaduni uwe unarithishwaa kizazi na kizazi.”

Mkakati wa kikundi hiki ni kujitangaza zaidi ambapo kwa sasa wamejipanga kutengeneza vipeperushi na kuvisambaza kwa watu ili waweze kufahamika nchi nzima.

Pia wamekuwa wakitembelewa na vituo vya redio na televisheni ili kuona namna wanavyopiga ngoma na kuimba nyimbo mbalimbali zenye ujumbe wa uhifadhi.

Kamishina Msaidizi Abel Mtui aliyekuwa Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Milima ya Udzungwa

Aliyekuwa Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Milima ya Udzungwa , Kamishina Msaidizi Abel Mtui  anasema  mfuko  wa uhifadhi wa Tawo la Mashariki ambao wameshirikiana nao katika kuanzisha vikundi  vya ngoma  ambapo kwa sasa viko viwili ikiwamoSangula Fagilia Mazingira na Lizombe.

“Vikundi hivi tunavitumia katika kuhamasisha utalii kwenye hifadhi yetu kwa kukaribisha na kuburudisha wageni na hivi karibuni alikuja Balozi wa Norway vikundi vyote tuliviita  kwaajili ya kuburudisha,” anaeleza.

Hifadhi ya Milima ya Udzungwa imekuwa na uhamasishaji wa utalii wa mbio za furaha na kikundi cha Sangula Fagilia Mazingira kimekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha utunzaji wa hifadhi na ushoroba wa Nyerere Selous-Udzungwa. 




Club News Editor - Julieth Ngarabali

Comments

Popular posts from this blog

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RC PWANI AFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MKURUGENZI WA KIBAHA MJINI DKT.ROGERS SHEMWELEKWA

TANROADS YATOA UFAFANUZI KUTOZWA FAINI GARI LA SIMBA LOGISTICS KITUO CHA MIZANI YA VIGWAZA MKOA WA PWANI