MWEKEZAJI GARDEN KIBAHA MJINI AMLILIA RC KUNENGE




Na Mwandishi Wetu,Kibaha

MWEKEZAJI wa eneo maarufu  la Garden lililopo Kata ya Tumbi katika Halmashauri ya Mji Kibaha Zakaria Jensen amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge kumsaidia kutatua changamoto zinazomkabili ili haweze kufanya biashara yake katika mazingira mazuri .

Jensen,amesema kwasasa anafanya biashara zake kwa mashaka makubwa kutokana na baadhi ya watendaji kutoka katika Halmashauri hiyo kutaka kumuondoa kinguvu katika eneo hilo bila kupewa sababu ya msingi.

Anasema,anachokishangaa kuona baadhi ya watendaji wa Halmashauri wakifanya njama za kumuondoa wakati yeye amepangishwa eneo hilo na Wakala wa barabara Mkoa wa Pwani (Tanroads).

Eneo la garden lililopo Kata ya Tumbi katika Halmashauri ya Mji Kibaha lililowekewa alama nyekundu ya x inayomtaka mmiliki wake Zakaria Jensen kubomoa kama linavyoonekana pichani.

Amesema, eneo la Kibaha Mailimoja na eneo la Tumbi lililopo kando ya barabara ya Morogoro ni eneo la Tanroads na kuna wafanyabiashara zaidi ya 3000 ambao wengi wao wapo kuanzia mita 5 lakini yeye yupo kwenye umbali wa mita 118 lakini chaajabu yeye pekee ndio anayenyanyaswa ili aondoke.

Kauli ya Jensen imeibuka leo Juni 12 wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuvamiwa na wafanyakazi wa Tanesco kwa ajili ya kuondoa Mita ya umeme katika eneo lake bila taarifa yoyote .

"Leo wamekuja watu kutoka Tanesco wakidai wametumwa na baadhi ya watendaji kutoka Halmashauri kung'oa Mita ya umeme na walifanikiwa kufanya hivyo lakini baada ya muda wakarudisha japo nimepata hasara ya vitu vyangu kuharibiwa,"anasema Jensen.

Mmiliki wa eneo la Garden Zakaria Jensen ( kushoto)akihojiwa na mmoja wa waandishi wa habari kuhusu tukio la ukataji umeme katika eneo hilo kwa amri ya mtumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha.

Kwa mujibu wa Jensen , wafanyakazi wa Tanesco kupitia kitengo cha dharula (Emergency) walipewa taarifa  ya kwenda kuondoa mita hiyo kufuatia ombi la barua iliyodaiwa kuandikwa na Jensen ikisema anaomba Tanesco waondoe mita hiyo kwakuwa anataka kuhamisha kontena lake na kupeleka eneo iliyopo benki ya NMB.

Anasema, chakushangaza yeye hajaandika barua hiyo wala hana mpango wa kuhama lakini likaja pia gari la kunyanyua kontena (Crane) jambo ambalo anadai hizo ni hujuma ya baadhi ya watu wanaotaka kuvuruga biashara yake na hata kutaka kumhamisha eneo hilo.

Wafanyakazi wa Tanesco kitengo cha dharula wakishusha ngazi katika gari yao tayari kwa kuondoa mita ya umeme katika eneo la Garden lililopo Kata ya Tumbi katika Halmashauri ya Mji Kibaha linalomilikiwa na mwekezaji Zakaria Jensen.

"Mimi nimefanya uwekezaji wangu hapa kwa kipindi cha miaka nane sasa, lakini mwenye eneo hili ni Tanroads na ndiye aliyenipangisha kwa kufuata utaratibu  ikiwa pamoja na kulipa kodi ya Serikali ya  Sh.1,600,000 kwa mwaka sasa hao Halmashauri sijui wanataka nini kwangu,"anasema Jensen.

Amesema, Serikali ya awamu Sita chini Rais Samia ni sikivu na ipo kwa ajili ya kuwasaidia Wananchi wake na ndio maana wafanyabiashara wanalipa kodi zao bila kushurutishwa lakini wapo watendaji wachache ambao wanamrudisha Rais nyuma.

Jensen, ameenda mbali zaidi kwa kusema uvamizi huo katika eneo hilo umekuwa ukijirudia kwani Agosti 18, 2023 walimvunjia miundombinu yake sambamba na kumpiga virungu lakini Juni 12 ,2024 wamevamia tena kwa kuondoa umeme .

Hii ni picha ya eneo la Garden lililopo Kata ya Tumbi katika Halmashauri ya Mji Kibaha 

Taarifa kutoka kwa kiongozi wa kikosi cha Emergency Tanesco ambaye hakupenda kuandikwa jina lake amesema yeye alipigiwa simu na mtumishi mmoja kutoka ofisi ya ujenzi ya Halmashauri ya Mji Kibaha  sambamba na kutumiwa barua maalum kutoka ofisi yake kitengo cha dharula (Emergency).

"Mimi na kikosi changu nilikuwa Mitamba kwa ajili ya kuweka miundombinu vizuri ya umeme lakini ghafla nikapokea simu  ya mtumishi wa Halmashauri pamoja na barua maalum ili nije hapa kuondoa mita ya umeme ikabidi nije haraka kwakuwa jambo la dharula kama kitengo kinavyojieleza", amesema kiongozi huyo 

Kwa mujibu wa kiongozi huyo namba ya simu aliyopigiwa ni  0757 487 458 mali ya Andrea Charles Dittu kutoka ofisi ya ujenzi ya Halmashauri ya Mji Kibaha.

Mtumishi huyo wa Halmashauri alipopigiwa simu na mwandishi wa habari baada ya kuambiwa kuhusiana na jambo hilo alimtaka mwandishi wa habari kwenda ofisini kwake licha ya kuwa akisema taarifa hizo zipo Wilayani na mkoani.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Rogers Shemwelekwa kwa mujibu wa maelezo yake amesema yeye hajamtuma mtu kufanya hivyo na kwamba yupo safari.

MWISHO.

Club News Editor






Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA