MLAO AWATEGA WABUNGE NA MADIWANI ,ASEMA WATAPIMWA KWA KAZI ZAO,AVUNJA NGOME YA CUF NA CHADEMA MKURANGA.
Na GUSTAPHU HAULE, PWANI
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao amewataka wabunge na madiwani kujiandaa kisaikolojia kwani kurudi au kutokurudi kwa majina yao kutapimwa na kazi zao walizofanya.
Mlao,ametoa kauli hiyo Juni 7 mwaka huu akiwa katika ziara yake Wilayani Mkuranga iliyokuwa inalenga kufanya tathmini ya kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa,Vijiji,na Vitongoji kwa mwaka 2024.
Katika ziara hiyo, Mlao aliambatana na Watendaji mbalimbali akiwemo Katibu wa CCM Mkoa Bernard Ghaty, Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Pwani na Makamu mwenyekiti wa Kamati ya uchumi Dkt. Chakou Tindwa,Katibu wa UWT Mkoa Fatuma Ndee na watendaji wengine.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao,akizungumza na wanachama wa CCM Wilayani Mkuranga ikiwa ni sehemu ya ziara yake aliyoifanya Juni 7 mwaka huu.
Aidha,Mlao alipita katika Kata ya Dondo,Kitomondo,na Kata ya Njia nne zilizopo katika tarafa ya Kisiju ambapo akiwa katika mikutano yake alikutana na Watendaji wa matawi,Kata,wazee maarufu,watumishi wa Serikali,mikutano mikuu Kata,na mabaraza ya Jumuiya zote.
"Madiwani na wabunge jiandaeni kisaikolojia majina yenu kurudi au kutokurudi, CCM itakupima kwa kazi zako, endeleeni kuwajibika, na ukiwa ni mtendaji mzuri wala usihofu",amesema Mlao.
Katika hatua nyingine Mlao amewapokea wanachama wapya 21 kutoka vyama vya upinzani ikiwemo CUF na Chadema sambamba na kuwakabidhi kadi na kuwapa kiapo huku akiwataka wawe wanachama Wazuri na kuyasemea yale yanayofanywa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan .
Mlao amehimiza maadili kwa wanaCCM,umoja na ushirikiano katika shughuli za maendeleo huku akiwataka wanaCCM na wananchi kueleza kazi nzuri zinazofanywa na serikali ya CCM katika maeneo yao.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Pwani Bernard Ghaty ,amewahimiza makatibu tawi, Kata wa Chama na jumuiya zote kufanya ziara mara kwa mara katika maeneo yao ili kuweza kuuwaunganisha wanaCCM .
Ghaty,amewataka wanaCCM na viongozi wote kila mmoja kwa nafasi yake kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa ,Vijiji na Vitongoji ikiwemo kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Katibu wa CCM Mkoa wa Pwani Bernard Ghaty akiwa katika moja ya mikutano waliyoifanya Juni 7 mwaka huu Wilayani Mkuranga .
Mbali na hilo lakini pia Ghaty amesisitiza wanachama wake kujisajili katika madaftari ya mabalozi pamoja na kujitokeza kugombea bila kuogopa huku akivitaka vikao vya mapendekezo na uteuzi ngazi ya Vijiji, Vitongoji na Kata kutenda haki.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi (CCM) Mkoa wa Pwani Dkt. Chakou Tindwa ametumia nafasi yake kuwahimiza wanaCCM wa ngazi ya Matawi na kata kuunda kamati ndogo ndogo za uchumi ili kurahisisha CCM kujiendesha kiufanisi zaidi.
Dkt. Tindwa amesema baadhi ya viongozi waache dhana tofauti za kuwazuia wanachama wenye nia ya kukisaidia chama wakidhani wanautafuta uongozi kwani kila mwanaCCM anahaki ya kukichangia Chama chake.
"Ndugu zangu naomba sana tuungane tuwe kitu kimoja kwa faida ya Chama chetu,hizi dhana za kuwazuia wanachama wenye dhamira ya kukichangia chama wakidhani wanautafuta uongozi ni wazi kuwa tunajirudisha wenyewe nyuma,"amesema Tindwa.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Pwani Dkt. Chakou
Tindwa katika mikutano ya ziara Wilayani Mkuranga.
Hata hivyo,Dkt.Tindwa ameendelea kuwasisitiza wanaCCM wenzake kujenga umoja na ushirikiano ili waweze kujiimarisha kiuchumi pamoja na kukifanya chama kiwe imara zaidi.
MWISHO.
Comments
Post a Comment