MAGUMU YA JOSEPHINE GUNDA NA HARAKATI ZA UDIWANI VITIMAALUM KIBAHA VIJIJINI.



Na Gustaphu Haule,Pwani

UNAPOWATAJA Madiwani wa Viti maalum Mkoa wa Pwani hutakosa kumtaja Josephine Gunda diwani wa viti maalum anayetokea katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini.

Josephine ambaye ni Mkazi wa Kata ya Kwala na mama wa watoto watatu alianza harakati za Kisiasa mwaka 2010 kwenye kinyang'anyiro cha kuwania udiwani wa viti maalum.

Kwasasa Josephine ni awamu yake ya tatu kushika nafasi hiyo tangu alipoanza kuchaguliwa mwaka 2010,2015 na 2020 kupitia Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Kibaha Vijijini.

Katika mahojiano na Mwandishi wa makala haya Josephine anasema kuwa awali kabla hajaingia katika kisiasa alikuwa kiongozi wa moja ya  kanisa lililopo nyumbani kwake Kwala.

Sio uongozi wa kanisa tu,lakini amewai kuwa kiongozi wa masuala ya kijamii akifanyakazi na Shirika la Camfed lililokuwa linashughulika na elimu kwa wanafunzi wakike Kibaha Vijijini.

Anasema ,kilichomvutia kuingia katika Siasa ni baada ya kuona viongozi wa kisiasa namna wanavyoweza kukusanya makundi ya kijamii na kisha  kutatua changamoto zao.

Josephine Gunda diwani wa viti maalum katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini katika harakati za kuhudumia jamii


"Nilikuwa nawaona viongozi wa kisiasa wanakuja hapa Kwala tunapitanao katika Shule za Sekondari na Msingi  na wakati mwingine ukusanya Wananchi katika mikutano na kisha kutatua changamoto zao ndipo na mimi nikapenda,"anasema Josephine 

Anasema,kwakuwa alijiona anauwezo wa  kuwahudumia Wananchi kama ambavyo viongozi wengine wanafanya naye akavutiwa kugombea na hatimaye kushinda.

Anasema, tayari ameshiriki uchaguzi vipindi vitatu na vyote ameshinda lakini anaamini ushindi wake unatokana na uwajibikaji katika jamii,kuwa muwazi ,mkweli, mtetezi wa haki bila kujali makundi ya kisiasa na kuwa mtekelezaji wa ahadi kwa wakati.

 Kuhusu mume wake.

Josephine anasema kikubwa anachofurahia ni kuona mume wake Gunda amekuwa mstari wa mbele pale anapotaka kugombea kwani tangu ameanza kugombea mara ya kwanza amekuwa akipata msaada na ushauri  kutoka kwa mume wake.

"Namshukuru mume wangu amekuwa akinipa moyo na wakati mwingine kunisaidia pale ninapopata changamoto uenda bila yeye nisingekuwa diwani maana alikuwa na uwezo wa kunikataza kugombea lakini kwakuwa muelewa mambo yanakwenda vizuri," anasema Josephine 

Josephine,anasema pamoja na kuwa diwani lakini amekuwa akipangilia vizuri muda wake  kwani kwasasa ametenga muda wa kuhudumia jamii kama diwani na muda wa kuhudumia familia.

Josephine Gunda diwani wa viti maalum Kata ya Kwala katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini katika shughuli mbalimbali za kijamii.


Anasema ,kitendo cha kutenga muda wa utekelezaji wa majukumu yake kumemfanya aweze kutumikia nafasi ya udiwani kwa faraja kwakuwa akitoka nyumbani nyumba inabaki kuwa salama na ndoa inazidi kuimarika.

Kwa upande wa Chama cha Mapinduzi

Josephine anasema ukiachilia mbali familia yake lakini mara nyingi amekuwa akipata nguvu na kutiwa moyo na WanaCCM wenzake kutokana na utayari alionao wa kuwatumikia Wananchi.

"Ndio maana wakati wa uchaguzi ukifika mimi huwa napewa moyo na wapiga kura na wao ndio wananifanyia kampeni bila ya kuwashawishi kwa chochote zaidi kuona kile ninachowafanyia hasa katika kuwatatulia changamoto zao,"anasema Josephine 

Magumu aliyopitia katika uchaguzi.

Josephine,anasema ukiwa mwanamke unaweza kukabiliwa na changamoto nyingi katika uchaguzi ikiwemo rushwa ya fedha na hata rushwa ya ngono.

Anasema ,wakati wa uchaguzi  watu hupewa rushwa ya pesa ili wasimchague kwa maslahi ya mtu fulani lakini  pia kusambaza taarifa mbaya za uongo ili kuwaaminisha wapiga kura ubaya wake.

"Wakati mwingine siasa zilikuwa zinaingia mpaka kwenye ndoa yangu lakini mimi ni mtu wa Mungu kwani hawajawahi kufanikiwa kwakuwa mume wangu  anajitambua na anajua kile ninachofanya ,"anasema Josephine 

Anasema,sio pesa tu lakini hata rushwa ya ngono kwani wapo baadhi ya watu au viongozi ambao walikuwa wanataka  rushwa ya ngono ili waweze kupitisha jina lake.

Anasema,yeye ameweza kukabiliana na changamoto hizo kwakuwa mara zote huwa anamtanguliza Mungu ,kujiamini katika shughuli zake pamoja na wananchi anaowaongoza kufahamu yale anayowafanyia.


Sababu zaidi Wanawake kushindwa kugombea nafasi za uongozi.

Josephine anasema mbali ya rushwa lakini sababu nyingine zinazokwamisha Wanawake kugombea kuwa ni uwezo mdogo wa kiuchumi,kutojiamini na kukatishwa tamaa.

Anasema ,sababu nyingine ni makundi ya kisiasa ,kuwepo kwa mfumo dume pamoja na Wanawake wenyewe kutopendana kwani mara nyingi mwanamke umtia moyo mgombea wa kiume badala ya mwanamke mwenzake.

Anaitumiaje nafasi ya udiwani .

Hapa Josephine anasema mpaka sasa ameweza kushiriki vikao vyote vya kisheria ikiwa pamoja na kuwasilisha changamoto za Wananchi wake .

Pia ,amekuwa akishiriki katika bajeti ya Halmashauri na kuhakikisha vipaumbele vya Wananchi wake vinazingatiwa katika bajeti husika .

Anasema ,pamoja na ushiriki wa vikao hivyo lakini amekuwa mstari wa mbele kuchangia shughuli za maendeleo kwa kutoa pesa,vifaa na hata nguvu kazi kila anapohitajika.

Mpaka sasa Josephine amepita katika Shule mbalimbali za msingi na Sekondari kwa ajili ya kutoa msaada wa taulo za kike, sare za shule,vitabu,madaftari na kalamu kwa wanafunzi zaidi ya 500.


"Wakati mwingine nimekuwa nikitoa asilimia 10 ya posho yangu ya udiwani kuchangia shughuli za maendeleo katika jamii,kuchangia vikao vya Wanawake ikiwemo mabaraza ya UWT Kata,Wilaya ,Mkoa na hata Taifa,"anasema Josephine 

Ushauri kwa Wanawake wenzake.

Josephine anasema Wanawake wanapaswa kujiamini na kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwakuwa uwezo wa kuongoza wanao.

Josephine anatolea mfano kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anafanyakazi bora ndani ya  nchi na hata nje ya nchi.

"Wakati Rais Samia anachukua Kijiti cha Urais wengi walisema hatoweza kwakuwa ni mwanamke lakini ebu angalia leo hii kazi anazofanya ni kubwa na mfano kwa Mataifa mengine,"anasema Josephine 

Josephine,anasema Wanawake wasikubali kukatishwa tamaa ila kinachotakiwa ni kujiamini kwakuwa kila mwanamke anauwezo wa kuwa kiongozi.




Anasema ,yeye yupo tayari kumsaidia mwanamke yeyote ndani ya eneo lake atakayejitokeza kugombea nafasi ya uongozi kwani anaamini kufanya hivyo itakuwa hamasa ya Wanawake wengi kugombea.

Nini matarajio yake ya baadae

Josephine anasema safari ya udiwani kwake ni mwanzo wa kuwa Mwanasiasa mkubwa hapa nchini kwani anatamani uenda siku moja aje kuwa kama Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson.

Josephine anamkubali Dkt.Tulia kwa namna ambavyo analiendesha Bunge kwa kufuata misingi ya Sheria, Kanuni,taratibu na hata katika maadili.

Club News Editor

Comments

  1. Mwenyezi Mungu aendelee kumlinda na kumuongoza ili afikie malengo yake ya kuisaidia jamii na wananchi kwa ujumla

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA