Maboresho ya ushoroba yapunguza maumivu ya tembo Kilombero
Uvamizi wa tembo kwenye makazi ya watu na mashamba yapungua ndani ya miaka mitatu.
Baadhi ya waumini wa Kiislamu na Kikristo wabadili ratiba za ibada kukwepa madhila ya wanyamapori.
Na Gustaphu Haule, Kilombero
Miaka mitatu iliyopita ilikuwa ni kawaida kwa baadhi ya waumini wa kiislamu na kikristo wanaowahi asubuhi kufanya ibada katika Kijiji cha Magombera wilayani Kilombero kukutana na tembo njiani mara kwa mara.
Sehemu kubwa ya wakazi hao walikuwa wanakutana na wanyamapori hao katika ibada zinazoanzia 11:00 alfajiri hadi angalau Saa 2:00 asubuhi.
Mbali na kukutana na waamini hao njiani, baadhi ya wanyama hao walivamia hadi nyumba za ibada ikiwemo makanisa na misikiti.
Ili kuwanusuru waumini hao wa kata ya Mkura, viongozi wa dini katika maeneo hayo walilazimika kubadili muda wa kufanya ibada ili kupunguza hatari za kuathiriwa na wanyamapori hao.
"Tembo wamekuwa wakisumbua sana hapa kijijini kwetu na tunashindwa kuswali swala tano kwa kuwa tunaogopa kuvamiwa, kujeruhiwa na hata kuuawa," anasema Hamad Mtungila, kiongozi wa dini ya kiislamu katika msikiti wa Kijiji cha Magombera.
Waumini wa dini ya Kiislamu kwa sasa, kwa mujibu wa Mtungila, huswali ibada moja ya Ijumaa badala ya swala tano kama ilivyozoeleka.
Mtungila, ambaye ni Mkazi wa Kijiji hicho kwa miaka 32 sasa, anasema muongozo wa dini ya kiislamu unamtaka muumini wake kuswali swala tano kwa siku ikiwemo ibada za usiku, mchana, alasiri na hata jioni lakini kwao ni kama hadithi kwani kwa sasa huswali swala moja tu ya Ijumaa.
Hali ni hivyo pia kwa baadhi ya wakristo wa maeneo hayo. Baadhi ya wakristo nao ratiba zimebadilika baada ya viongozi wao wa dini kulazimika kuondoa ibada ya mikesha ya Pasaka, Mwaka Mpya na Christmas ili kunusuru madhila kwa waumini wa eneo hilo lililopo karibu na Ushoroba wa Nyerere Selous - Udzungwa.
Mchungaji wa kanisa la Pentekoste katika Kijiji hicho Edward Sika alilieza Coast Press kuwa kwa sasa ibada yao inafanyika siku ya Jumapili pekee tofauti na miaka ya nyuma walipokuwa na ratiba mbalimbali za ibada.
Sika anasema miaka ya nyuma wanyama hao hawakuwepo lakini ilipofika mwaka 2007 mpaka 2010 ndipo usumbufu wa wanyama hususani tembo ukaanza.
Anasema baada ya usumbufu wa tembo kuanza ratiba za ibada na mfumo mzima wa maisha ya Wanakijiji wa Magombera nao ukabadilika ikiwa pamoja na kuvunja baadhi ya ratiba za ibada za usiku na mikesha ya mwaka mpya na pasaka.
"Sisi hatufanyi ibada za mikesha ya Pasaka wala Mwaka Mpya, tumeamua kuvunja ratiba hizo sio kwa makusudi bali kwa sababu ya kuepuka na madhara yatokanayo na tembo wanaovamia nyumba zetu za ibada," anaeleza Sika.
Matumaini mapya yaja
Hata Hivyo, angalau sasa wanakijiji hao wameanza kupata ahueni ya maisha baada ya Serikali, mashirika na taasisi binafsi na wadau wengine wa uhifadhi wakiwemo wananchi wa kijiji hicho kuchukua hatua za kuuongoa ushoroba huo wa Nyerere Selous - Udzungwa.
Watalaamu wanasema moja ya sababu zilizochochea migogoro baina ya wanyamapori kama tembo na binadamu ni kuharibiwa kwa ushoroba huo kwa kufanya shughuli za kibinadamu kama ujenzi wa makazi, kilimo na shughuli nyinginezo.
Ushoroba ni njia ya wanyamapori kutoka eneo moja la hifadhi kwenda jingine kwa ajili ya kutafuta chakula, maeneo ya kuzalia au sababu nyinginezo za kiekolojia.
Katika kuungoa ushoroba huo, Serikali na wadau wa uhifadhi wekiwemo Shirika la uendelezaji Program ya Tembo Kusini mwa Tanzania ( STEP) wamechukua hatua za kurejesha ardhi iliyokuwa inatumika kwa shughuli za kibinadamu ili wanyama wapite kwenye eneo hilo na wasiende mtaani na kudhuru wakazi wa maeneo hayo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Magombera Said Simba anasema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita hakuna tukio la mtu kujeruhiwa wala kuuawa na wanyamapori lakini katika kipindi hicho tembo nane wameuawa kwa kugongwa na treni kati ya mwaka 2022 na 2024.
Hatua za kuimarisha ushoroba anasema zimeongeza usalama wa wananchi wake na mabadiliko yanayozidi kuimarika katika Kijiji chake yanatokana na hatua kubwa ya kuimarisha Ushoroba wa Nyerere Selous -Udzungwa mradi unaosimamiwa na STEP kwa ufadhili wa Watu wa Marekani chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.
Uongoaji ushoroba waleta ahueni
Wadau wa uhifadhi wanaeleza kuwa uongoaji wa ushoroba huo utazidi kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na binadamu na kurejesha shughuli za kijamii na kiuchumi kama ilivyokuwa awali.
Ofisa Ushoroba wa Nyerere Selous -Udzungwa kutoka Shirika la STEP Elizabeth Masatu anasema wanaendelea kuimarisha fensi katika ushoroba huo ili kuweza kupunguza adha ya wananchi inayotokana na tembo kuvamia katika maeneo yao .
Hii ni fensi ya bati iliyowekwa na Shirika la uendelezaji Programu ya Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP)katika Kijiji cha Magombera Kata ya Mkura Wilayani Kilombero ikiwa ni sehemu ya kuzuia Tembo katika Ushoroba wa Nyerere Selous -Udzungwa wasitoke katika makazi na mashamba ya wananchi wa Kijiji hicho .picha na Gustaphu HauleMasatu anasema awali walijenga fensi ya nyuki na baadae kujenga fensi ya mabati lakini fensi zote hizo zimeleta mabadiliko kidogo licha ya kuwa fensi ya mabati imesaidia kwa kiwango kikubwa.
Ili kuhakikisha ufanisi zaidi wa kudhibiti wanyamapori, anasema wanazidi kuimarisha ushoroba huo hasa kwa kuhakikisha wanajenga fensi imara ambazo zitamzuia tembo kutoka katika eneo la mapito hayo yanayounganisha Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa na Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere.
"Tumefanya majaribio mengi ya kujenga fensi katika ushoroba huo, tulianza na fensi ya pili pili, ikaja fensi ya nyuki na baadae fensi ya mabati lakini kwa sasa tumeanza na ujenzi wa fensi ya zege ambayo imeanzia Udzungwa na kuelekea katika Kijiji cha Magombera eneo ambalo ushoroba huo umepita," anasema Masatu.
Hii ni fensi ya Zege inayojengwa katika Ushoroba wa Nyerere Selous -Udzungwa kupitia Shirika la uendelezaji wa programu ya Tembo Kusini mwa Tanzania ( STEP) ikiwa ni sehemu ya kupunguza adha ya tembo kuvamia makazi ya binadamu na mashamba,Picha na Gustaphu HauleTochi zaendelea kuwa msaada
Mbali na hatua za muda mrefu za kuboresha ushoroba, wakazi wa eneo hilo wamekuwa na tochi zenye mwanga mkali kuwadhibiti tembo ambao hutumika kuwamulika machoni tembo mara tu wanapoonekana katika mazingira na kuwakimbiza.
Pamoja na mbinu ya tochi lakini mbinu nyingine ni ile ya kupiga debe, debe hupigwa na wananchi hao pale wanapowaona tembo kwa kuwa tembo huogopa kelele na wanaposikia kelele hizo hukimbia.
"Sisi tunapambana na wanyama wakali kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo ya kupiga madebe, kutumia tochi ya mwanga mkali zinazouzwa TSh 15,000 na hata kuwasha moto wa magogo ya miti usiku kucha ," anasema Shaban Juma mkazi wa Kijiji cha Magombera akieleza zaidi kuwa tembo wanapoingia katika makazi ya watu hufuata chakula hususani ndizi, embe, mpunga, mhogo, mapapai na mbaazi.
Anasema tembo wanapoingia katika mashamba yao na kuharibu mazao inawaathiri kiuchumi kwa kuwa wakati mwingine mkulima hukopa fedha sehemu wakitegemea kurudisha pale wanapovuna lakini hali inakuwa tofauti.
"Tembo wanatufanya tukimbie hapa kijijini kwa sababu ya madeni kwani tunapokopa tunategemea kuvuna ili tulipe madeni lakini wanapoingia shambani na kuharibu mazao hali zetu zinakuwa mbaya na hivyo kulazimika kukimbia makazi yetu," anasema Juma.
Mzee wa kimila katika Kijiji hicho Hussein Likwina (79) anasema miaka ya nyuma walikuwa wanatumia njia ya kimila kuzuia tembo wasiingie katika makazi wala mashamba ya wakulima kwa kutumia dawa za miti shamba kufunga katika mipaka au njia za kupitia wanyama.
Mwandishi wa makala haya Gustaphu Haule ( kushoto) akifanya mahojiano na mzee wa kimila katika Kijiji cha Magombera Kata Mkura Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro Hussein Likwina(Kulia)aliyefika Kijijini humo kwa ajili ya kujua namna ambavyo mbinu za kimila zinavyoweza kusaidia katika kupambana na wanyama wakali wakiwemo tembo .
Kwa mujibu wa Likwina tembo anapofika alikuwa anakutana na harufu mbaya na hivyo kurudi alipotoka.
Licha ya kuwa matukio ya tembo kuvamia kijiji yameendelea kupungua lakini Mwenyekiti wa Kijiji cha Magombera Simba anasema bado wamekuwa wakisumbua zaidi katika kipindi cha Julai hadi Desemba.
Vijana wanolewa kulinda kijiji
Simba anasema pamoja na wananchi kutumia mbinu zao mbalimbali lakini kijiji kimeunda mpango maalum wa ulinzi kupitia vikundi vya wakulima ambapo mpunga unapoiva huwa wanashirikiana kulinda wakiwa na vijana 10.
Vijana hao wamepata mafunzo ya ulinzi kutoka Tanapa (VGS) waliotoka Kijijini humo ambao wamesomeshwa na Serikali kupitia Tanapa kwa ajili ya kudhibiti tembo na hata kulinda usalama wa wanakijiji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Magombera Said Simba akitembelea ofisi yake mpya inayojengwa Kijijini hapo mara baada ya kuzungumza na mwandishi wa habari aliyefika Kijijini hapo kwa ajili ya kujua namna ambavyo Wanakijiji hao wanavyopambana na wanyama wakali .picha na Gustaphu Haule
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Dunstan Kyobya anasema wanatambua kuwepo kwa changamoto kubwa ya kuwepo kwa migogoro ya binadamu na wanyamapori katika wilaya yake lakini Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuipunguza kabisa.
Serikali yajitosa kumaliza migogoro
Kyobya anasema miongoni mwa mikakati mbalimbali kutatua migogoro hiyo ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu tabia za wanyamapori pamoja na njia salama za kujikinga na hata kuepuka migogoro.
Elimu hiyo inatolewa kwa njia ya warsha, semina, mafunzo juu ya maarifa na tabia za wanyamapori, kusambaza vipeperushi. mabango na hata kupitia ngoma za wasanii mbalimbali.
Taarifa kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TAWA) inasema kwasasa wanaendelea kufanya kampeni kwa jamii inayopitiwa Ushoroba wa Nyerere Selous -Udzungwa kwa ajili ya kuwaelimisha juu ya umuhimu wa hifadhi za taifa, mazingira na namna ya kuepuka migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Njia zinazotumika ni ufuatiliaji wa wanyamapori mara kwa mara katika hifadhi za Taifa za Mwalimu Nyerere, Pori la Akiba la Selous na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, njia inayosaidia kutambua maeneo yenye migogoro mingi kati ya binadamu na wanyamapori na hivyo kuchukua hatua za kuzuia.
Makala hii ni sehemu ya mafunzo ya uandishi wa habari za bioanuai yaliyofadhiliwa na watu wa Marekani kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaotekelezwa na Nukta Africa.
MWISHO
Comments
Post a Comment