Jinsi kamera zinavyosaidia kurejesha uhusiano kati ya binadamu na tembo Shoroba ya Nyerere Selous-Udzungwa
Na Julieth Mkireri, Ifakara
Inawezekana kabisa usiwe mgeni wa njia ya barabara ya Ifakara-Mikumi. Ikiwa umewahi kupita hapa, bila shaka umekutana na moja ya alama muhimu – bango la Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa likiwa na maneno “Welcome to Udzungwa National Park.”
Ukiwa unatoka Ifakara kuelekea Mikumi, bango hili lipo upande wako wa kushoto unapofika Mang'ula, na ukiwa unasafiri kutoka Mikumi kuelekea Ifakara, bango hilo lipo upande wako wa kulia.
Lakini usilolifahamu ni kwamba mbele kidogo ya bango hilo, kuna ushoroba wa Nyerere Selous-Udzungwa. Hii ni njia muhimu inayotumiwa na wanyama, hususan tembo, kutoka Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa kwenda Hifadhi ya Nyerere Selous.
Ili kuhakikisha ushoroba huu unakuwa salama kwa wanyama na binadamu, hatua mbalimbali za kuboresha mazingira zimechukuliwa. Hii ni pamoja na ufungaji wa kamera na ujenzi wa miundombinu rahisi ya kupita wanyama
Amina Mohamed, mkazi wa Mang’ula B, anasema ufungaji wa kamera katika ushoroba utasaidia kutambua tembo wanaopita katika njia zao, na pia kubaini majangili wanaoingia kinyume cha taratibu.
"Tuna taarifa kwamba kamera zimefungwa hifadhi ya Udzungwa. Kwetu tunaona itasaidia kutambua ni tembo wangapi wanapita na wanatumia njia gani ili ziwekewe uzio wasituathiri sisi wananchi tunaoishi karibu na hifadhi," anasema Amina.
Habibu Lipogola, mwenyekiti wa kijiji cha Mang’ula ‘B’, anaongeza kuwa uwepo wa kamera katika ushoroba wa Nyerere Selous-Udzungwa utasaidia kubaini njia halisi za tembo na itarahisisha kuweka uzio kuzuia tembo kuingia kwenye makazi ya wananchi.
Joseph Mwalugelo, Meneja wa Ushoroba wa Nyerere Selous-Udzungwa kutoka shirika la Southern Tanzania Elephant Program (STEP) anasema ushoroba huo wenye urefu wa km 12.6 na upana wa mita 150 hadi 200 ulianzishwa kupitia Sheria ya Uhifadhi ya mwaka 2009 na kanuni ya 2018, kwa lengo la kuhakikisha usalama wa tembo na binadamu.
Ushoroba huu unapita katika vijiji vitatu – Mang’ula, Sole, na Kanyenja. Kutokana na madhara yaliyokuwa yakitokea kati ya binadamu na tembo, STEP walifanya tafiti na kufunga kamera sehemu ambazo tembo wanapita, ikiwemo kijiji cha Magombera.
Teknolojia ya kutengeneza njia za chini za kupita wanyama ilichukuliwa kutoka Kenya, ambapo kwa mwaka mmoja tembo 1000 walipita katika njia hizo. Hali hii ilisababisha sasa kujenga njia za chini ili kuepuka vifo vya tembo vilivyotokea awali kutokana na kugongwa na magari.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa, Abel Mtui, anasema shughuli nyingi zinazofanyika ni pamoja na urejeshwaji wa njia za tembo. Baada ya kuanzishwa kwa ushoroba, baadhi ya wananchi wenye mashamba walifanyiwa tathmini na kulipwa fidia kupisha njia za wanyama.
Ushoroba huu unaosimamiwa na Shirika la STEP, ulifanyiwa tafiti kabla ya kufungwa kamera. Kamera hizo zilianza kuwekwa tangu mwaka 2018 na hadi sasa zimefikia 25.
STEP wanaendelea kuziweka kwenye maeneo ambayo yamefanyiwa utafiti na baadhi ya wanyama wameonekana wakiwemo nyati na tembo zaidi.
Afisa Ushoroba Shirika la Uhifadhi tambo kusini mwa Tanzania STEP (mwenye fulana ya bluu) Elizabeth Masatu na mmoja wa Waandishi Habari wakielekezwa namna kamera zinavyofungwa kwa ajili ya kubaini njia za tembo Shoroba ya Nyerere SELOUS--Udzungwa
Kamera hizo zinasaidia kubaini mapito ya tembo na kuweka uzio ili wanyama hao wasiingie kwenye makazi na mashamba. Katika maeneo ya barabara kuu, njia za chini zilijengwa ili wanyama wasipite juu ya barabara.
“Ushoroba wa Nyerere Selous-Udzungwa unatarajiwa kuwa shamba darasa la kujifunzia kwenye maeneo mengine, kutokana na kuwawezesha wanyama kuwa katika hali nzuri,”anasema Mtui.
Anasema Ushoroba huo utakuwa kivutio cha watalii kwani watu watapata fursa ya kuwaona tembo wanapopita kwenye njia zao.
Pia, wawekezaji watawekeza katika maeneo hayo na uchumi utakua kwa pande zote, kwa serikali na watu binafsi.
Kamera hizi pia zinasaidia kuzuia uhalifu, kwani yeyote anayeingia na kutoka katika ushoroba ataonekana. Katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira, Hifadhi ya Udzungwa ina kitengo cha ujirani mwema ambacho kimekuwa kikitoa elimu kwa wananchi na kimesaidia wengi kuachana na vitendo vya kuingia kwenye hifadhi na kufanya shughuli za kibinadamu.
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii hivi karibuni ilitangaza mikakati ya kuokoa ushoroba 20 kati ya 61 zilizotengwa ili kuwalinda wanyama pori pamoja na kuondoa mgongano kati ya binadamu na wanyama.
Moja ya ushoroba hizo ni Nyerere Selous-Udzungwa inayopita katika Hifadhi ya Milima ya Udzungwa iliyopo Ifakara, mkoa wa Morogoro. Waziri wa Maliasili na Utalii, Angela Kairuki, alisema kukosekana kwa uangalizi wa kutosha kwenye ushoroba kumekuwa kukichangia migogoro ya mara kwa mara.
Comments
Post a Comment