TEMBO WANAVYOWANYIMA USINGIZI WANANCHI WA MANG'ULA B. MOROGORO
Julieth Ngarabali, Kilombero
“Nilikosa usingizi kwa siku mbili usiku baada kumshuhudia Tembo akiingiza mkonga wake kwenye chumba cha jikoni na kuchukua Fenesi na kuanza kulila’’
‘’Tukio hili nilishuhudia mwanzoni mwa mwaka huu 2024 wakati nilipoenda nyumbani kwa bibi yangu kumsalimia huko katika kijiji cha Mangúla B. Wilaya ya Kilombero hakika nikawa naogopa sana.’’
Hii ni kauli ya mkazi wa Kitongoji cha NDC, Kata ya Mang’ula, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Halima Ally alipokuwa akisimulia matukio ya Tembo kuingia kwenye makazi yao.
Tukio hilo lilimjengea hofu Halima kila ilipofika usiku. Kila akilikumbuka anahisi kama tembo anaweza kurudi tena.
Hata hivyo, bibi yake Halima aitwaye Fatuma Rajabu alimweleza kuwa si tabia ya Tembo kuingia hovyo katika nyumba za watu isipokuwa pale tu anapohisi harufu ya matunda yakiwemo mafenesi na ndizi.
‘Yaani kumbe Tembo anaweza akaja nyumbani kwako, kama hakuna matunda yenye harufu hawezi kuingia ndani, lakini akisikia tu harufu mtakua kwenye hatari maana lazima atataka alichukue tu, hivyo tusiweke matunda ya aina hiyo ndani ili tulale salama,” anasema Halima.
Msemo huu wa kukosa usingizi pia umekua ukitumiwa na wananchi wa Kijiji cha Mang’ula B, Wilaya ya Kilombero mkoani humo kutokana na Tembo ambao huingia katika mashamba na makazi ya watu na kufanya uharibifu.
Hali hiyo imekuwa ikiwafanya wakose usingizi kwa sababu wanalazimika kutumia muda mwingi kufikiri namna ya kukabiliana na mnyama huyo.
Nini shughuli kuu ya kiuchumi Kijijini Mang’ula B
Shughuli kuu ya wananchi wa Kijiji cha Mang’ula B ni kilimo cha mpunga ambacho wamekuwa wakikitegemea kujiingizia kipato.
Mazao mengine ni ya mizizi ambayo yanapandwa baada ya mavuno ya mpunga. Mazao hayo ni muhogo, viazi, maharage, mikunde na mbaazi.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho kilichopo ushoroba wa Nyerere Selous-Udzungwa wanasema kila wanachokifanya katika kilimo, mafanikio yao yanakua kidogo. Wakati wa maandalizi ya mashamba Tembo hua huingia shambani kwa hiyo mtu anashindwa kufika kwa wakati shambani.
“Kuna siku umeme ulizima kukawa na giza, Tembo ndio hufanya vizuri mambo yao walikuja siku hiyo eneo la nyumbani kwangu wakavamia wakakatakata migomba, mipapai na mihogo niliposhtuka wameshafanya uharibifu mkubwa hakuna chochote kilichobakia shambani nilitegemea kwa matunda na chakula maana bado sina familia kubwa,” anasema Mkazi wa Kitongoji cha Mlimani, Uyanjo Beda na kuongeza
‘’...nilikasirika sana kwa kweli lakini nafanyaje sasa nilibaki tu na mawazo kibao kichwani hata kulala silali vizuri nawaza nikipanda tena hawa jamaa Tembo si watakuja tena maana hujui siku wala saa hasa nyakati za kiangazi, haya ndio maisha yetu sisi.”
Mwanahawa Omary, mkazi wa Kitongoji cha Madukani, Kata ya Mang’ula anasema amekuwa anatumia muda mwingi kufikiria uvunaji salama wa mazao yake kwa sababu anapanda mazao na akishapanda mpunga, mahindi na migomba Tembo wanapoingia kijijini wanaenda kukanyaga au kula mazao.
‘’Sasa hii hali ya uharibifu wa Tembo nakosa kabisa uhakika wa chakula na kipato kwa ujumla apo sasa napataje usingizi? nabaki nawaza nitaishi vipi na familia yangu, chakulla kimeharibiwa na kama biashara unauza nini hakuna tena hapo ni kulalamikia tu hii hali ya Tembo kuja maeneo yetu,” anasema Mwanahawa.
Naye Alawi Seif mkazi wa Kitongoji cha NDC anasema Januari mwaka 2024, Tembo waliingia shambani kwake wakaharibu mahindi ekari moja na nusu.
‘’Nakumbuka ilikuwa Januari 9, 2024 nilipoamka asubuhi kuelekea shambani kwanza nilianza kuona vinyesi vya Tembo njiani nikajua leo jamaa wameingia lakini sikujua wameharibu kwa kiasi gani mazao yangu. Alooh nafika shambani mahindi yameharibiwa mengine yamekanyagwa kanyagwa huku mengine yameliwa nikaishiwa nguvu,’’ anasema Seif huku akiinamisha kichwa chini.
Idadi ya wakazi wa kijiji hiki
Kijiji hiki cha Mang”ula B kina Jumla ya wakazi 1,929 na kimekuwa na changamoto ya kuvamiwa na Tembo kutokana pia kuwa jirani na hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Pori la Akiba la Kilombero.
Kutokana na changamoto hii imekuwa ikiwalazimu wanakijiji wa Mang’úla B kujihami na Tembo usiku kwa kugonga vipande vya bati.
Pia wamekuwa wakikaa nje ya nyumba zao wakiwasha mwanga mkali wa tochi na kuwamulikana Tembo. Hapa ndio wakati mwingine wanakatisha usingizi ili tu kulinda mali na wao wenyewe.
Takwimu za kitaifa za migogoro ya wanyamapori na binadamu
Kwa mujibu wa Takwimu za Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) za 2021/22, migogoro kati ya binadamu na wanyamapori imeongezeka kutoka 2,304 kwa mwaka 2021/22 hadi kufikia 2,817 mwaka 2022/23.
Hiyo ni sawa na kusema migogoro imeonezeka kwa asilimia 22.3 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Wizara ya Maliasili na Utalii inaeleza kuwa migogoro ya binadamu na wanyamapori kwa kiasi kikubwa husababishwa na kuwepo kwa matumizi ya ardhi yasiyozingatia mpango bora wa matumizi ya ardhi hasa baadhi ya watendaji wanaohusika na kugawa ardhi kutotimiza wajibu wao kwa kuzingatia miongozo iliyopo.
Pia kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu hususan katika maeneo yanayopakana na hifadhi za wanyamapori, shoroba za wanyamapori na maeneo ya mtawanyiko ya wanyamapori kuvamiwa na wananchi.
Uchungaji wa mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa; na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ukame wa muda mrefu na hivyo kusababisha baadhi ya wanyamapori kutoka nje ya hifadhi kwa lengo la kupata mahitaji nje ya hifadhi.
Ni wakati gani tembo wanavamia makazi ya watu?
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mang’ula B Ally Lipungula anakiri kuwa Tembo bado wanaingia katika makazi ya watu ambapo mara ya mwisho kwa mwaka huu wa 2024 waliingia kijijini hapo Januari na Februari.
Anasema Tembo wamekuwa wakiingia kijijini kwa nyakati tofauti ambapo imekuwa ni kuanzia majira ya saa 12.30 jioni ama wakati mwingine saa mbili usiku.
Kunapokucha wanyamapori hao huanza kurudi kwenye hifadhi asubuhi kuanzia majira ya saa 11 asubuhi mpaka 12 na hapo ndio wananchi wanakua huru kufanya shughuli zao nje ya makazi yao.
Lipungula anasema kutokana na Tembo kuingia kijijini, watu wamekua na taharuki na baadhi kupatwa na uoga hivyo wanashindwa kulala vema au kukosa usingizi kabisa.
“Unajua hawa wanyama kuingia kwao kijijini hua ni usiku kwa yule mtu ambaye anakua bado hajalala lazima atawasikia na lazima atapata wasiwasi kwamba sijui itakuaje hapa,” anasema Lipungula.
Mwenyekiti Lipungula ametoa mfano kuwa Januari 2024 Tembo waliingia kijijini hapo na wengi walionekana eneo la Ofisi ya Kijiji cha Mang’ula B na Kitongoji cha NDC.
‘’Hali ilikuwa mbaya yaani Tembo walikua wanafululiza kuingia kwenye makazi ya watu yaani kuanzia Desemba,, wakiingia wakati mwingine saa 1.30 usiku tu wanaingia na saa 11 alfajiri wanaanza kuondoka kwenda kwenye hifadhi, walikuwa wanasumbua sana kwa kweli kipindi hiki,’’ anasema.
Anabainisha kuwa hali hiyo ilileta taharuki kubwa lakini amelishukuru Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana nao wakawafukuza wakarudi kwenye hifadhi na tangu Februari 2024 Tembo hao hawajarudi tena katika makazi ya watu.
Naye Kaimu Mtendaji Kata ya Mang’ula B Mohamed Mohamed anasema misimu ya Tembo kuingia katika mashamba na kufanya uharibifu kijijini Mng’ula B ni nyakati za misimu ya mavuno na baada ya mavuno Tembo huzagaa na kuwa wengi.
Anasema nyakati za mavuno ni mwezi wa Juni mpaka Desemba. Kipindi hiki Tembo hua ni wengi sana kwa sababu wakulima wanakua wameshavuna na msituni chakula kina kuwa kime kwisha, hivyo Temba huzagaa katika makazi ya watu kusaka chakula.
Mohamed anaongeza kuwa hali hii huenda mpaka mwezi Februari ambapo unakua msimu wa masika mvua zinakua nyingi hivyo Tembo ndio hushindwa kutoka kwenye hifadhi kwa sababu mashamba mengi yanakua yanatitia.
“Mara tu mafuriko yakianza mwezi wa tatu Tembo wanashindwa kutoka ndani ya hifadhi kwa sababu mashamba mengi yanakua yanatitia kwa hiyo wanashindwa kuingia na pia matunda ndani ya hifadhi yanakua mengi hivyo hawatoki kuja kufanya uharibifu kwa jamii,” anasema Mohamed.
‘’Kiangazi kinapoanza Tembo wanakua wengi. Mazingira yenyewe yanawaruhusu kupita kila mahali bila changamoto, lakini wakati wa msimu wa mvua wanaogopa kuzama chini,” anasema.
Wadau wa uhifadhi wataja mikakati kudhibiti Tembo
Afisa Ushoroba wa Shirika la Uhifadhi wa Tembo la Kusini mwa Tanzania (STEP) Elizabeth Masatu anasema ili kudhibiti Tembo kuingia katika makazi ya watu na tayari wameanza mradi wa ushoroba wa Tembo.
Mradi huo una lengo la kusaidia Wanyama pori hususani Tembo kupita kwa usalama zaidi wanapokua wanatoka Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.
Pia wanaimarisha mahusiano bora baina ya wananchi na wanyama pori kwa kuhakikisha wanyamapori hao hawaingii katika makazi na mshamba ya wananchi.
‘’Tunategemea ushoroba utakapokamilika kutakuwa na usalama wa wanyamapori lakini pia usalama wa wananchi kwenye mashamba na maisha yao,’’ anasema Masatu.
Ushoroba huo wa Tembo utakuwa na umbali wa kilometa 12.6 kuunganisha hifadhi hizo mbili huku ukijingewa fensi ya bati ili kuwadhibiti tembo wasiingie katika makazi na mashamba ya watu.
‘’Tunatarajia fensi itakapokamilika yale madhara ambayo Tembo walikuwa wanayasababisha wanapovuka kwenye mashamba yatakua yamepungua kwa sababu watakua wanapita kwenye njia yao lakini pia mashamba ya binadamu yatakua salama kutokana na ule uharibifu wa Tembo,” anasema Masatu.
Aidha wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujilinda na Tembo hasa wanapoingia katika makazi yao ikiwemo kugonga vitu vyenye kutoa sauti kama ngoma, bati au ndoo na kwa kuwa mnyama huyu hapendi kelele hulazimika kuondoka.
Njia nyingine ni matumizi ya tochi yenye mwanga mkali kwa sababu Tembo anapoona mwaga mkali hukereka hivyo huondoka eneo husika.
Akili ya Tembo wa Udzungwa
Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa na Meneja Mradi wa Mahusiano ya Tembo na Binadamu kutoka STEP, Kim Lim kwa waandishi wa habari waliotembelea ofisi hizo mwishoni mwa mwaka 2023 anasema sio rahisi kumdhibiti Tembo wa Udzungwa.
Sababu kuwa ana akili sana jambo ambalo linawafanya kuendelea kubuni mbinu mpya kila wakati za kuwa dhibiti huku waki boresha maisha ya watu wanaoishi karibu na Hifadhi ya Milima ya Udzungwa.
Waandishi hao wa habari walikua katika mafunzo kwa vitendo yaliyoratibiwa na kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa kupitia mradi wa USAID Uhifadhi Maliasili yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kuripoti habari za bioanuai.
Anasema kwa sasa STEP imekuja na teknolojia ya kutengeneza fensi ya bati ambayo tayari imefungwa katika katika vijiji vya Magombera na Kanyenja Wilaya ya Kilombero.
Wanaendelea kubuni aina nyingine ya fensi ili kuhakikisha malengo ya kuzuia Tembo kutoka katika ushoroba yanafikiwa ili kuwafanya wananchi waishi kwa amani na usalama.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, idadi ya tembo imeongezeka kutoka 43,330 mwaka 2014 hadi 60,000 mwaka 2023 na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa nchi ya tatu barani Afrika kwa kuwa na tembo wengi.
Matokeo ya Sensa ya mwaka 2022 ya Wanyamapori katika Mfumo Ikolojia wa Nyerere - Selous - Mikumi - Liparamba yanao nyesha kuwa idadi ya tembo ni 20,006.
Matokeo hayo ikilinganishwa na sensa ya mwaka 2018, idadi ya Tembo imeo ngezeka kwa asilimia 22.
Aidha ongezeko hilo la tembo limekuwa likichangia wanyamapori hao kuingia katika maeneo ya watu na kufanya uharibifu.
Serikali katika utatuzi wa migogoro ya binadamu na Tembo
Hotuba ya Wizara ya Maliasili na utalii ya mwaka 2023/2024 inasema utatuzi wa migogoro baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu, Serikali imeendelea kukabiliana nayo kwa kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Utatuzi wa Migogoro baina ya Wanyamapori na Binadamu wa mwaka 2020-2024.
Utekelezaji wa mkakati huo ni pamoja na kutoa elimu kuhusu namna ya kukabiliana na wanyama hao.
Mkakati mwingine ni kutoa vifaa kwa wananchi vya kupambna au kuwafukuza wanyamapori wakali na waharibifu, kutoa kifuta jasho na machozi kwa wanaoathirika na wanyamapori wakali na waharibifu.
Pia wizara hiyo itaendelea kufanya tafiti kwa kuwafunga mikanda ya mawasiliano viongozi wa makundi ya Tembo ili kubaini mienendo yao, kutumia ndege maalumu kuondoa wanyamapori kwenye makazi na kuongeza vitendea kazi vya kupambana na wanyama hao.
Askari wa doria wataongezwa kwa kutumia askari wanyamapori wa vijiji na kuunda kamati maalumu ya wataalamu ya kumshauri waziri husika.




Comments
Post a Comment