RC PWANI AGUSWA NA MCHANGO WA WAANDISHI WA HABARI MKOANI KWAKE, AJIPANGA KUWEKA MKAKATI WA KUWAINUA KIUCHUMI.





Na Gustafu Haule,Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, amesema anathamini michango ya waandishi wa habari waliopo katika Mkoa wake kwakuwa wanafanyakazi kubwa ya kuchochea maendeleo.

Kunenge,ametoa kauli hiyo leo Mei 23 wakati akifungua mkutano wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari uliofanyika katika ofisi za  Mkoa huo  ukiwajumuisha Waandishi wa habari pamoja na wadau mbalimbali.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza katika ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyofanyika leo Mjini Kibaha yakiandaliwa na Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Pwani (CRPC).

Katika maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Klabu ya Waandishi Wa Habari Mkoa wa Pwani Kunenge amesema ,kazi wanazofanya Waandishi wa habari katika Mkoa wake zinaonekana na zimekuwa zikileta matokeo chanya huku akisema lazima wathaminiwa.

Amesema , kutokana na mchango mkubwa unaotolewa na waandishi hao ,yeye yupo mstari wa mbele kutoa ushirikiano katika kuhakikisha kazi ya Waandishi hao zinafanyika katika mazingira rahisi kama ambavyo Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan alivyoweka mazingira mazuri katika Sekta ya habari.

"Lazima niseme kweli Waandishi wa habari wa Mkoa huu wanafanyakazi vizuri ya kutangaza Mkoa wetu na niwahakikishie mimi ni kiongozi wa ushirikiano na lazima watendaji wangu nao wawe na ushirikiano ,"amesema Kunenge 

Baadhi ya Waandishi wa habari wa Mkoa wa Pwani wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge aliyekaa katikati mara baada ya kufungua maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari yaliyofanyika leo Mjini Kibaha chini Klabu ya Waandishi wa habari wa Mkoa huo na kushoto ni Mwenyekiti wa Klabu hiyo Ally Hengo na Kulia ni Katibu tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta

Akizungumzia masuala ya uchumi kwa Waandishi wa habari Kunenge amesema kuwa kwasasa ataweka mipango mizuri na wezeshi ambayo itawasaidia Waandishi kuwa na uchumi imara huku akimuagiza Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta kukutana kwa haraka na viongozi wa Klabu hiyo ili kuanza utekelezaji wa jambo hilo.

Amesema kuwa, Mkoa wa Pwani ni Mkoa wa viwanda wenye kuzalisha bidhaa mbalimbali lakini bado waandishi hawajafanikiwa kutangaza bidhaa zinazozalishwa ambapo amewataka Waandishi hao kujikita katika kutangaza bidhaa hizo ili Mkoa hupate kufahamika zaidi kutokana na bidhaa hizo.


Kuhusu changamoto  ya mazingira Kunenge amesema Mkoa umepokea maagizo kutoka kwa Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango wa kutoridhishwa na janga la kukata miti na kuchoma mkaa ambapo kwasasa tayari wameweka mkakati wa utekelezaji wa jambo hilo.

Amesema , miongoni mwa mambo ambayo Mkoa umeanza kuyafanyiakazi ni kupiga marufuku bodaboda zinazojulikana kwa jina la busta kubebea mkaa na badala yake zinazotakiwa kutumika ni Toyo ( pikipiki za matairi matatu).

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani  Rashid Mchatta,amewapongeza waandishi wa habari kwa namna wanavyofanyakazi na Serikali ya Mkoa huku akisema kwasasa ni lazima kuweka mikakati mizuri ya kufanyakazi.

 
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta akizungumza wakati wa mkutano wa madhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani kwa Mkoa wa Pwani.


Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi habari Mkoa wa Pwani Ally Hengo,amesema maadhimisho hayo kidunia yalifanyika Mei 03 mwaka huu na kitaifa yalifanyika Mkoani Dodoma lakini kwa Mkoa wa Pwani yalisogezwa mbele kwa ajili ya kupisha shughuli za mwenge.
 
Hengo,pamoja na mambo mengine ametumia nafasi hiyo kumshukuru Mkuu wa Mkoa kwa namna ambavyo anatoa ushirikiano kwa Waandishi wa habari  ikiwa pamoja na kuendelea kukamilisha ahadi yake ya kutoa kiwanja cha ofisi ya Waandishi wa habari aliyoitoa mwaka 2022.

Hata hivyo,katika maadhimisho hayo mada mbalimbali zilitolewa ikiwemo mada ya mazingira iliyotolewa na afisa misitu wa Mkoa wa Pwani Pierre Protas huku kamanda wa zimamoto Mkoa wa Pwani Jenifa Shirima akitoa mada ya kujiepusha na majanga ya moto pamoja na mada ya maadili iliyotolewa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Serikali kutoka Mkoa wa Pwani Zablon Bugingo.

Afisa misitu wa Mkoa wa Pwani Pierre Protas akitoa mada katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyofanyika leo Mjini Kibaha Mkoani Pwani.


Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa Mkoa wa Pwani Jenifa Shirima akitoa mada katika kwa Waandishi wa habari na wadau katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyofanyika leo  Kibaha Mkoani Pwani



Club News Editor - Charles Kusaga

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA