Mkaa mbadala ulivyosaidia kupunguza uharibifu ushoroba wa Nyerere Selous-Udzungwa



Na. Monica Msomba.Kilombero

Alikuwa ni miongoni mwa wanawake waliokuwa wakiamini kuwa kuni na mkaa ndio nishati pekee ya kutumia katika kupikia.

Hata hivyo, alichokua anakiamini hakikuwa sahihi, mpaka alipokuja kugundua kuwa nishati ya kuni na mkaa ina madhara makubwa kiafya.

Huyu ni Arafa Makeleketa, mkazi wa Mang’ula ‘B’ Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro ambaye ameachana na matumizi ya nishati hizo baada ya kupata elimu ya matumizi ya mkaa mbadala usio na madhara kiafya.

Arafa Makeleketa ni mmoja wa waathirika wa matumizi ya mkaa na kuni katika kijiji cha Mang'ula B

“Nimetumia mkaa na kuni kwa zaidi ya miaka 20 nikiwa napika maandazi na chapati vimenifanya  kupata ugonjwa wa kifua nakohoa mfululizo,” anasema Arafa, aliyewahi kuwa mama lishe maarufu Mang’ula B.

Arafa ambaye yeye na wenzake walikuwa wakiingia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa kuokota kuni anasema madhara aliyopata katika mfumo wa upumuaji hatamani tena mkaa na kuni.

“Ninachowashauri mama lishe wanaofanya biashara kama niliyokuwa nayo awali wajikite kutumia mkaa mbadala hauna moshi na hawezi kuathirika kiafya kama ilivyo kwangu lakini pia kwa kufanya hivi wanatunza mazingira na shoroba zilizokaribu yetu,” anasema Arafa.

Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Nyerere na Pori la Akiba la Kilombero ziko katika ushoroba wa Nyerere Selous-Udzungwa ambao umekuwa  sehemu muhimu ya mapitio, makazi na malisho ya wanyamapori wanaotoka na kuingia katika hifadhi hizo.

Shughuli za kibinadamu zimekuwa na athari kwa mazingira ikiwemo kupunguza idadi ya miti na uoto wa asili ambao unahitajika kwa wanyamapori kuishi katika ushoroba huo.

Hata hivyo, hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kukabiliana  na uharibifu huo ikiwemo kuhimiza matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia ikiwemo matumizi ya mkaa mbadala ambao Arafa na wenzake katika kikundi cha Mazingira kilichoanzishwa mwaka 2012 wanautengeneza.

Bibiana Kawaga ni Afisa Mauzo wa kikundi hicho anasema mkaa mbadala wanaotengeneza katika kikundi chao chenye wanachama 15 unatokana na mabaki ya mimea , majani ya miti, mabua ya mahindi, pumba za mpunga, mabaki ya migomba, maganda ya nazi, vifuu vya nazi na takataka zote zinazopatikana katika mazingira yao.

Afisa Mauzo wa kikundi cha watengezaji mkaa mbadala cha Mazingira Kijiji cha Mang'ula B. Bibiana Kawaga akielezea namna wanavyotoa elimu ya utengenezaji nishati hiyo.

Wakati kikundi cha Mazingira kikitengeneza mkaa mbadala kwa ajili ya kuingiza kipato, pia wanatumia fursa hiyo kuelimisha jamii za watu wanaoishi karibu na hifadhi za Taifa za Milima ya Udzungwa na Nyerere kutunza mazingira kwa kuacha kukata miti hovyo.

Anasema elimu yao wanayotoa shuleni na katika mikutano ya vijiji inalenga  kuwabadilisha wananchi kujenga tabia ya kupanda miti, kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kutumia mkaa mbadala.

“Tumekuwa tukienda shule za msingi,  sekondari, vikundi vya akina mama, mikutano ya vijiji tunawaelezea umuhimu wa kutunza mazingira ili wanyama waliopo hifadhini wasikimbie kwani kupitia hifadhi na hii shoroba ya Nyerere selous-Udzungwa watoto wetu wanapata ajira kuingia hifadhini na  watalii,” anasema Bibiana na kuongeza kuwa,

“Elimu hii tunayoitoa kwa makundi mbalimbali inasaidia wananchi kuacha tabia ya kuingia hifadhini,  tunawaeleza kabisa madhara ya uharibifu wa hifadhi zetu ambayo ni pamoja na kukosa watalii na mvua na ajira zitakosekana sambamba na kushuka kwa mapato.”

Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 na Sheria ya Misitu Sura 323 ya mwaka 2002 zinaeleza umuhimu kutunza misitu iliyopo Tanzania na kupiga marufuku ukataji hovyo wa miti katika maeneo muhimu yaliyohifadhiwa.

Kikundi cha Mazingira kilivyoinuka

Baadhi ya wanakikundi  wa kikundi cha Mazingira kilichopo Kijiji cha Mang'ula B. wakitengeneza mkaa mbadala 

Kikundi cha Mazingira kilipata ufadhili kutoka kwa Taasisi ya Associazione Mazingira ambapo wanachama wanaoishi karibu na hifadhi hufundishwa jinsi ya kutengeneza mkaa mbadala  na baada ya hapo wanajigawa katika Vijiji 18 vilivyopo Tarafa ya Mang’ula na kuendelea na kazi ya uhamasishaji na utoaji wa elimu ya utumiaji wa mkaa huo.

Kwa mujibu wa Waziri wa  Nchi Ofisi ya Makumu wa Rais Muungano na  Mazingira Dk Selemani Jafo akizungmza mjini Kisarawe mkoani Pwani hivi karibuni alisema zaidi ya hekta laki 400,000 za misitu zinakatwa nchini kila mwaka kwa matumizi ya kuni na mkaa.

Mkaa mbadala unatengenezwaje?

Mwenyekiti wa kikundi cha Mazingira kilichopo Mang'ula B. Suna Kulolela akizungumza na mwandishi wa makala hii Monica Msomba (hayupo pichani) umuhimu wa utunzaji wa hifadhi.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Mazingira Suna Kulolela anaikumbusha jamii kutodharau uchafu wa aina yoyote ile katika nyumba zao ikiwemo maganda ya ndizi, majani ya miembe, vifuu vya nazi ambavyo vyote kwa ujumla ni rasilimali kwa ajili ya kutengeneza mkaa mbadala  ambao ukitumiwa vizuri unasaidia kutunza shoroba.

‘’Tunapohamasisha akina mama kuna njia  nyepesi wanaweza kutengeneza bila kuwa  na mashine. Anachukua  vifuu anavichoma kutoa hewa ukaa na kuvitwanga  kwenye kinu, unachekecha kupata unga, unachukua unga wa muhogo kama gundi, unachanganya kwa kupikicha na mikono unapata mkaa wako,‘’ anasema Suna.

Uzalishaji wa mkaa mbadala unatumia malighafi ya mabaki ya mimea mbalimbali kama vile majani yanayodondoka kutoka mtini, mabaki ya nazi, maganda ya nazi, pumba za mpunga, maranda ya mbao na mabua ya mahindi.

Mkaa mbadala unaozalishwa na kikundi cha wanawake kata ya Mang'ula B. Wilaya ya Kilombero

Hivi vyote vinachukuliwa na kuchomwa ili kuondoa hewa ya ukaa na kupata malighafi safi kwa ajili ya kuzalisha mkaa mbadala.

Mratibu Msaidizi wa Miradi na Afisa Mazingira wa  shirika la Associazione Mazingira  Isaack  Shonga anasema lengo lao ni kuhakikisha jamii inajengewa uwezo wa  kulinda na kutunza misitu na hifadhi iliyopo karibu na makazi yao.

“Shirika hili linahamasisha  wananchi waunde vikundi  na viweze kutambulika katika ngazi ya Serikali za Mitaa, Wilaya na Taifa na baada ya hapo  tunawawezesha  kupata  mafunzo  na hata  kuwapa  mitaji ili wajiendeleze kiuchumi,” anasema Shonga.

Kwa mujibu wa mratibu huyo, wananchi wanajiendeleza kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwemo ushonaji na ufugaji nyuki.

Pia wamewezesha kikundi hicho kupata mashine inayotumika  kuzalisha mkaa  mbadala yenye thamani ya Sh. 10 milioni ambayo ina uwezo wa kuzalisha kilo 300 za mkaa kwa saa moja.

Serikali yahimiza uhifadhi wa mazingira

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mang’ula “B” Philomena Mosha anasema  Serikali inashirikiana na vikundi hivyo na pia inawaunga mkono kwa kuwasaidia kupata mikopo kutoka  katika ngazi ya halmashauri ili kuendeleza shughuli zao.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mang’ula “B” Philomena Mosha akizungumza na mwandishi wa makala hii Monica Msomba (hayuko pichani) juu ya matumizi ya nishati ya mkaa mbadala.

Anasema  elimu wanayoitoa  ina msaada kwa jamii na hata katika kulinda rasilimali za Taifa ikiwemo  Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa  pamoja na ushoroba  wa Nyerere-Selous –Udzungwa  zinazochangia mapato kutokana  na watalii.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mang’ula B  Habibu Lipongola  anasema mkaa mbadala umekuwa mkombozi kwa wananchi kwa kuwa unauzwa kwa bei nafuu ambayo mwananchi wanaimudu na hivyo kupunguza kasi ya wananchi kuingia katika hifadhi za wanyamapori kukata miti.

Diwani wa kata ya Mang’ula Frola Ndumba, anasema anaendelea kushirikiana na kikundi cha Mazingira na hata kuwasemea katika baraza la madiwani ili wapate msaada katika utekelezaji  majukumu yao.

“Matumizi ya mkaa mbadala  katika Kata yangu umesaidia kwa kiasi kikubwa  kupunguza tabia ya  ukataji miti hovyo katika hifadhi, hivyo  sisi viongozi  tunawahamasisha wanakikundi  kuendelea kutoa elimu ya matumzi ya nishati mbadala kwa jamii lakini nawasihi  wananchi kuendelea  kutunza mazingira na vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo yetu ya hifadhi,” anasema Ndumba.

Kaimu Afisa Tarafa ya Mang’ula Acley Mhenga anasema katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira vikundi hivyo vimekuwa mstari wa mbele  na kwamba  wananchi wamepata elimu ya kutosha kuhusu mazingira na masuala ya uhifadhi na kwasasa hawaingii katika hifadhi kwa ajili ya kufanya shughuli zao za kibinadmu.

Hifadhi ya Milima ya Udzungwa ni moja kati ya hifadhi hiyo zilizopata mradi wa Regrow wa kuendeleza hifadhi za kusini mwa Tanzania ambao unalenga hifadhi za Nyerere, Mikumi, Ruaha na Udzungwa.

Sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya milima ya Udzungwa iliyopo Morogoro Tanzania

Moja kati ya miradi hiyo ni pamoja na kikundi cha Mazingira Group,  mpango ambao unaratibiwa na wadau wa uhifadhi  wa mazingira kutoka katika Shirika  lisilo la kiserikali Associazione Mazingira ambao wanawezesha kikundi cha akina mama wanoazalisha mkaa mbadala.

Hatua zaidi kuwawezesha wananchi katika uhifadhi

Afisa Ushoroba wa Shirika la Uhifadhi wa Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP) Elizabeth Masatu anasema kuwa katika vijiji ambavyo vimepitiwa na shoroba wanawapatia elimu wananchi na kusaini nao mkataba wa uhifadhi  wa shoroba ili wazilinde.Afisa Ushoroba wa Shirika la Uhifadhi wa Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP) Elizabeth Masatu

Pia kila kijijii kinapokea Sh. 10 milioni kwa mwaka ambapo zinaenda katika maendeleo ya jamii kama ujenzi wa zahanati na kukata bima ya afya kwa wazee.

Sambamba na hilo pia Shirika hilo linatoa ajira kwa vijana ambao wanatoka katika vijiji vilivyopitiwa na shoroba , wanafanya ulinzi na kuhakikisha usalama wa shoroba ya Nyerere Selous -Udzugwa.

 




Club News Editor Julieth Ngarabali.

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA