Serikali yapanua likizo ya Uzazi kwa wanaojifungua Njiti
Serikali
imetangaza kupanua kipindi cha likizo ya uzazi kinachotambuliwa kisheria kwa
wanawake katika utumishi wa umma wanaojifungua watoto wanaozaliwa kabla ya muda wake maarufu njiti na kwamba hatua hii imepokelewa
kwa mikono miwili na wadau mbalimbali ambao wamesema ni muhimu katika kuimarisha
afya ya mama na mtoto.
Tangazo la Serikali la kupanua kipindi cha likizo ya uzazi kwa wanawake katika sekta ya umma wanaojifungua watoto njiti limekuja ikiwa ni mda mrefu sasa limekuwa likipigiwa kelele na wadau mbalimbali ikiwemo chama cha wafanyakazi wa Serikali kuu na afya (TUGHE) pamoja na wadau na masuala ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kupitia programu Jumuishi ya PJT-MMMAM ambao unalenga kutatua changamoto za ukuaji na maendeleo ya awali ya watoto wa umri wa miaka 0-8
Akizungumza
kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa sherehe za siku ya Wafanyakazi
mwaka 2024 Mkoani Arusha , Makamu wa Rais Philip Mpango amesema kuanzia sasa
likizo ya wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya umma itaanza mara tu watoto
wanaozaliwa mapema yaani Njiti watakapotoka katika chumba cha uangalizi maalum.
Ameongeza
kuwa wanawake wenye watoto njiti wanapaswa pia kupewa muda wa kunyonyesha kwa
miezi sita ili kuhakikisha watoto wao hao wanapata uangalizi bora zaidi.
"Serikali imewekeza fedha nyingi katika huduma za afya ya mama na mtoto, ikiwa ni pamoja na kuanzisha vyumba zaidi vya uangalizi wa watoto njiti kwa hivyo naagiza kwamba likizo ya uzazi katika hali kama hizo ianze mtoto anapotoka katika chumba cha uangalizi maalum kama itakavyoamuliwa na madaktari." Amesema Dk. Mpango.
Dk. Mpango amebainisha kuwa wafanyakazi wanaojifungua watoto njiti wamepewa ruhusa ya kuondoka kazini saa 07.30 kwa muda wa miezi sita baada ya kumaliza likizo yao ya uzazi ili kuwapa muda wa kutosha wa kunyonyesha.
Amebainisha
kuwa kwa wafanyakazi wa sekta binafsi, Serikali pia itafanyia marekebisho sheria
husika ili nao wanufaike, sheria hiyo ni sheria ya
ajira na mahusiano kazini sura ya 366 na marekebisho yake ya mwaka 2019 .
Uamuzi
huo umepokelewa kwa mikono miwili na wadau wa masuala ya mama na mtoto nchini, wakisema
umechelewa kuchukuliwa.
Kwa
mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mtoto anachukuliwa kuwa ni njiti ikiwa tu
amezaliwa kabla ya wiki 37 za ujauzito.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Mtandao wa Programu za Jinsia Tanzania (TGNP) Lilian Liundi amesema
uamuzi huo utasaidia kina mama kufanya malezi ya watoto hao ambao kimsingi ni wenye
mahitaji maalum.
Ameongeza kuwa, hata hivyo, Serikali iongeze bajeti ya Wizara ya Afya ili kukidhi mahitaji ya vifaa vya kisasa vya kutunza watoto Njiti.
Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu Bungeni Dododom, kuhusu makisio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara hiyo kwa mwaka 2023/2024 bajeti yake kwa kipindi hicho ni sh. Trilioni 1.235 ikiwa na ongezeko la sh. Bilioni 121 ukilinganisha na bajeti ya 2022/2023 sawa na ongezeko la asilimia 10.9 kuongezeka kwa bajeti hii kulilenga pia kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto nchini.
Nini anachokisema mmoja wa wanawake waliowahi kujifugua mtoto Njiti;
Naye mmoja wa wanawake waliowahi kujifugua mtoto njiti ambaye pia ni mtumishi katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Pwani yaTumbi Felister Assenga amesema hatua hiyo isiishe katika hatua ya tangazo na kushaui kuwa mabadiliko hayo yanahitaji kupelekwa Bungeni ili yawe sehemu ya sheria ya kazi .
Picha ni mmoja wa wanawake waliowahi kujifugua mtoto njiti ambaye pia ni mtumishi katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Pwani yaTumbi Felister Assenga ."Ni muhimu iingizwe katika sheria ya kazi na kurasmishwa ili hata waajiri waweze kuichukua na kuitekeleza katika ofisi zao na pia tunaishukuru Serikali kwa hatua hii nzuri ya mwanzo’’amesema
Mapema
mwezi machi Mwaka huu 2024 ,Wafanya kazi
wanawake waliojifungua watoto kabla ya muda wake maarufu
watoto njiti waljitokeza hadharani na kusema siku 84 zilizowekwa
kisheria kama likizo ya uzazi hazitoshelezi kulea watoto
njiti na kwamba kuna umuhimu wa Serikali kuangalia upya uwezekano
wa kuboresha sheria ya ajira na mahusiano kazini sura ya 366 na
marekebisho yake ya mwaka 2019 .
Katika sheria hiyo kifungu kidogo cha 33
kifungu kidogo cha 6 (a ) kinasema mtumishi mwanamke aliyejifungua mtoto mmoja
atapata likizo ya siku 84 huku kifungu cha 33 kifungu kidogo cha 6 ( b )
inaeleza kuwa mtumishi mwanamke aliyejifungua watoto zaidi ya mmoja atapata
likizo ya siku 100 ambapo sheria hiyo imeishia hapo haijasema kama atajifungua
watoto njiti atapata muda wa ziada na hivyo shida imeanzia hapo
Chanzo cha kuzaliwa watoto njiti .
Kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani (WHO) maradhi katika njia ya mkojo (UTI ) wanawake wenye historia ya kupatwa na uchungu mapemawapo katika hatari ya kujifungua njiti ukilinganisha na wasio na historia hiyo, kuwa na mimba yenye zaidi ya mtoto mmoja ,wanawake wenye matatizo katika maumbile ya mfumo wa uzazi nao wapo katika hatari zaidi, maradhi yanayosabishwa na ngono zembe ikiwemo Ukimwi,kisonono ,kaswende na trikomonasi.Ingine ni shinikizo la damu ,kutokwa na damu
katika sehemu za uzazi ,mama kuwa na uzito mdogo au mkubwa kupitiliza
wakati wa ujauzito,wanawake walio na umri unaozidi miaka 35 wapo katika hatari
pia, msongo wa mawazo na matatizo ya kifamilia
Hali ikoje
Kwa mujibu shirika la Umoja wa Mataifa la afya
Duniani WHO na shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF makadirio
yanaonyesha kwamba mwaka 2020 takribani watoto milioni 13.4 walizaliwa kabla ya
muda yaani njiti huku karibu milioni 1 kati yao wakifariki kutokana na matatizo
yanayotokana na hali hiyo ya kuzaliwa kabla ya wakati .
Aidha Afisa elimu kazi wa chama cha
wafanyakazi wa Serikali kuu na afya (TUGHE) makao makuu Nsubisi
Mwasandende amesema sheria ya sasa ya ajira na mahusiano
kazini imekuwa ikitoa siku 84 kwa wanawake wanaojifungua mtoto mmoja na siku
100 kwa wanaojifungua zaidi ya mtoto mmoja .
Lakini sheria hiyo haisemi chochote kuhusu wale wanawake wanaojifungua watoto njiti na ndio maana walijitokeza hadharani kuikumbusha Serikali ifanyie kazi changamoto hiyo.

"Sheria ya sasa ya ajira na mahusiano kazini imekuwa ikitoa siku 84 kwa wanawake wanaojifungua mtoto mmoja na pia siku 100 kwa wanaojifungua zaidi ya mtoto mmoja wala haisemi chochote kuhusu wanawake wanaojifungua watoto njiti ndio maana tumeona ni vyema kuikumbusha Serikali ili ifanye mabadiliko ili kuwaongezea muda wanawake hao"amesema Mwasandende
Matatizo kadhaa yanayoweza kumkumba mtoto
njiti
Matatizo yanayowakumba zaidi watoto njiti ni pamoja na kupumua kwa sababu wakati huu mapafu yanakua hayajakomaa, shida ingine mi kwenye ulaji au unywaji kutokana na mfumo change wa chakula
Aidha Programu Jumuishi ya Taifa ya
malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT-MMMAM ) tayari imeanza kutekelezwa
nchini na unalenga kutatua changamoto za
ukuaji na maendeleo ya awali ya watoto wenye umri wa miaka 0-8 kupitia afua
tano ikiwemo lishe ya kutosha kuanzia ujauzito, afya bora kwa mtoto na
mama/mlezi ,malezi yenye muitikio ,fursa za ujifunzaji wa awali ,ulinzi na
usalama kwa watoto.
Comments
Post a Comment