Elimu ya tembo inavyoboresha maisha ya wanafunzi .





Beatrice Lihaku ni mwalimu wa somo la mahusiano kati ya Tembo na wanafunzi shuleni

Na Julieth Ngarabali.

 

Hana wasiwasi tena wa kutimiza ndoto yake ya kuelimika na kuwa kiongozi mwenye mafanikio katika jamii. 


Uhakika huu umetokana na kikwazo cha kwenda shule kusoma kuondolewa. 


Huyu ni Joseph Sefu, mwanafunzi Shule ya Msingi Mlimani iliyopo Kata ya MangĂșla ‘B’ Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro. 

Joseph Sefu, mwanafunzi Shule ya Msingi Mlimani akieleza namna yeye na familia yake walivyonufaika na somo laTembo shuleni.

Wanafunzi wa shule tatu za msingi na awali za Mlimani, Kanyenja na Magombera akiwemo Joseph walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya tembo kuvamia makazi ya watu katika Kata ya Mang’ula ‘B’.hivyo muda mwingi wakawa ni wenye hofu tu.


Tembo hawa walikuwa wakifanya uharibifu wa makazi, mashamba, kujeruhi na hata kuondoa uhai wa watu matukio yaliyochangia hofu na wasiwasi mkubwa kwa watoto wakiwemo wale wa chini ya miaka nane.


Hali hii iliwaweka wanafunzi wa shule hizo za msingi na awali ambazo zipo mpakani mwa milima ya Udzungwa katika hofu na kuhatarisha usalama wao waendapo na wawapo shuleni kwa sababu tembo walikuwa wakizaga mitaani.


Tembo hawa ni wale wanaopatikana katika ushoroba wa wanyamapori wa Nyerere Selous-Udzungwa unaounganisha Hifadhi za Taifa za Milima ya Udzungwa, Nyerere na Pori la Akiba la Kilombero. 


Kutokana na tembo kupitia katika mapitio yao ya asili ili kutafuta chakula, kuzaliana na kuishi huibua migogoro na binadamu kwa sababu katika njia hizo kuna shughuli za binadamu. 


Mmoja wa wazazi katika Kijiji cha Kanyenja Kata ya MangĂșla ‘B’ Ezra Igole anasema katika miaka ya 2020 /2021, wanafunzi katika kata hiyo walikuwa hawataki kwenda shule kwa hofu ya kuvamiwa au kujerubiwa na Tembo njiani.

 

“Tembo wanaingia kijijini kuanzia saa 12 jioni na saa moja usiku watoto bado hawajalala wanapowaona nje ya nyumba zao hupata hofu ,wasiwasi na woga sana asubuhi ukimwambia aende shule anakataa kabisa anahofia atakutana naye njiani,” anasema Igole na kuongeza kuwa,

 

“Mara nyingi  niliwaacha wakae nyumbani wasubiri Tembo waondoke ndio waende shuleni na kwa wale wa awali  walisubiri wakue walau hadi miaka sita au saba ndio niwaandikishe shule lakini kwa sasa ni tofauti baada ya elimu ya Tembo watoto hawana tena uoga wanajua kujihami nao.”


Ikumbukwe pia Mkoani Pwani changamoto ya aina hii inawakabili wananchi katika Wilaya ya Bagamoyo. Chalinze na Rufiji ambapo zinapakana na hifadhi ya Saadan na Selous.


Elimu ya Tembo yabadilisha mambo

Mwanafunzi Joseph anasema shuleni wanafundishwa somo la tembo mara mbili kwa wiki na katika mafunzo hayo wamekuwa wakifundishwa tabia, mbinu za kujihami na vifaa vya kutumia katika kukabiliana na Tembo. 


Pia wanafundishwa kuwa tembo siyo adui bali ni rafiki ambaye wanatakiwa kujifunza jinsi ya kuishi naye. 

 

Mbinu mojawapo ya kujihami dhidi ya Tembo wana wanapokua wanaenda shuleni ni kuangalia upepo unaelekea upande gani kwa sababu mnyama huyu anatumia harufu hasa wakati wa mchana ambapo haoni vizuri.

 

“Kwa maana ukikaa upande upepo unatoka kuelekea Tembo alipo inakua hatari sana kwa sababu yeye ananusa na akishanusa akafata harufu inapotokea hivyo anaweza kukudhuru,” anasema Joseph.

 

Mwanafuzi mwingine wa Mlimani, Yusta Kasangai amefundishwa chakula anachopendelea Tembo ni magome ya miti na matunda.


Yusta, mwanafunzi wa darasa la tatu anasema wanashauriwa kutokuhifadhi ndani ya nyumba matunda yenye harufu ikiwemo ndizi na mafenesi kwa sababu Tembo akifika lazima atataka kula na hivyo anaweza kufanya uharibifu wa nyumba.

Mwanafunzi Janeth Jafari (kulia) wa darasa la tatu shule ya Msingi na awali Kanyenja huko Mang'ula Kilombero.


Mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Kanyenja  Janeth Jafari anataja tabia ingie ya Tembo aliyoifahamu baada ya kupata elimu kuwa Tembo akizaa mtoto wa kiume akifikia umri wa miaka 14 huachwa na mzazi wake anakwenda kutafuta makazi sehemu nyingine ili asije akajamiiana na dada zake.

 

“Pia ana tabia ya kutembea na Tembo jike mkubwa anayejua njia za asili kwa maana ya za zamani na ndio maana unakuta wanaingia kijiji licha ya kuwepo Ushoroba wa Nyerere-Selous Udzungwa,’’ anaongeza mtoto mwingine Ichaja Richard, mwanafuzi wa Kanyenja shule ya Msingi.

 

Amebainisha wao kama wanafunzi wamekuwa wanawafundisha na wadogo zao  na jamii kwa ujumla elimu hiyo wanayoipata shuleni na zaidi juu ya namna ya kuwa tayari kukabiliana na Tembo pale inapotokea wamekutana naye na tayari wengi wao sasa hawana hofu tena na mnyama huyo.

 

Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inaeleza kuwa jamii na wazazi na watu wote wanaohusika na malezi wanatakiwa kuwalinda watoto na kila hatari inayoweza kuwakabili ili wakue katika ustawi mzuri na kutimiza ndoto zao. 


Elimu ya tembo ina manufaa? 


Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kanyenja, Alfred Michael anasema kwa miaka mitatu iliyopita migogoro ya Tembo na binadamu katika kata hiyo ilikuwa ya mara ya mara iliyosababisha hofu na wasiwasi miongoni mwa wanafunzi, walimu na hata wazazi kushindwa kuwaandikisha shuleni.

Mwalimu Michael pichani, anasema elimu ya Tembo imesaidia ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi na hata ufaulu ni wa kuridhisha. 

   

Takwimu za elimu za Ofisi ya Mratibu Elimu Kata ya Mang’ula ‘B’ zinaonyesha kuwa kuna ongezeko la uandikishaji wa watoto madarasa ya awali tangu kuanzishwa kwa elimu ya mahusiano kati ya mnyama Tembo na watoto mashuleni katika kata hiyo.

 

Mwaka 2021 uandikishwaji darasa la awali ulikuwa watoto 135 kati yao wasichana ni 59. Uandikishaji uliongezeka hadi wanafunzi 139 mwaka 2022. 

 

‘’ Mwaka huu 2024 tumepokea wanafunzi zaidi ya 140  na tukawaanzisha madarasa ya awali na wengine darasa la kwanza  kutokana na umri wao kuwa umefikia miaka sita ‘amesema Njiku.  

 

''Pia elimu hii sisi kama walimu imetuongezea hata ufaulu katika madaraja maana katika miaka miwili iliyopita mfano kwa Shule ya Msingi Kanyenja  tumepanda kutoKa wastani wa daraja C mwaka 2021 na kuwa daraja la B mwaka 2023,” anasema Mwalimu Michael.


Mratibu Elimu Kata ya MangĂșla ‘B’ Orestes Njiku aanasema elimu ya Tembo imeanza  kutolewa mwaka 2021 kwa shule za msingi Kanyenja ,Mlimani na jirani zao Magombera na kwamba wanatarajia elimu hiyo kusambaa zaidi kwenye shule zingine 


Amebainisha wanafunzi nao huenda kuieneza elimu hiyo kwa wadogo zao nyumbani pamoja na wazazi hivyo karibu kila mkazi anakua na uelewa huo.

 

Elimu ya Tembo shuleni.

Mwalimu wa somo la mahusiano kati ya Tembo na wanafunzi shuleni kutoka Shirika la Programu ya Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP)Beatrice Lihaku akiwa darasani


Elimu ya tembo shuleni inaratibiwa na Shirika la Programu ya Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP) ambalo limekuwa likifanya shughuli kuboresha ushoroba wa Nyerere Selous-Udzungwa ikiwemo kutoa elimu ya uhifadhi na kubuni mbinu mbadala dhidi ya migogoro ya binadamu na wanyamapori. 


Beatrice Lihaku ni mwalimu wa somo la mahusiano kati ya Tembo na wanafunzi shuleni kutoka STEP anasema wanafunzi wanafundishwa kuhusu biolojia ya Tembo, tabia zao, na umuhimu wao katika mfumo ikolojia na  jinsi ya kuishi nao na njia za kuepuka migogoro.

 

“Kabla ya somo hili la mahusiano ya Tembo na Binadamu kutolewa wengi wa wanafunzi walikua na wasiwasi lakini baada ya kupata elimu watoto wamejua kujihami mfano wakiwa wanaenda shule wakikutana na Tembo wanapaswa kwanza kusimama wasubiri wapite.


Pia wanangalia upepo unapoelekea kama ni upande alipo Tembo wao hupaswa kubadili uelekeo ili asinuse harufu,” anasema Lihaku.

 

Licha kutoa elimu ya tembo,STEP inashirikiana na Serikali kuanzisha Ushoroba wa Tembo, kufunga fensi ya mizinga ya nyuki na mabati kuwazuia wanyama hao kutoka hifadhini kwenda katika makazi ya watu. 


Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mlimani, Uyanjo Beda anashauri elimu ya tembo ifundishwe katika shule zote za Ifakara na mikoa mingine iliyopo karibu na hifadhi. 

 

“Hapa kwetu Mang’ula hili somo la mahusiano kati ya tembo na wanafunzi limekua mfano bora wa jinsi elimu inaweza kutumika kuboresha mahusiano kati ya binadamu na wanyama pori na nashauri mpango huu unaweza kuwa mfano kwa jamii zingine zinazokabiliwa na migogoro ya wanyama na binadamu,” anashauri Beda.

 

Elimu ya tembo ni ya jamii yote.

Kaimu Ofisa Mtendaji Kata Mang’ula ‘B’ Mohamed Mohamed anasema elimu ya tembo imeleta mabadiliko makubwa katika mtazamo wa jamii kuhusu mnyama huyo ambapo sasa watu wanaona ni kama sehemu muhimu ya mazingira yao, na wanajitaidi kuwalinda

 

“Na kwa watoto wanavutiwa na kujifunza kuhusu tembo, na wanatamani kuwa sehemu ya juhudi za uhifadhi,” anasema Mohamed alipokuwa akizungumza hivi karibuni na mwandishi wa makala haya.


Aidha Mkoani Pwani kupitia kwa Afisa Elimu Sara Mlaki akizungumza umuhimu wa kuanza kwa somo la Tembo shuleni , ameahidi kutumia ubunifu wa wenzao hao kwenye shule zake za msingi na awali ilizopo jirani na maeneo ya hifadhi za Saadan na Selous .


Hivyo Elimu ya Tembo ni mfano mzuri wa jinsi elimu ya ubunifu inaweza kuboresha maisha ya watu na jamii kwa ujumla kwenye maeneo yote yalipo ndani au jirani na hifadhi za wanyama,

 



 

 

 















Club News Editor

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA