KUUZWA KWA GESI BEI YA RUZUKU KUPUNGUZA MATUMIZI YA MKAA NA KUNI.
Na Yohana Msafiri, Kibaha.
Wakati wananchi wengi wanaendelea kupikia mkaa na kuni huku wakikwepa matumizi ya gesi kwa kushindwa gharama, wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kikongo Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani wamesema serikali inapaswa kuweka utaratibu utakaowezesha makampuni yanayohusika na nishati hiyo kuwauzia wananchi kwa bei ya ruzuku.
Wametoa kauli hiyo machi 27,2024 wakati wa maadhimisho ya upandaji miti yaliyofanyika shule ya Sekondari Kikongo kwa ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.
"Miti inateketea, jangwa linaenea, hali ya hewa inazidi kuchafuka, chanzo ni ukataji wa miti unaofanywa na watu ili kutengeneza mkaa na hilo halikwepeki kwa sasa kwakuwa hata hizo bei za gesi ni kubwa ndio maana wananchi wengi wanakimbilia mkaa na kuni kupikia"amesema Khadija Selemani mwanafunzi wa shule hiyo ya Sekondari Kikongo.
Na kuongeza“Tumekuwa tukiona ugawaji wa mitungi bure kwa baadhi ya wananchi mama lishe na baba lishe lakini hilo pekee haliwezi kusadia wengi wakapata kwa wingi kikubwa hapa kinachotakiwa bidhaa hiyo hasa mitungi iuzwe kwa bei ya ruzuku na Serikali iiingie mkataba na hizo kampuni zinazouza bidhaa hiyo”.
Amesema kuwa utaratibu huo utapunguza matumizi ya mkaa na kuni kwa jamii ya madaraja yote hata wale wenye vipato vya chini kwani watamudu gharama ya kununua gesi tofauti na ilivyo sasa ambapo nishati ya gesi imeendelea kutumiwa na wenye uwezo pekee ingawa wauzaji wameenea maeneo mengi ya nchi.
Mwanafunzi wa kidato cha tatu kwenye shule hiyo Masudi Mabura amesema kuwa kuna umuhimu wa Serikali kwenda mbali zaidi kwa kuwa mdhamini wa wananchi wanaohitaji kununua mitungi ya gesi lakini hawana uwezo wa mara moja ili wawe wanakopeshwa kwa bei ya ruzuku na kurejesha kidogokidogo
“Mitungi ya gesi inauzwa bei kubwa wengi wanashindwa kununua na hata kama kuna baadhi ya makampuni yanaweza kukopesha kwa sasa lakini gharama hizo kwa wenye vipato vya chini hawawezi kumudu na kukimbilia kwenye mkaa hivyo hili ni vema likaangaliwa na serikali”amesema
Kwa upande wake mhifadhi kutoka wakala wa huduma za misitu (TFS) Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani Theodory Kavishe amesema kuwa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwa na ukataji wa miti Halmashauri hiyo inatarajia kupandwa miche 210,000 kwa kipindi cha mwaka huu.
“Kati ya idadi hiyo miche 150,000 kutoka kwenye vitalu 8 vya Halmashauri na miche 60,000 kutoka wakala wa huduma za misitu Wilaya pamoja na mkakati huo pia tunaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya kuepuka matumizi ya mkaa na kujikita kwenye kutumia niashati mbadala katika mapishi”amesema
Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo katibu Tawala Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Moses Magogwa amesema serikali imeendelea kuogeza jitihada za kuratibu mipango ya upandaji miti kwenye maeneo mbalimbali lengo ni kurejesha uoto ambao umekuwa ukipotea kutokana na shughuli za kibinadamu
Amesema kuwa wakati taasisi mbalimbali zikiendelea kuitikia wito huo kuna umuhimu wa kuweka mipango na malengo ya kupanda miti hiyo ili kuwe na tija kwa jamii na taifa kwa ujumla hasa katika kuwapa matokeo chanya.
Kauli za serikali kuhusu kudhibiti matumzi ya mkaa na kuni zimekuwa zikitolewa mara kwa mara na viongozi mbalimbali akiwemo waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Comments
Post a Comment