KIBAHA HURU YACHANGIA MADAWATI YA MILIONI 3 HALMASHAURI YA MJI.




Na Gustafu Haule, Pwani.

KUNDI la mtandao wa kijamii la Whatsapp linalofahamika kwa jina la "Kibaha Huru" limekabidhi madawati 30 yenye thamani ya shilingi milioni tatu (3,000,000) kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mussa Ndomba ikiwa ni kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

 
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika leo katika ofisi za Halmashauri ya Mji wa Kibaha tukio ambalo limeshuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkurugenzi wa  Halmashauri hiyo Dkt.Rogers Shemwelekwa,baadhi ya madiwani na hata wanakikundi wa Kibaha Huru.

Kiongozi wa Kibaha Huru Sudi  Mohamed akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi madawati 30 kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Musa Ndomba katika hafla iliyofanyika April 19, 2024.

 Aidha,katika hafla hiyo Ndomba amewashukuru wadau hao huku akiomba wengine kuiga mfano wa kutumia vizuri makundi ya mitandao ya Kijamii kuchangia shughuli za maendeleo.

Viongozi wa Kibaha Huru akiwepo mchungaji Pascal Mnemwa kushoto ,Sudi Mohamed na Hamis Wayne Kulia wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukabidhi madawati 30 kwa mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Musa Ndomba hafla iliyofanyika  April 19, 2024.


Ndomba ,amesema kuwa kama makundi yote ya kijamii yatakuwa yanafanya shughuli za kuchangia katika maendeleo ni wazi kuwa Kibaha itapiga hatua hasa katika kupunguza changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.

 
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo mwenyekiti wa kundi hilo Mchungaji Paschal Mnemwa ameitaka jamii kutumia vizuri makundi ya Whatsapp kuchangia masuala ya maendeleo badala ya kusubiri kufanywa na Serikali pamoja na wafadhili pekee.

 
Mnemwa,amesema kwasasa wameona waanze katika kusaidia  sekta ya elimu kwa kumfuta mtoto vumbi na hivyo kuchangia madawati 30 ili wasikae chini jambo ambalo litasaidia kuongeza juhudi katika masomo yao na hivyo kuweza kufaulu vizuri.

 “Tunatakiwa kutumia vizuri mitandao ya kijamii kwa kuchangia maendeleo, sisi tumeanza na madawati tuliona wanafunzi katika baadhi ya shule wanakaa chini kwenye vumbi jambo ambalo linapunguza kasi ya wanafunzi kupenda kusoma,” amesema Mnemwa.

Msemaji wa kundi hilo Hamis Wayne, ameshukuru wanakikundi kwa kufanikisha ununuzi wa madawati hayo ambayo yanakwenda kuwasaidia wanafunzi kuondokana na adha ya kukaa chini.

Msemaji wa Kibaha Huru Hamis Wayne akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi madawati 30 kwa mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Musa Ndomba leo April 19, 2024.


Wayne,amewashukuru wadau waliochangia fedha za kununua madawati hayo kuwa  ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Pwani Mussa Mansour, Rugemalira Rutatina, mke wa Mbunge wa  Jimbo la Mkuranga Mariam Ulega na Mbunge wa viti Maalum Subira Mgallu.

Kwa upande wake Ahmad Kibwerere mmoja wa viongozi wa kundi hilo amesema wakati wanaanzisha kundi hilo kulikuwa na mahitaji mengi lakini waliamua kuanza kwa kujitolea kuchangisha fedha kwa ajili ya kununua madawati kunusuru wanafunzi kukaa chini na kwamba wataendelea kuchangia katika sekta mbalimbali kukabiliana na vikwazo vilivyopo.

Awali Afisa elimu taaluma Adinani Livamba, ameshukuru kundi hilo kwa kuigusa sekta ya elimu huku akisema kwa takwimu za hivi karibuni kulikuwa na uhaba wa madawati 3000 lakini pia zaidi ya madawati 1300 yamefanyiwa ukarabati kupunguza uhaba uliopo.

Hatahivyo, Livamba ,amesema Halmashauri hiyo inakabiliwa na vikwazo vingi katika sekta ya elimu na kwamba mbali ya madawati pia wapo wanafunzi wanatembea umbali mrefu kufuata huduma za shule jambo ambalo utatuzi wake umeanza kufanyiwa kazi kwa kujenga shule shikizi.

Club News Editor - Charles Kusaga







Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA