UMEME WAKUTOSHA UNAKUJA WAWEKEZAJI TULIENI, ASEMA RC KUNENGE
Na Gustafu Haule,Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge,amefungua Baraza la Biashara la Mkoa huku akiwatoa wasiwasi wawekezaji kuhusu suala la umeme kwakusema changamoto hiyo inakwenda kuisha kwakuwa Serikali imeweka mipango mizuri.
Kunenge, amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanyakazi kubwa ya kutengeneza miundombinu ya umeme ikiwemo ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere lililopo Wilayani Rufiji ambalo tayari mpaka sasa limeanza kufua umeme Kwa kuwasha mambo mmoja unaozalisha megawati zaidi ya 200.
Kunenge,amesema hayo wakati akifungua baraza hilo leo Machi 06 lililofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa uliopo Mjini Kibaha kikao ambacho kimehudhuriwa na wawekezaji mbalimbali wa viwanda, viongozi wa chemba ya biashara Mkoa, Taasisi wezeshi za Serikali,Watendaji ofisi ya Biashara Mkoa pamoja wawakilishi kutoka Baraza la Taifa la biashara.
Amesema kuwa,Mkoa wa Pwani unahitaji kuwa na wawekezaji wengi ndio maana wamejipanga vizuri katika kila idara na kwamba hakuna mwekezaji ambaye atashindwa kuwekeza kwa changamoto ya kufelishwa na wakuu wa idara au taasisi wezeshi ikiwemo TRA,Osha,Tanesco,Tarura, Tanroads na Dawasa
Kibaha
Amesema,juhudi za uwekezaji zinazofanyika Mkoa wa Pwani zinatokana na nguvu kubwa ya Rais Samia ambaye ndiye aliyetengeneza mazingira mazuri na wezeshi kwa wawekezaji hivyo lazima yafanyike mazuri ambayo Rais anayataka.
Kunenge,amesema kuwa Rais Samia anatambua changamoto ya umeme inayowakabili wawekezaji ndio maana ameelekeza nguvu nyingi katika kuhakikisha umeme unapatikana ili kusaidia katika kuongeza uwezo wa uzalishaji na kwamba wawekezaji wasiwe na hofu juu ya umeme.
"Suala umeme tunaona namna ambavyo Rais wetu anavyolipambania kwahiyo tuwaombe wawekezaji mtuvumilie kidogo kwani muda si mrefu mtapata umeme wa uhakika na hivyo kuongeza uzalishaji,"amesema Kunenge
Kunenge, amesema kuwa Mkoa wa Pwani unajumla ya viwanda 1,533 lakini viwanda 33 vimepatikana kipindi cha Rais Samia tangu aingie madarakani na viwanda 7 vimetoka kuwa viwanda vya kati kuwa viwanda vikubwa na kwamba vingine vinaanzishwa.
Kuhusu migogoro ya ardhi Kunenge amesema kuwa, migogoro ipo lakini tayari kuna hatua zimechukuliwa kwani wapo watu ambao wamechukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kupelekea mahakamani huku akisema hatokubali kuona utapeli wa ardhi unafanyika ndani ya Mkoa wake.
Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Biashara la Taifa Dkt.Godwin Wanga ,amesema kuwa Mkoa wa Pwani unafanya vizuri katika masuala ya uwekezaji na Biashara huku akitaka kuongeza juhudi ili wafanye vizuri zaidi
Wanga,amesema,mwaka huu kuna tuzo Kwa ajili ya mkoa utakaofanya vizuri katika masuala ya uwekezaji na biashara huku akisema hana mashaka na Mkoa wa Pwani kwakuwa vigezo vyote muhimu wanavitimiza.
Katibu wa Baraza la Biashara Taifa Dkt.Godwin Wanga akitoa somo katika kikao cha Baraza la Biashara la Mkoa wa Pwani kilichofanyika Machi 06,2024 Mjini Kibaha
Wanga,ametaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na hupatikanaji wa ardhi ,hupatikanaji wa taarifa na uwazi wa kushughulikia masuala biashara,kuondoa sera kandamizi katika biashara na uwekezaji,kazi na mafunzo,huduma za kusaidia biashara, kipaumbele katika uwajibikaji na vigezo vingine
Hatahivyo,afisa mahusiano wa kampuni ya MMI Abubakar Mlawa,ameipongeza juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na hasa katika kushughulikia changamoto mbali huku akiomba utaratibu wa ukaguzi kwa wafanyakazi viwandani huwe shirikishi baina ya taasisi moja na nyingine huku akitolea mfano wa OSHA na TMDA
Comments
Post a Comment