RC PWANI AHAMASISHA KUPELEKA WATOTO KUPATA CHANJO YA SURUA NA RUBELLA.
Na Gustafu Haule,Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,amesema kuwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano 174,298 wamelengwa kufikiwa kwa ajili ya kupata chanjo ya Surua - Rubella inayotolewa katika maeneo mbalimbali.
Kunenge, amesema kuwa kampeni ya chanjo hiyo tayari imeanza Februari 15 mwaka huu na itamalizika Februari 18 na kwamba kwa Mkoa wa Pwani chanjo hiyo inapatikana katika ngazi ya vituo vya huduma ya afya,ngazi ya kaya kupitia huduma ya mKoba pamoja na maeneo mengine yaliyoainiashwa.
Kunenge,ametoa kauli hiyo Februari 16 mwaka huu wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalum wa kuhamasisha kampeni ya masuala ya chanjo ya Surua na Rubella uliofanyika ofisini kwake .
Katika mkutano huo, Kunenge amewaomba wananchi hususani wenye watoto chini ya umri wa miaka mitano kuhakikisha wanawafikisha watoto wao katika vituo mbalimbali vya kutolea chanjo ili waweze kupata huduma hiyo.
Kunenge,amesema magonjwa ya Surua na Rubella husababishwa na virusi vinavyoenea kwa haraka kwa njia ya hewa hususani pale mgonjwa anapokohoa au kupiga chafya na huathiri watu wa rika zote lakini watoto wenye umri chini ya miaka mitano huathirika zaidi.
"Nawaelekeza Wananchi kuzingatia ushauri wa wataalamu wetu wa afya kwa kuimarisha hali ya usafi na vifaa vya kunawa mikono katika maeneo yetu,kuvaa barakoa na kutoa taarifa na kufika katika vituo vyetu vya huduma za afya kwa wakati",amesema Kunenge
Kunenge,katika hatua nyingine amewaelekeza viongozi waliopo katika maeneo mbalimbali kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa kampeni kwenye maeneo yao ikiwa pamoja na kuhakikisha watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano wanafikiwa.
Aidha,Kunenge ametumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi wa dini na taasisi mbalimbali kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha zoezi hilo katika maeneo yao ili kuweza kufikia malengo ya Serikali ya kuwanusuru watoto dhidi ya magonjwa hayo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Dr Benedicto Ngaiza, amesema dalili za magonjwa hayo ni homa,mafua,na kikohozi ,macho kuwa mekundu na kutoka machozi,kutoka vipele vidogovidogo vinavyoanzia katika paji la uso,nyuma ya masikio na kusambaa usoni na mwili mzima.
Dr .Ngaiza amesema magonjwa hayo madhara yake ni makubwa Kwa binadamu ikiwemo masikio kutoka usahau ambao unaweza kusababisha kutosikia ,vidonda vya macho vinavyopelekea upofu,Nimonia,utapiamulo na kwamba mgonjwa hasipopata tiba sahihi anaweza kupata ulemavu na hata kupoteza maisha.
"Magonjwa haya yanazuilika kwa chanjo,Mtoto hupata dozi mbili za chanjo ya kumkinga na Surua na Rubella ambazo hutolewa anapotimiza umri wa miezi 9 na marudio ni pale anapotimiza miezi 18",amesema Dr.Ngaiza
Mratibu wa mpango wa Taifa wa chanjo kutoka Wizara afya Geogina Ngaiza,amesema kuwa chanjo hiyo inatolewa hapa nchini muda mrefu na ipo salama na wala haina madhara yoyote na kwamba inatolewa bure .
Hata hivyo,Ngaiza,ameitaka jamii kuacha hofu kwani Serikali inaendesha zoezi la utoaji chanjo kwa ajili ya kuwapa kinga watoto ili wasishambuliwe na magonjwa hayo .
.
Comments
Post a Comment