MAGUMU ALIYOPITIA MSICHANA KINARA TUMBI SEKONDARI

  •  Magumu ya kwenye familia yalimpeleka kusikojulikana lakini shuleni anaonekana


Happness Fredy mmoja wa wasichana 34 waliofaulu mtihani wa kidato cha nne 2023 shule ya Sekondari Tumbi .


Na Gustaphu Haule

FEBRUARI 3 ,2024 nimekutana na msichana Happness Fredy ambaye ndiye kinara wa ufaulu wa  matokeo ya mtihani wa kidato cha nne katika shule ya Sekondari Tumbi .

Happness katika matokeo ya mtihani huo amefanikiwa kupata ufaulu wa daraja la kwanza pointi saba matokeo ambayo yameifanya shule ya Sekondari Tumbi kushika nafasi ya pili kimkoa.

Katika mazungumzo yetu ya awali Happness ameanza kwa kusema,"Shule za Kata zimekuja kuwakomboa wanafunzi wanaotoka katika familia duni na kwamba wanaobeza shule hizo ni wazi kuwa hawana wanalolijua," 

Happness ambaye ni mtoto wa pili wa mzee Fredy Godfrey anasema bila kuwepo kwa shule za Kata uenda leo hii angekuwa tayari ameshaolewa na kuitwa mama.

Happness (18)mkazi wa Mtaa wa  Tanita, Kata ya Kibaha Halmashauri ya Mji Kibaha alichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza  Shule ya Sekondari Tumbi mwaka 2020 akitokea Shule ya Msingi John Bosco iliyopo Kata ya Tumbi.

Magumu ya Happness.

Happness, anasema amepita katika magumu mengi kwani miezi miwili tangu aanze kidato cha kwanza mwaka 2020  alimpoteza baba yake mzazi Fredy Godfrey kwa ugonjwa wa kisukari .

Anasema,kufariki kwa baba yake ndipo ikawa mwanzo mgumu wa safari yake ya elimu kwani baba yake ndiye alikuwa nguzo na tegemeo kubwa kwake na hata familia kiujumla.



Anasema mzee Godfrey alikuwa mjasiliamali wa kuuza vinywaji mbalimbali kama soda ,juisi na Maji na pesa iliyokuwa ikipatikana ndiyo ilikuwa ikiwasaidia katika mahitaji ya Chakula cha nyumbani na hata mahitaji ya shule Kwa watoto.

Maisha yalibadilika, Happness alianza kuishi maisha magumu kwakuwa mzazi wake aliyebaki( mama) hakuwa na kazi ya kufanya kwani katika maisha yake alikuwa akimtegemea mume wake.

Kutokana na hali ya nyumbani kuwa duni, Happness alikuwa anakwenda shuleni kwa msaada wa marafiki na majirani wema ambao ndio walikuwa wakimnunulia sare za Shule,kumlipia nauli,vifaa vya kusomea na mahitaji mengine ya kibinadamu.

"Mama yangu hakuwa na kazi ila miaka ya nyuma alijifunza cherahani na baada ya baba kufariki alianza kutumia cherahani kushona nguo tena viraka ambavyo vilimpa vijisenti kidogo vilivyotusaidia kupata chakula tu"anasema Happness

Happness,ameishi na mama yake katika mazingira magumu kwani hapakuwa na msaada wowote kutoka kwa familia zaidi ya kukandamizwa ili waporwe mali hususani nyumba iliyoachwa na baba yao.

Uvumilivu wa Happness ulifika ukingoni kwani baada ya kufika kidato cha tatu mambo yalikuwa magumu zaidi na hivyo kuamua kutoroka nyumbani na kuelekea kusikojulikana lakini hatahivyo alikuwa mazingira  salama kwani alifanikiwa kwenda na kurudi shuleni kila siku.

"Nilitoroka nyumbani baada ya kuona mateso na vurugu za familia zikiendelea,nikaenda kuishi sehemu ambayo hakuna aliyejua lakini nilifanikiwa kwenda Shule kila siku na mpaka nimemaliza kidato cha nne,"anasema Happness

Mahali alikokuwa anaishi Happness kulimpa wakati mgumu kwani kila siku alilazimika kupanda magari matatu mpaka manne  na bodaboda moja mpaka kufika shuleni Tumbi lakini vivyo hivyo wakati wa kurudi nyumbani.


 Maisha ya Happness akiwa barabarani:

Anasema,amekumbana na changamoto nyingi ikiwemo kunusurika na ajali na hata ushawishi wa wanaume lakini kikubwa alichokiangalia ni kuweka nia na kumtanguliza Mungu katika masomo yake.

Happness ,anasema pamoja na mambo kuwa magumu lakini aliweka malengo kwani alikuwa anatoka nyumbani saa 11 alfajiri kuelekea shuleni na kurudi nyumbani saa tatu usiku  na hakuwai kukosa kipindi darasani.
 
 Akiwa Shuleni;

Akiwa Shuleni mara nyingi alikuwa anasahau magumu anayopitia kwani aliweka kipaumbele katika masomo ambapo anasema mazingira ya Shule yalikuwa mazuri kwani alikuwa anaingia darasani mpaka saa 8:30 mchana na baada ya hapo anaingia katika vipindi vya jioni kwa ajili ya majadiliano na mwenzake.

Anasema ,sehemu ya majadiliano ilikuwa inampa hali ya kujiamini na kumjenga katika masomo yake huku akiweka lengo la kutaka kufaulu ili aweze kuendelea na masomo yake.

Matokeo yalipotangazwa.

Ilikuwa furaha kubwa kwa Happness kwani alirukaruka  na kugalagala chini mithili ya jongoo aliyeguswa na fimbo kwani furaha ilizidi kipimo na hivyo kumaliza machungu aliyoyapitia.

Happeness alishangaa kuona anapata matokeo yenye ufaulu mzuri wenye daraja la kwanza pointi Saba na hivyo kumpa nafasi katika Shule ya Tumbi Sekondari kuwa msichana kinara wa matokeo hayo.

Baada ya matokeo anasemaje?

Anasema,anaishukuru Serikali hususani Rais Samia kwa kusimamia vizuri Shule za Kata na kuendelea kutoa fedha za kuboresha Shule za Kata kwani bila kuwepo Kwa Shule hizo hata yeye hasingeweza kusoma.

Anasema ,mambo yote mazuri huwa yanakuja katika sura mbaya kama ambavyo amepitia katika mambo magumu lakini katika ufaulu kuna mambo muhimu yakuyafuata.

Happness, anasema japo la kwanza ni mwanafunzi mwenyewe kuamua na kuweka nia kwani yeye aliamua kutumia nafasi hiyo kushauriana na kushirikiana vizuri na walimu wake huku akiwa na msukumo wa kutaka kufaulu.

Jambo la pili, Happness anasema kujiwekea malengo,ambapo binafsi alijiwekea malengo ya kupata division one ya pointi Saba japo hakuwai kumwambia mtu lakini anashukuru kwani malengo yake yametimia kwa asilimia 98.

Anasema jambo la tatu ni kumtanguliza Mungu katika kila jambo kwani pamoja na misukosuko ya maisha aliyopitia lakini mara zote alikuwa karibu na  Mungu akipeleka maombi yake.

Lakini pamoja na hayo anawashukuru walimu wa Shule hiyo kwa jitihada kubwa za ufundishaji kwani wakati wote walikuwa karibu na wanafunzi katika kuwaandaa na kuwajenga kimasomo.

Haya ndio matarajio ya binti  Happness .

Happness ,anatamani kuwa daktari bingwa na mkuu wa kitengo fulani cha afya ili aweze kusaidia jamii kwa ukaribu zaidi.

 Ushauri kwa wanafunzi wenzake.

Changamoto zipo,lakini wapo wanafunzi wanamalengo ya kupata elimu kwahiyo lazima waweke msingi imara wa kufikia malengo yao na kikubwa ni kujua nini unataka(Focusing).

Anasema , wanafunzi lazima wawe na nidhamu,watoe ushirikiano kwa walimu na ikibidi wazingatie yale  wanayofundishwa darasani .

Mkuu wa Shule anena.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Tumbi Fidelis Haule,anasema wasichana waliofanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne mwaka jana walikuwa 34.

Kati ya hao waliopata ufaulu wa daraja la kwanza ni 14,waliopata daraja la pili ni 16 ,waliopata daraja la tatu ni watatu na waliopata daraja la nne ni msichana mmoja pekee ambapo ufaulu huo ni sawa na asilimia 99.

Haule,anasema siri ya ufaulu kwa wasichana hao ni nidhamu nzuri inayotekelezwa na walimu pamoja na wanafunzi wakike pamoja na motisha mbalimbali zinazotolewa kwa walimu.

Haule ,anamshukuru Makamu wa Rais Dkt .Philip Mpango ambaye Februari 4,2023 alipita shuleni hapo na kutoa motisha ya Sh.milioni 50 kwa walimu baada ya kuridhishwa na matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2022.

Amesema ,motisha ya Dkt.Mpango imekuwa chachu ya kuongeza molari Kwa walimu katika ufundishaji na kwamba aadi pekee ilikuwa kuongeza ufaulu .

Anasema , Shule yake imekuwa na vifaa vya kutosha vya kufundishia, walimu wakutosha pamoja na kuwepo kwa miundombinu mizuri iliyokarabatiwa na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia.

"Ufaulu mzuri wa wasichana hao ni jitihada za Serikali ya awamu ya Sita maana imeleta kila kitu na hata kukarabati miundombinu ya Shule yetu ,kwahiyo tunamshukuru sana Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyofanya ,"anasema Haule

Haule anasema,kazi iliyobaki kwao ni kuhakikisha wanaendelea kulipa deni kwa Rais Samia katika kuhakikisha wasichana wanaendelea kufaulu zaidi na hivyo kutoa heshima kwa Rais.

Diwani Kata ya Tumbi atoa ya moyoni.

Diwani wa Kata ya Tumbi Raymond Chokala(CCM) anasema kuwa ufaulu wa wasichana Shule ya Tumbi umetokana na ushirikiano baina ya walimu ,wazazi na wanafunzi.

Chokala,ameomba ushirikiano huo uendelee ili kuifanya Shule ya Tumbi kuwa kinara katika matokeo ya miaka ijayo  huku akimpongeza Mkuu wa shule hiyo kwa kazi kubwa anayofanya ya kusaidia wanafunzi wa shule hiyo.

Aidha,Chokala anamshukuru Rais Samia kwa jitihada kubwa anazofanya katika elimu hususani katika kuhakikisha wanafunzi wakike walioacha Shule kwa matatizo mbalimbali wanarudi shuleni kuendelea na masomo yao.

"Wanafunzi wakike walioacha shule sasa hivi wanarudi Shule kuendelea na masomo yao ,hakika ili jambo jema sana kwahiyo lazima tumshukuru Rais wetu kwa kutoa maamuzi mazuri kwa maslahi ya Taifa letu,"anasema Chokala

Chokala, amewaomba wazazi kuwa wasimamizi wa karibu wa watoto wao ili kukomesha tabia ya ukatili wa kijijsia unaofanyika katika maeneo yao na ikiwezekana wapunguze ratiba za Vikoba ili kutoa nafasi ya kukaa na watoto.

Hatahivyo,anasema wazazi wasimuamini mtu yeyote kulala na watoto wao hawe ndugu, rafiki au mtu yeyote kwani kufanya hivyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo viovu .


Club News Editor, Julieth Ngarabali

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA