ELIMU YA ULINZI NA USALAMA KWA WATOTO BADO INAHITAJIKA PWANI




Julieth Ngarabali, Pwani.

Suala la ulinzi na usalama wa mtoto hasa wa miaka chini ya nane limekua likielekezwa na kusisitizwa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wanaojishughulisha na masuala ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto kuwa ni jukumu la jamii nzima na siyo wazazi ama walezi tu wa watoto hao.

Pia Serikali kupitia kwa viongozi mbalimbali imekua ikitoa elimu juu ya umuhimu wa kumlinda mtoto dhidi ya aina zote za vitendo vya ukatili kwani vitendo hivyo huweza kuathiri mfumo wa ukuaji na maendeleo ya mtoto kiakili,kimwili na kisaikolojia.

Hata hivyo kiuhalisia kwenye maeneo mengi bado hakuna uelewa wa kutosha kufuatia kuendelea kutokea kwa matukio kadha wa kadha ya ukatili kwa watoto wakiwemo wa chini ya miaka nane ambapo watu wa eneo husika hukaa kimya bila kuyaripoti mahala popote kama ambavyo imetokea katika mtaa wa Boko Mnemela na Mwendapole Wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Hivi karibuni mkazi wa eneo la Boko Asnah Mohamed (62) amemchoma moto mjukuu wake wa kiume mwenye umri wa miaka (5) kwa tuhuma ya kuiba fedha kiasi cha shilingi 2,000 lakini majirani walikaa kimya bila kuliripoti tukio hilo kitendo ambacho sio sahihi kwani ulinzi na usalama wa watoto ni jukumu la jamii nzima na sio mzazi au mlezi pekee.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Boko Mnemela Michael Mwinza amesema baadhi ya majirani wa mtuhumiwa huyo walifahamu tukio hilo lakini hawakuchukua hatua yoyote ya kuliripoti kwa madai kuwa wamehofia kueleweka vibaya na familia ya mtuhumiwa endapo wangetoa taarifa sehemu husika juu ya mtoto huyo kuchomwa moto.

Madhara ya kutoliripoti tukio hili la ukatili

Mwinza amesema uzembe huo wa kukaa kimya ulisababisha mtoto huyo kukaa ndani kwa muda wa wiki mbili akiugulia vidonda vya moto kwani hakupelekwa hospitali mpaka alipozidi kupata maumivu makali zaidi.

‘’Nilisikia mtoto mwenzake anayechezaga naye akisema mwenzake analia ndani tu kafungiwa hivyo kama kiongozi eneo hili nilitoka kufuatilia na kugundua hali hiyo na kumhoji bibi huyo ambapo alidai mjukuu wake aliangukia kwenye moto na alipoulizwa ni kwa nini hakumpeleka hospitali hakuwa na majibu ndipo alipopelekwa ofisi ya Serikali ya Kijiji kisha alipelekwa Polisi,"amesema.

Mwinza amebainisha kuwa tukio hilo halikuripotiwa kwa muda uliotakiwa kwenye vyombo husika  kwa sababu majirani walikaa kimya pasipokutoa taarifa wakidai waliogopa kuwa endapo watatoa taarifa wataeleweka vibaya na familia ya mtuhumiwa  hivyo mtoto huyo kukaa kwa kipindi cha wiki mbili pasipo kupata matibabu.

Amesema faida ya mtoto mwenzake kutoa taarifa iliwezesha mtuhumiwa kuchukuliwa hatua ya kufikishwa Polisi na pia majeruhi alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi kwa ajili ya matibabu na mtuhumiwa ameshafikishwa Polisi kwa taratibu zingine..

Mmoja wa walimu wa Shule ya Msingi Boko anakosoma mtoto huyo (jina linahifadhiwa kwa kuwa sio msemaji wa shule ) amesema mtoto huyo ambaye anasoma darasa la kwanza Shuleni hapo alikuwa akiishi na bibi yake huyo ambaye anauza vitumbua baada ya mama yake mzazi kuolewa na mwanaume mwingine.

Aidha jirani wa mtuhumiwa Zainabu Mtende ameongeza kuwa siku ya tukio hilo mtuhimiwa alimfunga kwa kutumia kamba mikono yote miwili na kuchukua nyasi kavu kisha kumchoma na kumsababishia maumivu makali mjukuu wake.

"Bibi huyo anamlea mjukuu wake huyo tangu akiwa na mwaka mmoja baada ya mama mzazi wa mtoto kuolewa na mume mwingine ambapo aliachiwa mtoto huyo amlee,"amesema Zainabu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Pius Lutumo amesema wanamshikilia mtuhumiwa huyo ambaye amemjeruhi mjukuu wake baada ya kumchoma moto viganja vya mikono yake kwa tuhuma ya kuiba shilingi 2,000 na kwamba atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa tukio hilo kukamilika.

Tukio jingine ni la mtoto wa kike mwenye umri wa miaka saba mkazi wa Mwendapole ambaye yeye alirubuniwa na kijana anayefahamika kwa jina la Mgosi na kumbaka lakini majirani walikaa kimya hawakutoa taarifa kwa mzazi wa mtoto huyo na hivyo kupelekea mtuhumiwa kutoroka kabla ya kutiwa nguvuni.

Balozi wa Mtaa wa Mwendapole Ramadhani Biya amesema wapo baadhi watu hunyamazia matukio ya ukatili kwa sababu zao mbalimbali ambazo hazina mashiko zaidi ya kuchochea kuendelea kutokea na kushauri itungwe sheria ndogo itakayowabana watakaodhibitika kufahamu au kuyaona matukio ya ukatili kwa watoto lakini hukaa kimya.

‘’ mfano hili nilichelewa kupata taarifa na hivyo mtuhumiwa ambaye alihamia eneo hili  mwaka mmoja uliopita alitoroka na kwa sasa tunaendelea kumsaka kwa kushirikiana na Polisi, ila taarifa ingetolewa mapema kwa sasa angekua anatumikia adhabu yake kwa mujibu wa sheria na ingekua fundisho kwa wengine eneo hilo”’ amesema

Serikali kupitia Wizara yenye dhamana na Watoto iliandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 ambayo imeainisha Haki tano za Msingi za Mtoto ikiwepo haki ya kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushiriki na haki ya kutobaguliwa.

 Mkurugenzi wa Kituo Cha Msaada wa Sheria Kibaha (KPC) Catherine Mlenga amebainisha kuwa wamekuwa wakitoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili kwa wazazi lakini baadhi wamekuwa wakifanya vitendo hivyo kwa watoto.

Mlenga amesema kutokana na vitendo hivyo kuna haja ya Serikali kutoa adhabu kali kwa watu wanaofanya vitendo vya ukatili ndani ya jamii ili vitendo hivyo visiendelee kutokea na iwe fundisho kwa wanaofanya matukio hayo sambamba na kuendelea kutolewa elimu ya ulinzi na usalama wa mtoto kuwa ni jukumu la kila mtu.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya maendeleo ya jamii ,jinsia ,wanawake na makundi maalumu katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka 2022 matukio ya ukatili kwa watoto yalikua 12,163 wavulana wakiwa ni 2,201 na wasichana 9,962 ikilinganishwa na matukio 11,499 kwa mwaka 2021 sawa  na ongezeko la asilimia 5. 8










 

Comments

Popular posts from this blog

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RC PWANI AFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MKURUGENZI WA KIBAHA MJINI DKT.ROGERS SHEMWELEKWA

TANROADS YATOA UFAFANUZI KUTOZWA FAINI GARI LA SIMBA LOGISTICS KITUO CHA MIZANI YA VIGWAZA MKOA WA PWANI