BAADHI YA ASASI CHANZO CHA KUKWAMISHA UFANISI WA PROGRAM YA MALEZI.MAKUZI NA MAENDELEO YA AWALI YA MTOTO
- Ni kwa kuwakwepa maafisa maendeleo ya jamii
- Baadhi zaanza kuchukuliwa hatua.
- Serikali yaonya
Julieth Ngarabali, Pwani.
Moja ya wadau wakubwa katika utekelezaji wa program jumuishi ya Taifa ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ni maafisa ustawi wa jamii ambao hufanya kazi kwa niaba ya Serikali katika kusimamia utekelezaji wa Pogram hii ambayo Serikali imetoa maelekezo ya utekelezaji wake kusambaa maeneo yote nchini ifikapo mwezi wa nne mwaka huu.
Katika mkutano wa mwaka uliofanyika mwezi
Disemba mwaka 2023 na kuwakutanisha wadau wote kutoka Serikalini, asasi za
kiraia pamoja na waandishi wa habari,msukumo mkubwa ulikuwa kutengeneza
muunganiko wa pamoja kati ya wadau muhimun ili elimu juu ya malezi,makuzi na
maendeleo ya awali ya mtoto kuanzia umri wa miaka 0-8 iweze kuifikia jamii na
kuelewa huku kilio kikubwa kikitajwa kwa baadhi ya wadau kutoshiriki kikamilifu
ama kukwepa kufuata taratibu kama zilivyoainishwa na mpango huu wa Taifa.
Mkoani Pwani baadhi ya asasi za kiraia
zinazojihusisha na masuala ya malezi, makuzi na maendelo ya awali ya mtoto
wakiwemo wa umri chini ya miaka nane zimebainika kukwepa
kuwashirikisha Maafisa Maendeleo ya jamii kwenye shughuli
zao wanazofanya katika jamii na hivyo kufanya mambo kinyume na maadili ya
kitanzania na ya usajili wao.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi,umebaini
kuwepo kwa taasisi isiyo ya kiserikali katika moja ya kijiji Wilayani Bagamoyo
mkoani Pwani ambayo inaendesha shughuli za kulea watoto wakiwemo wenye umri
chini ya miaka 8 bila kufuata muongozo wa Taifa wa Program ya malezi,makuzi na
maendeleo ya awali ya mtoto huku shughuli zake zikiendeshwa bila kuihusisha
ofisi ya afisa maendeleo ya jamii Wilaya.
Asasi hiyo iliyotambulika kwa jina la Mango Kinder ambayo inatuhumiwa kutoa elimu isiyo na maadili ya ki Tanzania kwa watoto wadogo wakiwemo wa chini ya miaka nane katika kijiji cha Duda Bagamoyo ambapo toka Novemba 2023 ilikua ikiwakusanya watoto wengi kutoka maeneo mbalimbali Bagamoyo kwa madai ya kuwapa elimu ambayo hata hivyo imetiliwa shaka.
" Februari 06 mwaka
2024 imegundulika kuwepo taasisi moja ya Mango Kinder ambayo inatuhumiwa
kufanya malezi na kutoa elimu isiyo na maadili ya ki Tanzania kwa watoto wadogo
wakiwemo wa chini ya miaka nane katika kijiji cha Duda Bagamoyon na hawa
waliwakwepa maafisa maendeleo jamii wakawa wanajifanyia wanavyotaka,sio sahihi
kabisa"' amesema Bi. Judith Mayunga,afisa maeneelo ya Jamii kata ya
Dunda,Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Judithi ameeleza kuwepo kwa changamoto hiyo ya baadhi ya asasi za kiraia zinazojihusisha na masuala ya malezi ya watoto wakiwemo wa chini ya miaka nane kwenye uzinduzi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani mpango ambao unalenga kutatua changamoto za ukuaji na maendeleo ya watoto wenye umri wa miaka 0-8 .
Ameongeza kuwa ni muhimu na ni lazima kwa asasi zote za kiraia zinazofaya kazi za watoto kushirikiana na maafisa hao ngazi ya kata kwa sababu wanachotaka kujua maafisa hao ni huduma zinazotolewa kama zinaendana na malezi,makuzi na maadili kwa mtoto pamoja na mazingira rafiki.
“Ikumbukwe kwamba malezi ni matendo yote yanayofanywa na wazazi, walezi na jamii ikiwemo asasi za kiraia zinazojihusisha na msuala hayo kwa lengo la kumlea ,kumkuza,kumlinda,kumuendeleza mtoto kimwili,kiakili ,kijamii,kihisia na kimaadili ili aweze kuishi ,kukua vizuri na kukubalika na jamii”. Amesema Judith
Katika misingi hiyo yapo mambo muhimu ambayo
kila mmoja anapaswa kuyazingatia wakati wote wa malezi na makuzi , moja wapo ni
afya hapa mtoto anahitaji kupatiwa tiba na kinga zote dhidi ya marathi ya
kuambukiza kwa njia ya chanjo,lishe kwa maana ya chakula bora ama lishe
kamili,uchangamshi ,uangalizi kwa maana ya ulinzi wakati wote katika mazingira
anayokuwepo mtoto mamba ambayo yote haya asasi zinatakiwa kuweka wazi
nini wanachokifanya lakini baadhi huwahofia maafisa hao.
Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Halima Okash
alifika kituoni hapo na kuwakuta watoto zaidi ya 200 pamoja na zana mbalimbali
ambazo imempelekea kugundua kuwa watoto hao wakiwemo wa chini ya miaka nane
walikua hawafundishwi maadili mema na mengi ya mambo wanayofundishwa ni ya
kijinsia ambayo yanakiuka taratibu,mila na desturi za Tanzania
Uamuzi wa Serikali ilikuwa ni kuisitishia kibali
na leseni ya taasisi hiyo na wote
wanaohusika na taasisi hiyo huku wahusika wakichukuliwa kwa ajili ya mahojiano
na uchunguzi zaidi.
Katika uzinduzi huo wa PJT-MMMAM Bagamoyo
taasisi hiyo imetajwa ni mojawapo ya zinazodaiwa kuwakwepa maafisa maendeleo ya
jamii na hivyo kutakiwa sasa kutoa ushirikiano kwani zikibainika
zinakwenda kinyume na usajili wake zitachukuliwa hatua ikiwemo kufungiwa kama
hiyo ya Mango Kinder.
“’Asasi za kiraia tunajua ninyi ni wadau wetu
wakubwa wa maendeleo na malezi ya watoto wakiwemo hawa wa miaka chini ya nane
mnafanya kazi zetu kwenye kata na sisi Maafisa maendeleo ya jamii ndio waratibu
huko lakini mnatukwepa sijui mnadhani tutawaomba posho, kitu ambacho sio kweli
msiwe na hofu hii, sisi tunachotaka kujua ni mnachofanya kama kinaendana
na maadili ya mtoto”amesema Judithi.Baadhi ya wadau wa PJT
- MMMAM Bagamoyo.
Naye Mkuu wa Polisi Jamii Bagamoyo Fardina Hozza ameongeza kuwa katika kesi wanazopata inaonyesha wazazi na walezi wengi wamejitenga kulea watoto wao wameelekeza nguvu zaidi katika mambo mengine ya kijamii na kiuchumi ambayo hayahusiani zaidi na malezi bora.
“Watu wanaondoka alfajiri watoto wamelala na
wanarudi usiku wamelala ,wanaobaki wanakuwa bize na mambo yao tu hawazingatii
chochote huku nyuma hajui mtoto amebaki na msichana wa kazi au mjomba wake au
dada yake je analelewa vipi?’’ amehoji na kuongeza
“ Kwa hiyo watoto sasa hivi wanakua ilimradi tu
kitu ambacho mbali ya kukosa maadili mema wanakutana na ukatili aina tofauti
tofauti na wakiletwa kituoni unakuta ameshaharibiwa mbele na nyuma mda mrefu
hata zaidi ya wiki sita” amesema Hozza.
Amesema Bagamoyo baada ya kutoa elimu na kuweka sheria thabiti sasa kesi za ukatili za watoto zimepungua kwa kiasi kikubwa lakini mwanzo ilikua ni hatari unakuta mtoto wa miaka mitano, minne au miwili amebakwa na mjomba wake, kijana wa kazi au babu yake
“ Kwa hiyo sasa kupitia Programu hii ya PJT
‘MMMAM tukijumuika kwa pamoja kwa sababu sisi hua tunafanya dawati kama
dawati lakini tukiwa jumuishi tukafanya kazi pamoja tutaweza kufika mbali
zaidi katika malezi, makuzi na maendeleo ya awali watoto hasa hawa chini ya
miaka nane”’ amesema Hozza ambaye ni Mkuu wa Polisi Jamii Bagamoyo.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Bagamoyo
ameshauri wadau wa programu hiyo kushirikiana na serikali katika kuratibu
na kuomba Halmashauri itenge bajeti ya kufanikisha mpango huo.
Shabani Omari ni mmoja wa wazazi wenye watoto
waliokutwa kwenye taasisi hiyo iliyofungiwa anasema Serikali iwe inafanya
ufuatiliaji wa kina kwenye vituo vinavyokusanya watoto chini ya miaka nane kwa
sababu ndio inayowapa leseni ya kulea watoto ,kuliko kumlaumu mzazi ambaye yeye
anachofahamu mtoto yupo kituo salama kwa sababu kimesajiliwa na Serikali na
wapo maafisa ukaguzi wa elimu , ustawi wa jamii na mendeleo ya jamii.
Katika mkoa wa Pwani mpango huo wa PJT
-MMMAM inatekelezwa na taasisi ya ANJITA kwa kushirikiana na Serikali
kwenye eneo la afya bora ,lishe ya kutosha
kuanzia ujauzito, malezi yenye muitikio,fursa za ujifunzaji wa awali, ulinzi na
usalama kwa watoto,
Mkoa wa Pwani, kupitia madawati ya ustawi wa Jamii na maeneo
ya utoaji huduma za kijinsia katika Halmashauri yamepokea migogoro ya ndoa 689
,matunzo 908 na migogoro inayohusu watoto wa nje ya ndoa 973 katika kipindi cha
Julai hadi Disemba 2022 .
Comments
Post a Comment