Ushoroba wa tembo: Kivutio kipya milima ya Udzungwa

  • Ni Ushoroba mpya utakaomaliza pia migogoro ya binadamu na tembo Tanzania

                   Njia ya chini ya kupita Tembo(underpass )katika shoroba ya Nyerere -Selous- Udzungwa

Na Gustaphu Haule, Kilombero

“MWAKA 2018 hatutaweza kusahau katika maisha yetu, jinsi tulivyomwona yule jamaa akiuwawa kwa kuchanwa chanwa na Tembo, yaani tulivyoenda kumuona asubuhi daaah!!!! Hakika tukio lile ni moja ya matukio mabaya yaliyowahi kutokea hapa Magombera.

“Kifo cha mwanakijiji mwenzetu Bata Limu kilikuwa kikali sana, kwa kweli kilisikitisha kwa sababu yule mtu alichanwa vipande vipande. Hakika kilikuwa kifo cha majonzi makubwa  na ndio kifo cha kwanza tulichowai kukishuhudia.

“Leo hii tunapomuona Tembo sisi wanakijiji wa Magombera tunamheshimu na tunakimbia mbali sana kwa kuwa tunajua kuwa Tembo ni mnyama mwenye madhara makubwa endapo utamsogelea.”

Haya ni maneno ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Magombera, Kata ya Mkura katika Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Said Simba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho Novemba 23, 2023.
           Mwenyekiti wa Kijiji cha Magombera Said Simba akizungumza na waandishi wa habari Kijiji humo.(picha na Gustaphu Haule)

Waandishi hao walifika kijijini hapo kwa ajili ya mafunzo ya vitendo ya kuripoti habari za bioanuai yaliyoandaliwa na kampuni ya Nukta Africa kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) chini ya mradi wake wa “USAID Tuhifadhi Maliasili.”

Simba ambaye ameishi miaka tisa katika kijiji hicho maarufu wa kilimo cha mpunga anasema kero kubwa kwao ni muingiliano wa shughuli za binadamu na mnyama Tembo.

Anasema kwa muda aliokaa kijijini hapo hajawai kuvuna mpunga licha ya kuweka juhudi kubwa katika kilimo cha zao hilo.

Tembo ndio walikuwa wakiwakatisha tamaa wakulima kwani wakati wote wanapita mashambani na kutafuna mpunga. 

"Nimekaa Magombera miaka tisa lakini sijawai kuvuna mpunga, hata wanakijiji wangu nao kila siku walikuwa wanalia juu ya Tembo kupita katika mashamba yao na wakati mwingine huwa tulikuwa tunaacha kabisa kulima kwa hofu ya Tembo," anasema Simba.

Shida juu ya shida
Sauti kutoka katika Kijiji cha Magombera haikuishia tu kwa Simba lakini pia ipo sauti nyingine iliyosikika kutoka kwa Shaban Juma ambaye ameishi kwa miaka mitano katika kijiji hicho.

Juma mwenye umri wa miaka 24 ni baba wa mtoto mmoja anasema siku moja alipatwa na madhara baada ya kumkimbia Tembo aliyekuwa akipita katika maeneo ya shambani kwake.

Juma alikuwa wa kwanza kumuona Tembo lakini Tembo hakumuona Juma. Juma alianza kutimua mbio mwenyewe na ndipo akajikuta anaumia mguu wake wa kushoto na kupata maumivu makali.

Juma kwa sasa ni mfanyakazi wa Shirika lisilo la Serikali la Uhifadhi wa Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP) ambalo limejikita katika Ukanda wa Mashariki wa Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Iringa.

Migogoro ya binadamu na tembo imetokana na kuwepo kwa ushoroba wa wanyamapori katika kijiji hicho unaojulikana kama Nyerere Selous-Udzungwa ambao ndio mapitio ya asili ya Tembo.

Kutokana na hali hiyo, Tembo wamekuwa wakitoka hifadhini na kuingia katika mashamba ya wakulima na hata katika makazi ya wananchi na hivyo kuleta madhara mbalimbali kwa binadamu na mazao shambani.

Tembo msumbufu zaidi
Miongoni mwa Tembo aliyekuwa akisumbua zaidi ni Tembo anayejulikana kwa jina la Kieleni. Tembo huyu alama yake kubwa ni kukosa meno na mwenye kuwa na sifa za ugomvi.

Tembo Kieleni anaelezwa kuwa ni mkorofi tena mbabe. Huiingia majumbani na akikuona anakukimbiza ili yeye aweze kula ndizi au miwa uliyopanda na kama unajisahau basi anakuvaa na kukujeruhi vibaya.

Undani wa ushoroba wa Nyerere Selous - Udzungwa
Meneja Shoroba wa STEP Joseph Mwalugelo anasema ushoroba wa Nyerere Selous -Udzungwa una urefu wa kilomita 12.6 na upana mita 150 mpaka 200.

Ushoroba huo ulianzishwa kupitia Sheria ya Uhifadhi ya Shoroba ya Mwaka 2009 lakini kanuni ya kusimamia shoroba ilikuja mwaka 2018 ambapo lengo kubwa ni kuhakikisha uhifadhi wa Tembo unakuwa salama na binadamu pia.

“Ushoroba wa Nyerere Selous - Udzungwa pia unaitwa ushoroba wa Tembo bonde la Kilombero (Kilombero Elephant Corridor) kwa kuwa ni miongoni mwa shoroba za awali ambazo zilifungwa katika maeneo hayo,” anasema Mwalugelo.

Ushoroba huo na nyingine zilifungwa kutokana na muingiliano mkubwa wa Tembo na shughuli za kibinadamu lakini ushoroba huo iko katika mchakato wa kuunusuru na ukarudi kama zamani.

Kwa mujibu wa STEP, ushoroba huo umepita katika vijiji vitatu vya Mang'ula "A", Sore na Kanyenja na unaunganisha Milima ya Udzungwa ikipitia Kijiji cha Magombera na kuunganisha hifadhi ya Taifa ya Nyerere.

Ushoroba huo umeanzishwa kwa tangazo la Serikali namba 123 wa mwaka 2018 kwa jitihada kubwa zilizofanywa na STEP kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa faida ya Tanzania chini ya mradi wa “USAID Protection”.

      Meneja ushoroba wa Nyerere Selous -Udzungwa Josephu Mwalugelo,akiwaelezea waandishi wa habari juu ya        umuhimu wa kuanzishwa kwa ushoroba huo .

Anasema awali kabla ya Shirika la STEP kufufua Shoroba huo kulionekana madhara mengi yakitokea kati ya Tembo na binadamu ikiwemo mwaka 2019/2020 wanafunzi kujeruhiwa na hata waumini kuvamiwa asubuhi wakiwa wanaenda kanisani.

Baada ya kuona madhara hayo, STEP ilianza kufanya utafiti na ufuatiliaji ikiwemo kufunga kamera sehemu ambazo Tembo wanatoka ikiwemo Magombera na upande wa Nyerere.

"Baada ya kufunga kamera tulianza kuwaelimisha wananchi  juu ya umuhimu wa kuanzisha hifadhi kupitia shoroba na kisha kuunda kamati ya usimamizi wa shoroba ikijumuisha wenyeviti wa vijiji, mkurugenzi na kiongozi wa kamati hiyo ni mkuu wa wilaya," anasema Mwalugelo ambapo 

Mwaka 2021 kamati hiyo ilizinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na kisha kuanza kazi rasmi ya utekelezaji wa kufufua ushoroba huo.

Tembo kujidai katika barabara zao

Miongoni mwa kazi zilizofanyika ni kupanua barabara na kutengeneza njia za chini za kupita Tembo (Underpass) yenye urefu wa mita  4.5 na upana mita 5 ikiwa na lengo la kunusuru wanafunzi kutoka Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa hadi Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.

Teknolojia ya kutengeneza njia za chini za Tembo imechukuliwa nchini Kenya ambapo kwa mwaka mmoja jumla ya Tembo 1000 walikuwa wamepita katika njia hizo na ndipo wakaona wailete Tanzania.

Pia shoroba ya Nyerere Selous - Udzungwa imepitiwa na reli na kwamba miaka miwili iliyopita Tembo Sita waligongwa na treni lakini kwa sasa wamejaribu kuweka alama na kuainisha maeneo yote wanayopita wanyamapori hao ili kuzuia vifo hivyo.
    Fensi ya Bati katika Shoroba ya Nyerere-Selous -Udzungwa iliyowekwa na STEP katika Kijiji cha Magombera. 

Meneja Mradi wa Mahusiano ya Tembo na Binadamu kutoka STEP, Lim Kim anasema wameamua kuimarisha ushoroba huo kwa ajili kuendeleza uhifadhi hapa nchini.

Lim anasema kukamilika kwa ushoroba huo ni sehemu ya kuongeza idadi ya watalii kutoka nchi za nje na hata ndani ya nchi na hivyo kufanya Milima ya Udzungwa kupata umaarufu zaidi na hivyo kuongeza pato la Taifa.

"Mbali na kuzuia madhara ya Tembo kwa binadamu lakini malengo yetu mengine ni kuhakikisha tunaimarisha ushoroba huu kwa ajili ya kuchangia masuala ya uhifadhi na utalii hapa nchini na sasa tupo mbioni kutengeneza bango kubwa la kuonyesha ushoroba huu na tutaliweka pale Mikumi," anasema Lim.

Fensi ya nyuki kiboko ya Tembo
Afisa Uhusiano  Mradi wa Tembo na binadamu kutoka STEP, Catherine Kimario anasema kuwa changamoto zilizokuwa zinawakumba wananchi juu ya madhara ya Tembo kwa sasa zimepungua na hali ipo shwari.

Hiyo ni kutokana na matumizi ya fensi ya mizinga ya nyuki ambayo huwazuia Tembo kutoka hifadhini.

      Afisa uhusiano wa Tembo na Binadamu kutoka Shirika la STEP Catherine Kimario akimuelezea mwaandishi wa habari umuhimu wa fensi ya nyuki iliyofungwa katika milima ya Udzungwa .(picha na Gustaphu Haule )

Kimario anasema awali walianza kutengeneza fensi ya pilipili iliyochanganywa na oil chafu na kisha kupakwa katika fensi ya miti na nyaya lakini kwa kiasi kikubwa ilileta mafaniko lakini wamekuja na mbinu mpya.

"Fensi hizi mbili zote zilifanikiwa lakini hii ya nyuki ilikuwa na mafanikio zaidi kwani Tembo anapogusa fensi hiyo ushambuliwa na nyuki na kisha Tembo kukimbia na hatimaye kuogopa kupita katika eneo hilo," anasema Kimario.

Kwa sasa STEP imekuja na teknolojia ya kutengeneza fensi ya bati ambayo tayari imefungwa katika shoroba hiyo katika vijiji vya Magombera na Kanyenja..

Wanaendelea kubuni aina nyingine ya fensi ili kuhakikisha malengo ya kuzuia Tembo kutoka katika ushoroba huo yanakwisha kabisa na hivyo kufanya wananchi waishi kwa amani na usalama.

            Njia ya Tembo iliyoanzia katika milima ya  Udzungwa ikielekea Nyerere na Selous





Club News Editor, Julieth Ngarabali

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA