RC KUNENGE APIGA KAMBI BAGAMOYO KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI WILAYANI HUMO
Na Gustafu Haule,Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,leo Januari 24 amefika Wilayani Bagamoyo kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi hususani migogoro ya ardhi.
Katika ziara hiyo Kunenge ameambatana na wataalamu kutoka ofisini kwake ikiwemo kitengo cha idara ya ardhi na Sheria pamoja kamati ya ulinzi na usalama ya Wilayani Bagamoyo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani akiwa na wataalamu kutoka Ofisi yake na Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Bagamoyo katika Mkutano na wananchi wilayani humo
Kunenge,amefika Wilayani Bagamoyo ikiwa ni sehemu ya kutekeleza maagizo ya Waziri wa Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( Tamisemi) Mohamed Mchengerwa aliyoitoa mwishoni mwa wiki iliyopita Wilayani Bagamoyo.
Mchengerwa,alitoa maagizo hayo katika ziara ya Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Paul Makonda ambaye alipita Wilayani humo na kupokea changamoto mbalimbali ikiwemo masuala ya Ardhi.
Akiwa Wilayani Bagamoyo Kunenge amekutana na wananchi mbalimbali ambapo mbali na kutatua kero hizo amezungumza na Wananchi hao huku akisema Serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni sikivu.
Wananchi wilayani Bagamoyowakimsikiliza Mkuu wa Mkoa
Kunenge,amesema Serikali lazima ihakikishe kila mwenye haki anapata haki yake bila kuonea mtu na kikubwa ni ukweli kwakuwa ukweli unamuweka mtu huru.
Mkuu wa Mkoa Abubakar Kunenge akihutubia wananchi wilayani Bagamoyo
"Nimekuja hapa kusikiliza kero na changamoto zenu lakini lazima tujue yapo ambayo yatapata majibu hapa hapa na mengine kutoka nayo kwenda kuyafanyiakazi na ambayo yatakuwa juu ya uwezo wetu tutayapeleka juu,"amesema Kunenge
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okash,akiwa katika mkutano huo amemkaribisha mkuu wa Mkoa huku akisema tayari mengine alishaanza kuyafanyiakazi tangu wiki iliyopita.
Mwisho.
Club News Editor - Charles Kusaga
Comments
Post a Comment