MWELEKEO MPYA UTALII HIFADHI YA TAIFA YA MILIMA UDZUNGWA



Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa

Na Gustaphu Haule, Kilombero 

UNAPOVITAJA vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania hutakosa kutaja Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa kutokana na upekee wa vivutio vilivyopo.

Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa inapatikana katika Kata ya Mang'ula, Halmashauri  ya Mji Ifakara Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro ikiwa ni kilomita 350 kutoka Jiji la Dar es Salaam.

Asili ya jina la hifadhi ya Milima ya Udzungwa imetokana na milima hiyo  ikiwa na maana ya nchi ya Wadzungwa tawi la Wahehe ambapo kilele chake cha juu ni mlima Luhombero.

Udzungwa ni hifadhi pekee iliyopo Kanda ya Mashariki mkoani Morogoro yenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,900 na kufanya kuwa hifadhi kubwa kuliko zote ukanda wa Mashariki mwa Tanzania.

Hifadhi hii maarufu yenye vitu adimu ambavyo ni hazina kwa Taifa. Ina aina  nyingi za mimea, ndege na wanyamapori ambao hawapatikani sehemu nyingine yoyote duniani.

Moja ya vivutio hivyo ni nyani ya aina ya Mbega Wekundu na Sanje (Crested Mangabey).

Mbega wekundu waliopo Hifadhi ya Mlima Udzungwa

Pia wapo ndege aina nne akiwemo Chozi Bawa Wekundu, jamii mpya ya Kwale wa Udzungwa na Komba ambao kwa pamoja hufanya hifadhi hiyo kuwa ni makazi makuu na muhimu kwa ndege pori barani Afrika.

Tunasema Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa imebarikiwa kwani kuna maporomoko ya Mto Sanje yenye urefu wa mita 170 ambayo yanapotua yanaleta ukungu kiasi cha kuwavutia watalii.

Upekee wa hifadhi hiyo.

Mandhari yake ni nzuri na yenye kuvutia hasa ukiingia ndani ya msitu utakutana na miti mizuri, mirefu na mifupi, vilele vya mlima, makumbusho ya kale yenye rasilimali za kitamaduni na kidini.

Ukifika Mlima Udzungwa utakutana na wadudu mbalimbali ambao hupiga mruzi kwa hisia tofauti kiasi ambacho sauti zao hufananishwa na sauti za redio.

Udzungwa na vivutio vya aina yake.

Maporomoko ya Sanje yaliyoko katika hifadhi ya Milima ya Udzungwa
 
Kuna ua ambalo linapatikana ndani ya hifadhi katikati ya miti mirefu inayofikia mita 30 ambalo harufu yake ni mithili ya manukato yanayotumika kujipulizia binadamu.

Kama haitoshi ,ukiingia katika hifadhi hiyo unaweza kupata utalii wa kutembea umbali wa kilomita 400 huku ukishuhudia wanyamapori kama vile Simba, Tembo, Nyati, Chui na wengineo wengi.

Mita 200 kutoka katika lango la kuingia ndani ya hifadhi hiyo nakutana na Edwin Mwangosi (62), Mkazi wa Mang'ula "A" anasema amefanya utalii mara kadhaa katika hifadhi hiyo na ameona maajabu ambayo hakuyaona sehemu nyingine yoyote.

"Binafsi nimetembelea katika hifadhi ya Mlima Udzungwa lakini nimebahatika kuona vitu vingi vya asili hasa maporomoko ya Sanje na Nyani Wekundu maana nina miaka mingi lakini sikuwahi kuona wanyama wa namna hii," anasema Mwangosi, mkulima wa mpunga wilayani Kilombero.

Mwangosi anajivunia kuwepo kwa hifadhi hiyo kwa sababu anapata hewa safi kutokana na uhifadhi mzuri wa mazingira unaoendelea. 

Kwa mujibu wa Mwangosi, uongozi wa hifadhi hiyo umekuwa ukishirikiana na wananchi hasa katika kutoa elimu juu ya kulinda na kutunza mazingira  huku wananchi wakitoa ushirikiano kulinda rasilimali zake.

"Nimekuwa nikishiriki mikutano mingi ya wananchi inayoitishwa na hawa wenzetu wa uhifadhi kuhusu elimu ya umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira.

“Na sisi tumegeuka kuwa watu wahifadhi kwani tukiona mtu anaingia katika hifadhi kwa kufanya uharibifu wowote tunakuwa mstari wa mbele kumkamata na kumpeleka kwa uongozi wa uhifadhi kwa hatua zaidi,” anasema Mwangosi.

Vivutio zaidi.

Kamishna Msaidizi wa uhifadhi wa hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa  Abel Mtui anasema upekee wa hifadhi hiyo imekuwa kivutio kikubwa kwa Watanzania tofauti na hifadhi nyingine.

                     Moja ya Ndege katika hifadhi ya Mlima Udzungwa

Mtui anasema hifadhi hiyo imebarikiwa kuwa na aina ya miti 2500 ambayo hutumika kutengenezea dawa za kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu na wanyama.

Pia imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya maji kwani kuna zaidi ya mito 38 na huchangia maji  yanayoelekea katika kituo cha bwawa la kuzalisha umeme cha Kidatu.

Anasema vivutio hivyo huwavutia zaidi Watanzania kuliko wageni kwa sababu kila mwaka asilimia 75 wanaotembelea hifadhi hiyo ni wazawa.  

Kwa mujibu wa Mtui, mwaka 2004 walipokea watalii 4,000 lakini mwaka 2008 walifikia 8,000 na mwaka 2023 wamepokea watalii 11,000.

"Hifadhi yetu inapendwa sana na Watanzania na kwa sasa ndio tunaongoza kwa kutembelewa na Watanzania wanaofikia asilimia 75 na wengi wao wanapenda kuona hiki kivutio cha maporomoko ya mto Sanje," anasema Mtui. 

Mtui alikuwa akizungumza hivi karibuni katika mafunzo ya vitendo ya kuripoti habari za bioanuai yaliyoandaliwa na kampuni ya Nukta Africa chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili. 

Mikakati ya kutunza hifadhi hiyo

Mtui anasema kwa sasa kuna kazi kubwa inafanywa kwa kushirikiana na wadau hasa katika kufufua njia za kupita tembo chini ya daraja (underpass) ambayo kukamilika kwake itakuwa sehemu ya utalii.

Mkakati mwingine ni kutengeneza ushoroba wa Mwalimu Nyerere -Selous- Udzungwa ambao itakuwa sehemu pekee ya Tanzania kuwa na Ushoroba wa tembo na kwamba huo ni mradi wa kipekee na kazi imeshaanza kufanyika.

"Tunaamini kupitia ushoroba tunaotengeneza kutoka hapa hifadhi ya Mlima Udzungwa mpaka hifadhi ya Mwalimu Nyerere itakuwa kivutio kikubwa cha watalii kwa kuwa ushoroba huo utahusika na tembo pekee,” anasema Mtui.

Viunzi vya kuvuka. 

Changamoto zinazoikabili hifadhi hiyo ni pamoja na uvamizi katika hifadhi wa kukata miti kwa ajili ya kuni na mbao pamoja na ujangili wa wanyamapori.

Hali hiyo inasababishwa na ukosefu wa mipaka (Bafa Zone) inayotenganisha eneo la wakulima, mifugo na hifadhi.

Mtui anasema wanatumia njia shirikishi kutatua changamoto hizo ikiwemo doria za askari wa uhifadhi na kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi karibu na hifadhi hiyo ili wawe sehemu ya uhifadhi.

  Kamishna Msaidizi wa uhifadhi wa hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa  Abel Mtui akiwaeleza waandishi wa habari juu ya vivutio vya utalii vilivyopo katika hifadhi hiyo.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, mwaka 2023 Tanzania ilipata watalii milioni 1.47 ambapo idadi hiyo imeongezeka kutoka milioni 1.45 waliorekodiwa mwaka 2022.

Idadi hiyo ya watalii walioingia Tanzania mwaka 2023 huenda ikawa kubwa zaidi ikizingatiwa takwimu zake ni za miezi 10 tu yaani ni za Januari hadi Oktoba.

Ongezeko la watalii nchini imetokana na juhudi za Serikali kutangaza utalii ikiwemo programu ya filamu ya The Royal Tour ambayo mwasisi wake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Meneja Mradi Mahusiano ya Tembo na binadamu kutoka shirika lisilokuwa la Serikali la Southern Tanzania Elephant Program (STEP) Kim Lim anasema wanashirikiana na Hifadhi ya Udzungwa katika kukuza masuala ya Utalii .

Kazi kubwa wanayofanya ni kuhakikisha idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi ya Mlima Udzungwa inaongezeka kila mwaka kwa kutunza na kuvitangaza vivutio vya utalii. 

Lim, anasema kupitia uongozi wa hifadhi hiyo, STEP limefanikiwa kuingia makubaliano na Balozi wa Poland nchini Tanzania kwa ajili ya kutengeneza filamu ya Hifadhi ya Milima ya Udzungwa.

Kazi ya kutengeneza filamu hiyo tayari imeshaanza na mara ikikamilika itawekewa utaratibu wa kuitangaza katika katika maeneo mbalimbali kupitia vyombo vya habari.

“Step tunafanya kazi kubwa ya uhifadhi mazingira hasa katika Mlima Udzungwa lengo kubwa ni kutangaza vivutio vilivyopo ili kuwavutia watalii na kwa sasa tunakamilisha shughuli ya ushoroba na kisha kuweka mabango eneo la Mikumi kwa ajili ya kutangaza utalii," anasema Lim.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict Wakulyamba anasisitiza wadau kuendelea kushirikiana kulinda na kuendeleza hifadhi za Taifa ili zilete matokeo chanya.

"Lazima tulinde maliasili zetu kwa udi na uvumba, ndiyo kazi tuliyokabidhiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba,  hatujapewa kwa hisani ya mtu tumepewa kwa mujibu wa Katiba na sheria za bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” anasema Kamishna Wakulyamba.

        Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict Wakulyamba



Club News Editor - Julieth Ngarabali

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA