MVUA YAUA WATATU, MMOJA ANING'INIA MTINI KWA SAA NNE




Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Bigwa Manispaa ya Morogoro wakishuhudia uopoaji miili ya watu watatu waliokufa maji kwenye mto Mgolole
 

Na. Mwandishi wetu.

 Watu watatu wamekufa maji na mmoja kunusurika kifo Mkoani Morogoro wakati wakivuka korongo lililopo karibu na mto Mgolole ambapo maji yalikuwa yakipita kwa kasi kufuatia mvua kubwa zilizonyesha usiku wa kuamkia Januari 10,2024.

Akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari ,Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Morogoro Shaban Marugujo amesema aliyenusurika kifo ni Sengo Hamis(47) ambaye alipanda juu ya mti kwa zaidi ya saa nne.

Amesema vifo vya watu hao vilitokea katika mtaa wa Lukuyu kata ya Bigwa Manispaa ya Morogoro na kwamba tayari miili miwili imeshaopolewa na jitihada za kuupata uliobaki zinaendelea

‘ni kweli watu watatu wamepoteza uhai na wameshatambuliwa majina yao ni Asnath Thomas, Theresia Adolf(73) pamoja na  Mwanahamis Issa(35) na taarifa ya hili tukio tulichelewa kupata maana ilitufikia saa mbili asubuhi ya leo [Januari 11,2024] na tukio lilitokea majira ya saa saba hivi usiku.”amesema na kuongeza

“Tunaona namna muda ulivyopotea bila taarifa kutolewa, lakini taarifa ingetolewa mapema uwezekano wa kuwaokoa waliofariki ingewezekana,  sasa juhudi za kuutafuta mwili wa Mwanahamisi zinaendelea,”ameongeza

Kamanda huyo pia ametahadharisha tabia ya baadhi ya wananchi kupima maji kwa kuona ama kuweka mti huku akiwataka kusubiri maji kupungua ama kuchuku tahadhari nyingine zaidi kabla ya kuamua kuyavuka.

Awali Mwenyekiti wa mtaa wa Bigwa standi Benjamin Suzee amesema siku hiyo ilinyesha mvua kubwa katika mtaa huo ambapo ilipelekea mto huo kujaa maji  na kusababisha tukio hilo


Ameongeza kuwa majeruhi wa mafuriko hayo amelazwa katika hospitali ya rufaa mkoani humo na kwamba waliokumbwa na tukio hilo ni familia ya majeruhi huyo Sengo ambaye ndiye aliyetoa taarifa baada ya yeye kufanikiwa kupanda juu ya mti

‘nashauri kila mtu achukue tahadhari hasa kipindi hiki cha mvua ambapo pamekuwa na matukio mbalimbali ya watu kusombwa na maji ama kuingiliwa na maji kwenye makazi yao”amesema Benjamin






Club News Editor; Julieth Ngarabali

Comments

Popular posts from this blog

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA

RC PWANI AFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MKURUGENZI WA KIBAHA MJINI DKT.ROGERS SHEMWELEKWA