Miradi ya Kijamii inavyoipa thamani Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa
Na Monica Msomba ,Kilombero
Hifadhi hii iliyoanzishwa mwaka1992 ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 1900 ni kati ya hifadhi 22 zilizopo Tanzania.
Maporomoko ya Sanje ambayo yapo ndani ya hifadhi hii yanamwaga maji yake ardhini ambayo yanaleta ukungu wa kuvutia watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Udzungwa ni moja kati ya hifadhi za Taifa Tanzania ambazo zimepata mradi wa Regrow wa kuendeleza hifadhi za kusini ambao unalenga hifadhi za Nyerere, Mikumi, Ruaha na Udzungwa.
Mradi huo unalenga kuimarisha ulinzi wa hifadhi hizo na kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi karibu na hifadhi hizo kupitia vikundi vya kijamii.
Moja kati ya miradi hiyo ni pamoja na ufugaji wa nyuki unaotokana na fensi ya mizinga ya nyuki, mpango ambao unaratibiwa na wadau wa uhifadhi kutoka katika Shirika la Uhifadhi wa Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP).
Ahmed Churi ( 65) ni mwalimu katika kikundi cha Njokomoni kilichopo Kijiji cha Magombera wilayani Kilombero anasema wamekuwa wakinufaika na mradi wao wa fensi ya mzinga ya nyuki iliyopo pembezoni mwa mlima huo.
Fensi hiyo ya chuma yenye mizinga ya nyuki ilijengwa ili kuzuia tembo wanaoingia katika makazi ya watu na mashambani na kufanya uharibifu.
Fensi hiyo hufanya kazi kama kinga kwa sababu tembo akijaribu kuiguza anatingisha mzinga na nyuki hutoka na kutoa sauti ambayo humkera na kurudi hifadhini.
Kupitia mizinga hiyo wanapata asali na nta ambayo huuza kisha kujipatia kipato cha kuendeleza maisha.
Churi, baba wa familia ya mke mmoja na watoto watano anasema kikundi chao kilianzshwa mwaka 2012 kikiwa na wanachama 30.
Sambamba na malengo mengine lakini kubwa zaidi ilikuwa ni kuungana kwa kupambana na mnyama Tembo ili asiingie katika mashamba ya wakulima ambao mara nyingi walikuwa wakilima lakini walijikuta hawapati chochote kutokana na Tembo kuharibu mazao. .
Wakiwa tayari wameanza harakati zao walifanikiwa kuwapata wafadhili kutoka Shirika la STEP ambao walisaidia kutengeneza fensi ya kwanza iliyojulikana kama chili fensi ambayo ilitumia kamba na kushikilia miti halafu inafungwa vitambaa na kuchanganya na pilipili.
Katika fensi hii baada ya pilipilii kuchanganywa hatua inayofuata ni vitambaa hivyo kuloweshwa kweye mafuta na kisha kuvitundika katika miti ya fensi ambapo tembo walianza kuona ni karahaa kuingia katika mashamba ya wakulima kutokana na kuwashwa wanapopita kwenye mashamba ya wakulima.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, idadi ya tembo imeongezeka kutoka 43,330 mwaka 2014 hadi 60,000 mwaka 2023 na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa nchi ya tatu barani Afrika kwa kuwa na tembo wengi.
Matokeo ya Sensa ya Wanyamapori katika Mfumo Ikolojia wa Nyerere - Selous - Mikumi - Liparamba yanaonyesha kuwa idadi ya tembo ni 20,006.
Matokeo haya yakilinganishwa na sensa ya mwaka 2018, idadi ya tembo imeongezeka kwa asilimia 22.
Ongezeko hilo la tembo limekuwa likichangia wanyamapori hao kuingia katika maeneo ya watu na kufanya uharibifu.
Nyuki ni mkombozi
Kutokana na teknolojia kukua siku hadi siku walilazimika kuacha fensi ya chili kwa kuwa tayari ilikuwa imezoeleka na Tembo hao.
“Kulikuwa na changamoto moja, hii fensi ya pilipili kipindi cha mvua ilikuwa inatoka na hivyo kusababisha Tembo kupita hovyo, tukalazimika kubuni mbinu mpya ya kuwazuia ambayo ni fensi ya nyuki tunaitumia mpaka sasa na imekuwa na mafanikioa makubwa,” anasema Churi.
Moja ya mizinga ya nyuki iliyopo katika hifadhi ya Milima ya Udzungwa(Picha,Na.Monica Msomba)
Churi aliwaeleza hayo waandishi wa habari walioshiriki mafunzo kwa vitendo ya kuripoti habari za Bioanuai yaliyoratibiwa na kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa na kufadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Kupitia mradi wa “USAID Tuhifadhi Maliasili”.
“Kusudi la fensi lilikuwa ni Tembo wasiingie kwenye makazi na kuharibu nyumba na mazao, na hivyo sambamba na kufanya hivyo pia tumeielimisha jamii isiwaue kwani ni rasilimali ya Taifa.
“Pia kupitia wao watalii wanakuja na kuongeza pato la Taifa na kutoa fedha za miradi mbalimbali kama barabara, shule na vituo vya huduma za afya,” anasema Churi.
Fensi hii ya nyuki pia imekuwa msaada kwa kuzuia moto kutoka katika maeneo ya watu kuingia katika Hifadhi ya Milima ya Udzungwa. Miaka ya nyuma moto ulikuwa unawaka mara kwa mara na kusababisha madhara.
“Tunapoizungumzia fensi ya nyuki tunazungumzia mlinzi anayetatua matatizo zaidi ya moja kwani hata wale watu ambao ni wawindaji haramu walikuwa wanaingia kutega mitego ndani ya eneo la hifadhi sasa hawawezi kuiingia tena,” anasema mwalimu huyo.
Ni faida mara mbili
Wiliam Ngowi (56 )ambaye ni katibu wa kikundi cha Njokomoni anasema kutokana na wingi wa tembo waliokuwa wanaingia kwenye mashamba ya wakulima waliamua kuanza na uzio wa pilipili na kwamba kupitia uzio wa nyuki sasa wananufaika na asali.
Wiliam Ngowi Katibu wa kikundi cha Njokomoni akielezea kwa Waandishi wa habari kuhusu miradi hiyo ya fensi (Picha Na. Monica Msomba)Meneja Mradi wa mahusiano ya Tembo na Binadamu kutoka Shirika la STEP, Kim Lim anasema wamewasaidia vikundi saba vyenye wanachama 148 wakiwemo wanawake 69 ambao wanamiliki mizinga ya nyuki 463.
Meneja Mradi wa mahusiano ya Tembo na Binadamu kutoka Shirika la STEP(Picha Na. Monica Msomba)Siyo rahisi kumdhibiti tembo wa Udzungwa
Kim anasema tembo ana akili sana jambo ambalo linawafanya kuendelea kubuni mbinu mpya kila wakati za kuwadhibiti huku wakiboresha maisha ya watu wanaoishi karibu na hifadhi ya Milima ya Udzungwa.
Tembo katika hifadhi ya Milima ya Udzungwa
STEP ni miongoni mwa taasisi zinafanya kazi kwa karibu na hifadhi hiyo hasa kutunza bioanuai yake ili kulinufaisha Taifa.
Mkuu wa Hifadhi ya Milima ya Udzungwa, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Abel Peter anasema kupitia mradi wa Reglow, Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa imepatiwa vitendea kazi yakiwemo magari kupunguza migogoro ya binadamu na tembo.
Anasema pia wamepatiwa fedha za kuboresha miundombinu ya hifadhi hiyo ili kutunza vivutio vyake.
“Pamoja na kuwepo kwa vivutio vingi vya utalii katika hifadhi hii lakini bado tumeweka mikakati ya kuhakikisha tunaongeza vivutio vingine ili kusudi tuweze kupata watalii wengi zaidi,” anasema Kamishna Msaidizi Peter.
Mkakati uliopo ni kutengeneza njia maalum za kupitia Tembo chini ya daraja zinazounganisha na ushoroba wa Nyerere-Selous-Udzungwa ambapo kukamilika kwake itakuwa sehemu ya kuvutia watalii.
Mtui anasema wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia mikutano mbalimbali ili waweze kutambua umuhimu wa hifadhi hiyo na hivyo kuondokana tabia ya kuvamia hifadhi hovyo.
Comments
Post a Comment