MARUFUKU GARI LA WAGONJWA KUGEUZWA DALADALA KIBAHA





Na Julieth Mkireri,  Kibaha.

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Michael Mwakamo,amepiga marufuku tabia ya kutumia magari ya wagonjwa kama daladala la kubebea watendaji kuwapeleka kazini na kuwarudisha makwao na badala yake magari hayo yafanyekazi iliyokusudiwa. 

Mwakamo,ametoa tahadhari hiyo wakati akikabidhi gari la kubebea wagonjwa kwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kibaha Vijijini ikiwa ni kwa ajili ya  matumizi katika hospitali ya Wilaya iliyopo Mamlaka ya Mji mdogo wa Mlandizi. 

Mwakamo amesema ili gari hilo liweze kudumu kwa muda mrefu linatakiwa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ambayo ni kubebea wagonjwa pamoja na dharula nyingine zinazohusiana na masuala ya hospitali.

"Gari hili linakuja kuondoa kikwazo cha uhaba wa magari kilichokuwepo awali, natoa angalizo lisitumike kama daladala ya kubebea watendaji wanapoenda kazini, pandeni daladala, bajaji sio kupanda kwenye hili gari, mkifanya hivyo tatizo litarudi tena," amesisitiza.

Mwakamo,pamoja na mambo mengine ametumia fursa hiyo kueleza kuwa ujio wa gari ni jitihada za kuleta maendeleo katika Jimbo hilo na kwamba ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa namna inavyotoa fedha na vitendea kazi katika kumaliza kero za Wananchi.

 

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Dk.Wilford Kondo amesema  hakuna mgonjwa atakayetozwa fedha kwa huduma ya gari hilo na kusisitiza kuwa mwananchi yeyote  atakayetozwa fedha ya mafuta atoe taarifa maramoja.

Dk .Kondo amewataka wananchi kufika kupata huduma katika hospitali ya Wilaya kwani huduma nyingi kwasasa zinapatikana katika hospitali hiyo tofauti na awali ambapo ilikuwa lazima mgonjwa apewe rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi.

 Diwani wa Kata ya  Mlandizi Euphrasia Kadala ameshukuru kupatikana kwa  gari hilo ambalo kwasasa litakwenda kuondoa adha kwa wagonjwa na idara nzima ya afya katika Halmashauri hiyo.

 Tatu Haji na John Pilly ni wakazi wa Mlandizi ambao wanaishukuru Serikali kwa ajili ya gari hilo litakalosaidia kuhudumia wagonjwa kwa haraka.

 







Club News Editor Julieth Ngarabali

Comments

Popular posts from this blog

RC PWANI AONGOZA WAKAZI PWANI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

BARAZA LA MADIWANI KIBAHA MJINI LAMPONGEZA MKURUGENZI WAKE KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA SAMBAMBA NA KUONGEZA MAPATO.

RAIS SAMIA ATANGAZA KIBAHA MJINI KUWA MANISAPAA,MBUNGE KOKA AFURAHIA ASEMA KIBAHA ITANG'AA