MAKONDA AFICHUA SIRI MAANDAMANO CHADEMA
KATIBU wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa chama cha Mapinduzi (CCM)Paul Makonda amefichua siri ya maandamano ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yaliyopangwa kufanyika wiki ijayo kuwa ni njia anayotumia mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe kukwepa uchaguzi wa ndani.
Makonda amebainisha hayo alipokuwa katika ziara yake ya siku moja Mikoa ya Dar es Salam na Pwani ambapo alitumia nafasi hiyo kuzungumza na wananchi kwa kutatua kero zao mbalimbali zikiwemo za migogoro ya ardhi.
“Mimi ninafahamu hii taarifa na nimeitoa kwa mtu wa ndani sana kumbe kuna uchaguzi wa ndani ya chama,Katibu wa chama hicho John Mnyika ameamua kumbeba Mbowe kwasababu mwenyekiti huyo amegundua hawezi kumshinda Makamu wake Tundu Lissu,” anasema Makonda
Amesema taarifa alizonazo ndani ya chama hicho wanalalamika kwanini Mnyika anaungana na Mbowe kumhujumu Tundu Lissu akidai maandamano hayo yametengenezwa ili yamsaidie Mwenyekiti aonekane kuna jambo kubwa la kitaifa analipambani, halafu tarehe za uchaguzi zibadilishwe ili aendelee kushikilia nafasi hiyo.
Mwenezi Makonda amemshauri Mbowe ambaye anamuita kaka yake kuruhusu uchaguzi ufanyike na kuachana na mambo ya maandamano, huku akijivunia namna ambavyo CCM inasimamia Demokrasia..
Kadhalika ameishangaa CHADEMA kuitisha maandamano huku Makamu mwenyekiti wa chama hicho akiwa Ivory Coast akishuhudia mashindano ya mpira ya AFCON.
Kuhusu chaguzi zijazo
Akizungumzia kuhusiana na chaguzi zijazo amesema, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani watapimwa kwa kazi wanazofanya na sio kwa maneno au kujipendekeza kwa viongozi.
Amesema kuwa wasiofanya kazi taarifa zao zitapelekwa kwa Mwenyekiti wa CCM Dkt Samia Suluhu Hassani kwamba hawafai kupewa nafasi ya kugombea tena mwaka 2025.“Awamu hii tutawapima wawakilishi, Wabunge na Madiwani namna gani wanatatu changamoto za wananchi wao na jinsi gani wako mstari wa mbele kukijenga chama cha Mapinduzi,”.
“CCM hii ya Dkt Samia na mimi nikiwa msemaji na nishasema tangu nakabidhiwa ofisi sitabeba mzigo kila mtu atabeba mzigo wake,” anasema.
Hapa nchini Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika mwaka huu huku ukifuatiwa na Uchaguzi mkuu ambao utafanyika 2025.
Comments
Post a Comment